Dar es Salaam. Baadhi ya wadau, wakiwamo wa masuala ya sheria wamekuwa na maoni tofauti kuhusu kurejeshwa Jiji la Dar es Salaam, wakitaka sheria ya mamlaka za Serikali za mitaa ziwe na nguvu zaidi.
Ikiwa ni zaidi ya miaka miwili tangu Februari 24, 2021 jiji hilo lilipovunjwa, Oktoba 24, 2024 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa alielekeza mchakato wa uanzishaji wa Mamlaka ya Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam uanze ili kuratibu maendeleo yote yanayofanyika kwenye halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam.
Wakili Jebra Kambole amesema ni wakati muafaka kwa Bunge kuifanyia maboresho Sheria ya Serikali za Mitaa kupunguza mamlaka kwa kiongozi kuamua atakavyo.
“Bunge lifanye mabadiliko na kutoa mwongozo mzuri wa ugawaji wa maeneo, ikiachwa kama ilivyo hatutapiga hatua. Leo, unaweza ukawa na Rais wa namna hii, kesho utampa mwingine ana hulka tofauti na mtangulizi wake,” amesema.
Kambole amelitaka Bunge kutoa mwongozo utakaowezesha ugawaji wa maeneo kuwa ule unaopiga hatua za maendeleo.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe ameitaka Serikali kuangalia namna ya kuboresha sheria ili kutoa mamlaka makubwa kwa Serikali za mitaa.
“Uzoefu uliopo Serikali Kuu ndiyo yenye nguvu zaidi ya kufanya mabadiliko inavyotaka bila kuhusisha mamlaka za chini. Hii inatokana na Serikali za mitaa kunyang’anywa vyanzo vya mapato na mwisho wa siku hakuna mamlaka ya wananchi,” amesema.
Wangwe amesema sheria ziboreshwe ili kugatua madaraka kwenda Serikali za mitaa.
“Haya mabadiliko unayoyaona kila mara yanatokea kwa sababu mamlaka za chini hazina nguvu, zimehamia Serikali kuu ambako kiongozi anaweza kuamua kubadilisha anavyotaka,” amesema alipozungumza na Mwananchi Novemba 5, 2024.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Lugome amesema uamuzi wa kulivunja Jiji la Dar es Salaam ulikuwa sahihi kwa sababu kulikuwa na mwingiliano wa majukumu na mgongano mkubwa wa masilahi kati ya iliyokuwa halmashauri ya jiji na halmashauri za manispaa.
“Kulikuwa na gharama kubwa za kuwahudumia viongozi wa jiji na manispaa kiasi kwamba, mapato mengi yalitumika kwenye uendeshwaji wa ofisi kuliko shughuli za maendeleo. Hakukuwa na mpaka wa wazi wa kimaeneo kati ya jiji na manispaa.
“Ilikuwa siyo rahisi kusema Jiji la Dar es Salaam linaishia hapa na halmashauri za manispaa zinaishia hapa, ilikuwa mkanganyiko. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alikuwa na wakati mgumu wa kutenganisha mipaka ya majukumu yake na yale ya halmashauri,” amesema Lugome.
Pia, amesema uamuzi wa hayati Rais John Magufuli ulihitaji kuboreshwa zaidi na siyo kufutwa kwa kuwa tatizo kubwa lilikuwa mgawanyo wa eneo lililotakiwa kuwa la jiji, yaani Manispaa ya Ilala.
“Eneo hilo lilikuwa linaenda hadi Pugu na kuacha maeneo ya Oysterbay, Masaki, Magomeni, Kinondoni, Mwananyamala, Kijitonyama, Ubungo kuwa nje ya eneo la jiji halafu Pugu inakuwa ndani ya jiji,” amesema.
Februari 24, 2021 hayati Rais Magufuli aliivunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, akaipandisha hadhi Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kuwa jiji.
