HELLO MR.RIGHT MSIMU WA 06 WAZINDULIWA RASMI

ONESHO la Hello Mr Rights kuja na mpango wake baada ya miaka 10 ijayo ya onesho hilo wanatamani kuunganisha vijana wengi wanaotaka wenza na ikiwezekana kuweka historia mpya ya kuwafungisha ndoa za pamoja.

Akizungumza na Wanahabari Jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa onesho hilo msimu wa sita, Mkurugenzi wa Masoko na Maudhui wa Startimes Media David Malisa amesema nia yao sio tu kuwaunganisha vijana kupata wenza sahihi bali wanatamani kuona wanafika mbali kwa kufunga ndoa na kutengeneza familia.

“Tangu tumeanza jukwaa hili tumetengeneza sio chini ya mahusiano ya watu 12, wapo walioendelea wana watoto, wengine wana ndoa lakini tunataka tufanye kitu kimoja kikubwa sana hapo baadaye, harusi ya pamoja,”alisema.

Aidha katika msimu huu wa sita vijana zaidi ya 400 wa kike na 800 wa kiume waliomba kushiriki katika jukwaa hilo kwa ajili ya kutafutiwa wenza lakini wamechagua wachache na wengine watawapa nafasi siku nyingine.

“Niwaambie watazamaji wetu wasiache kulipia vifurishi kwasababu watafurahia burudani na kujifunza namna wengine wanavyounganishwa kupata wenza, sisi ni mabingwa na shoo zenye uhalisia kupitia Chaneli ya ST Bongo,”alisema.

Onesho hilo msimu huu limepata ongezeko la watangazaji wawili wapya ambao ni Swalehe Nassoro ‘Dk Kumbuka’ aliyesema amekuja kwa ajili ya kuwapa elimu washiriki namna gani ya kufanya uchaguzi sahihi utakaosaidia kupata watu sahihi wa maisha yao.

“Wameona Kumbuka tukimweka hapa ana kitu cha ziada ambacho tunakihitaji, mimi nimekuwa mkufunzi mkubwa wa suala la mahusiano, niko hapa kuwapa elimu, hekima, mafunzo, busara na namna ya kumsoma mtu,”alisema.

Kwa upande wake Aaliyah Mohamed amesema kuna baadhi ya watu wanakosa wenza sahihi labda wamehangaika sana na wengine wameumizwa akisema malengo ya kipindi hicho ni kutengeneza mahusiano bora.


Related Posts