Kigogo kiwanda cha Dangote matatani

Dodoma. Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hassan Mtenga amehoji kwa nini Serikali inapata kigugumizi cha kumuondoa Meneja Rasilimali Watu wa Kiwanda cha Dangote ambaye ni raia Nigeria wakati nafasi hiyo inatakiwa kuwa ya Mtanzania licha ya kulalamikiwa miaka mitatu sasa.

Mtenga amehoji swali hilo leo Jumatano Novemba 6, 2024 wakati alipokuwa akiuliza maswali bungeni jijini Dodoma.

Amehoji ni kwa nini Meneja Rasilimali Watu wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote Mtwara ni Raia wa Nigeria wakati Sheria inamtaka awe Mtanzania.

Pia, katika swali la nyongeza, Mtenga amesema takribani miaka mitatu meneja huyo amekuwa katika kiwanda hicho na kuhoji ni kigugumizi gani Serikali inapata cha kumuondoa meneja huyo.                                                

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amesema malalamiko yanayotolewa na Mbunge huyo yalishafika katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu na kufanyiwa kazi.

Amesema kwa kuzingatia Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni, Sura 436 na Sheria ya Uwekezaji Tanzania, Na.10 ya Mwaka 2022, ofisi ilifanya ukaguzi maalumu katika kiwanda hicho Septemba 23 na 24, Septemba, 2024.

Amesema ukaguzi huo ulilenga kujiridhisha na ukweli wa malalamiko haya na utekelezaji wa sheria za kazi kwa ujumla. Serikali ilithibitisha malalamiko hayo.

Amesema kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali, tunaendelea kushughulikia suala hili na pindi litakapokamilika, hatua stahiki zitachukuliwa.

Kuhusu kigugumizi Katambi amesema mbunge huyo amefuatilia jambo hilo kwa muda mrefu na wao walibaini kuwa kuna uvunjifu wa sheria.

Amesema Serikali haina kigugumizi ila kilichobainika pia kulikuwa na makosa ya jinai yalitendeka na kwamba tayari polisi wanaendelea kufanya uchunguzi.

“Sambamba na mamlaka ya uhamiaji pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu tunaendelea kuyashughulikia lakini tuliona kama tunachukua hatua maana yake kuna makosa ya jinai ambayo kama alikuwa ameyatenda ina maana sheria itakuwa haijatenda haki, hasa wale ambao walikuwa wametendewa,” amesema.

Amesema imebidi kuhakikishe mashauri yote na tuhuma zote (ambazo hakuzitaja), zimefanyiwa kazi.

Related Posts