Magufuli alitangaza kulivunja jiji hilo wakati wa uzinduzi wa Daraja la Kijazi lililopo Ubungo, akieleza Ilala itachukua sehemu ya umiliki wa zilizokuwa mali za Jiji la Dar es Salaam.
Siku hiyohiyo taarifa ya kuivunja halmashauri hiyo ilitolewa na aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Dk Selemani Jafo, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Viwanda na Biashara.
“Aliyekuwa mkurugenzi wa Ilala, ndiye atakayekuwa mkurugenzi wa jiji na meya wa Ilala na naibu wake ndio watakaokuwa mameya wa Jiji la Dar es Salaam,” alisema Dk Jafo.
Katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari, Dk Jafo alisema Rais Magufuli alitumia mamlaka yake chini ya kifungu cha 84 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka ya Miji) Sura ya 288 kufanya mabadiliko hayo.
Dk Magufuli alisema huwezi kuwa na manispaa zinazowakilisha maeneo, halafu kukawa na jiji ambalo halina maeneo yoyote.
Sababu nyingine alisema ni kuwa na madiwani wa jiji ambao wanachangiwa fedha, lakini miradi ya maendeleo hakuna, wanakula posho na hawakuchaguliwa na watu.
Kwa mujibu wa Dk Magufuli, kuliko kuwa na madiwani wa jiji wanaowakilisha manispaa wanazotoka na kutengewa fedha za posho na uendeshaji, ni bora zipelekwe kwenye miradi ya maendeleo ikiwamo ya barabara.
Alitoa mfano akieleza Mwanza na Dodoma ni majiji, lakini kuna maeneo yanayowakilisha jiji na kwa Dar es Salaam aliona Ilala ndiyo inafaa kuwa jiji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Mohamed Mchengerwa ameelekeza mchakato wa uanzishaji wa Mamlaka ya Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam uanze mara moja ili kuratibu maendeleo yote yanayofanyika kwenye halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam.
Amesema mkoa huo unatakiwa kuwa kioo cha nchi na wageni wote wanapokuja wanaiona sura ya Tanzania.
“Mkoa huu unatakiwa kuwa na chombo kinachoratibu maendeleo ya mji huu na kuhakikisha mipango yote ya maendeleo inayofanyika hapa inakuwa na muunganiko ili kuleta ile sura tunayoitegemea,” amesema.
Amesema kupitia Mradi wa Uendelezaji Mkoa Dar es Salaam (DMDP) awamu ya pili kuna miradi mikubwa inayotekelezwa ikiwamo uboreshaji wa miundombinu ya barabara na uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi.
“Miradi mikubwa kama hii ikiachwa kwenye halmashauri inaweza isijiendeshe, hivyo uwepo wa jiji ni muhimu kuisimamia na kuhakikisha inaungana na jitihada zingine za maendeleo zinazofanywa kwenye halmashauri za mkoa huu,” amesema Mchengerwa.
“Nataka hii Dar es Salaam iwe ya viwango na ubora na ukuaji wake uratibiwe kwa taratibu maalumu na si kukua kiholela tu, hii itafanya hadhi ya Dar es Salaam isikue haraka na kuwa na hadhi ya kimaraifa.”
Aliyewahi kuwa mbunge wa Ubungo mwaka 2015 hadi 2020, Saed Kubenea amesema muundo wa sasa wa jiji hilo haupo kokote duniani.
Kubenea aliyekuwa mjumbe wa jiji zamani, amesema Jiji la Dar es Salaam liliwakilishwa na halmashauri zote tano za Ilala, Temeke, Ubungo, Kigamboni na Kinondoni.
Amesema kwa mfumo wa sasa linaishia Daraja la Selander, upande wa Barabara ya Bagamoyo ukitokea katikati ya mji.
“Kuanzia ubalozi wa Ufaransa, Mwenge yote hiyo, haipo ndani ya jiji, upande wa Barabara ya Kilwa, jiji linaishia zilipo ofisi za Puma. Kuanzia Mivinjeni kuendelea Halmashauri ya Temeke.
