Kirusi kilichoichinja ANC kimeiua BDP Botswana

CCM inaendelea kuwa chama kikongwe kilicho salama madarakani. Hupepesuka kwa nadra, lakini mwisho hubaki imara. Inaonekana CCM ina kinga imara dhidi ya ugonjwa unaoviua vyama vyenye kuitwa “vya ukombozi” Afrika.

Botswana Democratic Party (BDP), chama cha ukombozi Botswana, kilichoasisiwa na Baba wa Taifa hilo, Seretse Khama kikalindwa na mwanasiasa mwenye heshima kubwa, Ketumile Masire pamoja na mshindi wa Tuzo ya Mo Ibrahim, Festus Mogae, kimeelekezwa kaburini.

Ugonjwa ulioiua BDP, ndio ambao chupuchupu uipeleke kaburini African National Congress (ANC), Afrika Kusini. Mgawanyiko wa ndani ulisababisha chama kibaki uchi. Kama Mokgweetsi Masisi na Ian Khama BDP, kama Jacob Zuma na Cyril Ramaphosa ANC.

Yupo mtu aliwahi kupendekeza kuwa usalama wa CCM umo ndani ya “Utanzania”. Neno Utanzania linakuwa kwenye masikio kwa sababu tafsiri yake halisi ni unafiki. Tanzania, watu huzungumza na hata kupinga pembeni, lakini kwenye vikao rasmi au hadharani huunga mkono wasiyokubaliana nayo.

Mathalan, kipindi cha urais na uenyekiti CCM wa Dk John Magufuli, sauti za chini kwa chini kumpinga ndani ya chama zilikuwa nyingi, ila hadharani walimuunga mkono. Ndivyo ilivyokuwa mwaka 2015, Edward Lowassa alipohama CCM. Wengi walibaki CCM Kitanzania, ila mioyo yao ilihama naye.

Magufuli alilijua hilo, ndiyo maana alipokabidhiwa uenyekiti CCM mwaka 2016, hakupitisha wiki, chama hicho kiliwavua uanachama viongozi waliodaiwa kusaliti, wengine wakaonywa. Waliofukuzwa waliomba msamaha, wakarejeshwa kundini.
Vyama vingine, unapotokea mgawanyiko unatikisa na kuchimba ndani. Ndivyo ilivyokuwa katika anguko la Kenya African National Union (Kanu), vilevile United Democratic Front (UDF), Malawi. Ugonjwa ni mgawanyiko wa ndani.

Haisahauliki hadithi ya aliyekuwa mbunge wa Kishapu (CCM), Fred Mpendazoe, alijiuzulu ubunge kuelekea Uchaguzi Mkuu Tanzania 2010. Akahamia Chama Cha Jamii (CCJ). Baadaye Mpendazoe alitimkia Chadema, akisema alibadili gia angani. Mpendazoe alifichua kwamba kuhama kwake ulikuwa mpango wa wengi CCM, akiwemo Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta. Baadaye akajikuta ni yeye peke yake aliyehama. Bila shaka, wengine walibaki CCM kwa shingo upande.

Kanu, wanachama wengi waandamizi walimgomea aliyekuwa kiongozi wao, Rais Daniel Moi, aliyeng’ang’aniza kumsimamisha kijana wakati huo, Uhuru Kenyatta, awe mgombea urais. Waandamizi wengi kwa hasira, waliondoka Kanu, wakaenda kuunda muungano wa National Rainbow Coalition. Kanu ikafa.

Malawi, ina simulizi sawa na Botswana. Aliingia rais mpya, Bingu wa Mutharika, ambaye alianza mapambano dhidi ya mtangulizi wake, Bakili Muluzi. Shida ikawa, Bingu alikuwa na nguvu serikalini, Muluzi chama (UDF). Bingu akaanzisha chama kipya, Democratic Progressive Party (DPP). UDF ikawa mahututi.
Botswana ilivyokuwa

Aprili Mosi, 2018, Masisi alikula kiapo kuanza kuiongoza Botswana. Ilikuwa baada ya Ian Khama kukamilisha mihula yake miwili madarakani. Hata hivyo, kutoka Aprili Mosi, 2018 hadi Oktoba 23, 2019, Uchaguzi Botswana ulipofanyika, tayari chama tawala, BDP, kilikuwa kimeshameguka. Muda mfupi baada ya kukaa pembeni, Ian Khama alimsakama Masisi kwa uongozi wa kidikteta. Halafu zikafuata nyakati za kutunishiana mbavu. Hatimaye, Ian Khama aliamua kuhama BDP, akawa kichocheo cha kuanzishwa chama kipya, Botswana Patriotic Front (BPF).