“Ukija Ubungo, jiji linaishia Jangwani, na ukivuka daraja la Jangwani kupanda juu ile ni Halmashauri ya Kinondoni,” amesema.
“Ilala haikupaswa kupandishwa hadhi kuwa jiji, haikuwa sahihi badala yake ilipaswa kubaki manispaa. Tunaweza kurudisha mfumo wa zamani wa halmashauri, lakini suala la eneo la utawala likazingatiwa ili kuleta ufanisi,” amesema.
Mjumbe wa zamani wa Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam, Boniface Jacob amesema jiji linaporejea muundo mzuri ni uleule wa shirikisho.
Jacob maarufu Boni Yai, ambaye ni meya wa zamani wa manispaa za Ubungo na Kinondoni, amesema endapo jiji linarejea, kila halmashauri iachwe na ardhi na watu, badala yake jiji liwe waratibu wa halmashuri zote.
Mjumbe wa zamani wa jiji hilo, Patrick Assenga amesema: “Nilishangaa kwa nini waliamua kulivunja jiji. Huwezi kuchukua manispaa moja ndiyo ukasema iwe jiji hicho kitu hakiwezekani, mfano ukivuka daraja la Jangwani kuja Magomeni si Jiji la Dar es Salaam.
“Kama wameamua kulirejesha basi watakuwa wamefikiri vizuri, kikubwa wazingatie muundo uwe uleule wa awali,” amesema Asenga aliyewahi kuwa diwani wa Tabata.
Mbunge wa Mbagala, Abdallah Chaurembo amepongeza uamuzi wa kurejeshwa jiji hilo akieleza itafungua milango ya ushirikiano na majiji makubwa duniani likiwamo la Hamburg nchini Ujerumani.
“Unajua miaka ya nyuma tulikuwa na ushirikiano mzuri na Jiji la Hamburg ambalo liliwahi kutuletea magari nchini, sasa kwa urejeo huu wa jiji utakwenda kuchochoe maendeleo makubwa ya ushirikiano.
“Hata huu mradi mkubwa DMDP uasisi wake ulianzia katika vikao vya Jiji la Dar es Salaam, hivyo hatua ya kurejeshwa itakwenda kufufua miradi mingi iliyokwama,” amesema Chaurembo aliyewahi kuwa mjumbe wa Baraza la Madiwani la Jiji la Dar es Salaam mwaka 2015/20.
Mhadhiri wa UDSM, Kitivo Sayansi na Jamii, Dk Zablon Kengera amesema kwa jinsi jiji lilivyokuwa kubwa ni lazima ligawanywe kwenye mamlaka ndogo-ndogo ili kufikisha kwa urahisi huduma kwa wananchi.
Kwa mujibu wa tovuti ya Jiji la Dar es Salaam, jiji hilo lilikuwa na meya, naibu meya, mameya wa halmashauri zote tano za Dar es Salaam, wajumbe (madiwani watatu kutoka kila halmashauri kwa kuzingajia uwiano wa vyama na jinsia).
Pia, lilikuwa na mbunge mmoja kutoka kila halmashauri, huku meya na naibu meya wakichaguliwa katika mkutano wa madiwani wote wa kata za Jiji la Dar es Salaam katika kikao cha kwanza baada ya uchaguzi mkuu.
Mwaka 1996, Serikali Kuu iliivunja Halmashauri ya Jiji na kuunda Tume ya Jiji la Dar es Salaam, kwa Tangazo la Serikali Na. 110 na 111 la Juni 28, mwaka 1996.
Tume ya Jiji ilifanya kazi kwa kipindi cha miaka minne, mwaka 2000 Serikali iliunda mamlaka nne za Serikali za Mitaa za Mkoa wa Dar es Salaam kwa sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Na. 8 ya Mwaka 1982, kama ilivyo rekebishwa kwa sheria na. 6 ya mwaka 1999.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam linaundwa na Madiwani 26 kutoka katika Manispaa tano.