Ian Khama, mtoto wa Baba mwasisi wa Botswana, Seretse Khama, alipiga kampeni ya kuhakikisha Masisi hachaguliwi. Kinyume na mapambano yake, Masisi alichaguliwa na kuongoza muhula wa kwanza. Ian hakuwa na jinsi, alikimbia nchi, akaenda kuweka makazi Afrika Kusini.

Muhula mzima wa Masisi kuiongoza Botswana haukuwa salama kwa Ian na familia yote ya Khama, kwa sababu hata mdogo wa Ian, Tshekedi Khama ambaye alishakuwa Waziri wa Mazingira, Uhifadhi, Maliasili na Utalii, wakati wa urais wa kaka yake, naye alikimbilia Afrika Kusini, kisha ubunge wake ulitenguliwa.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Botswana 2019, Tshekedi alihama BDP, akajiunga na BPF. Alishinda ubunge. Hata hivyo, mazingira ya kisiasa baada ya Masisi kuingia madarakani, yalimwelemea, akahama nchi. Nyuma yake, alifukuzwa ubunge kwa utoro.
Masisi alimgusa pabaya Ian, kwa kumfutia stahiki zake za kiupendeleo kama rais mstaafu. Serikali ya Masisi ilimfungulia Ian mashitaka ya kumiliki bunduki isivyo halali na kuzisambaza, kutakatisha fedha haramu na kupokea mali za wizi.

Wafanyabiashara walioonekana kuwa karibu na Ian, walifunguliwa mashitaka ya ufisadi na kusuka mipango ya kumpindua Masisi. Mahakama ya Juu Botswana ilitupilia mbali mashitaka hayo, kwa kile ambacho ilieleza kuwa ilikuwa kesi ya kutunga.

Wakati Masisi akipambana na Ian, ambaye hakupaswa kuwa mpinzani wake kwa sababu haruhusiwi kikatiba kurudi madarakani muhula wa tatu, upande mwingine alikutana na zahama la mdororo wa ukuaji wa uchumi.

Pato la Taifa (GDP), limetuama bila ongezeko lolote, wakati Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), limetoa ripoti yenye kuonesha uchumi wa Botswana unakua kwa asilimia moja, wakati mwaka 2022 ukuaji wake ulikuwa asilimia 5.5, vilevile asilimia 2.7 mwaka 2023.

Hali hiyo ya mdororo wa kiuchumi, inasababishwa kwa sehemu kubwa kuporomoka kwa mauzo ya almasi. Botswana, nchi ambayo ilikuwa ikitoa ahadi nzuri ya kiuchumi kutokana na usafirishaji wa almasi, hadi Machi 2024, mauzo yake yalishuka kwa asilimia 42.

Matokeo ya jumla kutokana na mtikisiko huo wa kiuchumi, kumekuwa na janga la ukosefu wa ajira. Mwaka 2019 tatizo la ajira lilikuwa asilimia 21, huku robo ya kwanza ya mwaka 2024, hali imefikia asilimia 28. Wakati huohuo, kundi rika la vijana wenye umri kati ya miaka 15 mpaka 24, limepanda kutoka asilimia 36 mwaka 2019 hadi asilimia 49 mwaka 2024.

Mitaani hali ni mbaya. Badala ya wananchi kushuhudia Masisi akipambana kuweka sawa hali ya kiuchumi, wanashuhudia akitumia nguvu nyingi kupambana na mtangulizi wake. Uchaguzi Mkuu Botswana uliofanyika Oktoba 30, 2024, wananchi wa Botswana wakaamua kuishangaza dunia.

Kilichokuwa chama cha upinzani, Umbrella for Democratic Change (UDC), kinachoongozwa na Duma Boko, kimevuna viti 36 kati ya 61, Botswana Congress Party (BCP), kimepata viti 15, BPF kimevuna viti vitano, BDP viti vinne, kiti kimoja kimechukuliwa na mgombea huru.

Related Posts