Dar/Mikoani. Kilio cha ukosefu wa huduma ya maji kimeendelea kusikika nchini, huku baadhi ya wananchi wakiandamana kupaza sauti wakitaka mamlaka husika kutatua kero hiyo.
Wakati wananchi wakilalama kukosa maji, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameshachukua hatua kadhaa kutatua changamoto hizo ikiwamo kuwasimamisha watendaji wa mamlaka za maji na kutembelea maeneo ya uzalishaji wa maji nchini.
Hata hivyo, katika maeneo mengine wananchi wanafurahia na kupongeza kwa kutekelezwa miradi ya maji.
Wakazi wa Mbezi Msakuzi wilayani Ubungo Mkoa wa Dar es Salaam, wameandamana leo Jumatano Novemba 6, 2024 kwenda ofisi za Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) Wilaya ya Ubungo kulalamikia adha ya kukosa maji.
Wengi wakiwa wanawake waliobeba mabango na ndoo tupu, wameilalamikia Dawasa wakidai wamekuwa wakipewa ahadi za uongo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye maandamano yaliyofanyika Msakuzi Kwalubaba, Upendo Mwankenja amesema:
“Tunaambiwa kuna kumtua mama ndoo kichwani, tunaona tu kwenye TV (televisheni) lakini hatuoni maji. Sijui hapa ni Dar es Salaam au ni wapi, tumechoka. Watu wanachota maji bondeni huko maji yana ugonjwa wa UTI (maambukizi ya njia ya mkojo).”
Stella Mwamba amesema maji wanayotumia ni machafu na hatari kwa afya zao.
“Tunaoga maji machafu, tunapikia maji machafu, tunaumwa matumbo kila siku kwa sababu maji ni machafu. Ukienda hospitali daktari anasema maji machafu, kwa mfano wiki iliyopita niliharisha wiki nzima ni kwa sababu ya maji machafu.
“Maji tunayotumia ni ya bondeni yanayotumika kumwagilia mchicha, maji yenyewe ya kijani, tunayaacha kidogo lakini uchafu hauishi, ukitaka kununua ya bomba ndoo Sh600. Hiyo ni halali? Tanzania hiihii, Dar es Salaam hiihii, Mto Ruvu uko hapo karibu kwa nini tusipate maji?” amehoji.
Meneja wa Dawasa Ukanda wa Kimara, Mhandisi Edson Robert amesema eneo la Msakuzi wanatekeleza mradi ulioanza mwaka wa fedha uliopita wa 2023/24.
“Nikiri mbele yenu, hatukufanikiwa kuumaliza kwa asilimia 100. Ninavyoongea nanyi mpaka muda huu, kuanzia eneo la Serikali ya mtaa kurudi eneo la Kwa Mkapa, kurudi eneo la Shule ya Makamba, kurudi mpaka Machimbo huduma ya maji imeshafika kwa maana chanzo chetu cha maji kilikuwa kimoja,” amesema na kuongeza awali hawakuweza kulaza mtandao wa mabomba kwa sababu hakukuwa na chanzo cha maji.
“Chanzo chetu kuelekea huku ni tangi la Mshikamano ambalo Serikali imeweka zaidi ya Sh4.8 bilioni, tangi limekamilika la lita za ujazo milioni sita. Baada ya kupata tangi, kazi ya ugawaji itaanza. Maji hayaruki mtaa, yanatoka eneo moja kwenda lingine.
“Tumeanza kutoa maji kwenye tangi la Mshikamano tumeelekea Barabara ya Machimbo, tumesogea mpaka Freetown, tumetandaza bomba la nchi nane kuja mpaka Makamba, kutoka hapo hadi Serikali yenu ya mtaa. Mpaka hapa Kwalubaba tumeshalaza bomba la nchi sita, kazi iliyobakia ni ya ugawaji, yaani bomba kwenda kwa wateja. Tusingeweza kuruka kule kuja kuanzia mwisho,” amesema.
Baada ya maelezo hayo, Mzee Bozo amesema maneno yamekuwa yakitolewa kila mara.
“Hayo unayotuambia ni maneno ya siasa, sisi tuna miaka mitatu mnatuahidi tu, ina
maana miaka mitatu hakuna bajeti? Huko kote unasema maji yamefika, hapa kwetu lini?” amesema.
Mhandisi Robert akijibu swali hilo amesema: “Nimewaambia mradi huu tumeanza kutekeleza, kwa hiyo kabla ya mwezi wa 12 (Desemba) utakuwa tayari na hii kazi ni ya kumalizia siyo ya kuanza.”
Mbali ya hayo, ikiwa imepita miezi minne tangu Serikali iliposema itajenga visima katika eneo la Mbezi Msumi wilayani Ubungo, bado havijaanza kutumika.
Mwananchi iliripoti kero ya maji katika mtaa huo Juni 2024, baadhi ya wananchi walieleza wamekuwa wakitumia saruji kusafisha maji machafu ya mtoni.
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew alilazimika kutembelea mtaa huo kusikiliza kero za wananchi akaeleza kwa kuwa mradi wa maji utachelewa, watachimbiwa visima vya maji ya chumvi ili kupoza tatizo hilo, jambo ambalo hawakuafiki.
Hata hivyo, katika eneo hilo Mwananchi imeshuhudia visima vimechimbwa ila bado havijakamilishwa.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Mkama Bwire alipotafutwa na Mwananchi hivi karibuni alisema: “Visima tumeshachimba viwili na sasa hivi tuko kwenye hatua ya kuviendeleza ili vianze kutoa maji, lakini wakati vinaendelea vile kuna sehemu tumepeleka maji ya dharura kwa kuweka matangi na tunaendelea kujenga visima ili kuweka mfumo.”
Alisema Msumi kuna matangi manne yaliyowekwa maeneo tofauti.
Hata hivyo, alisema kulingana na maji yaliyopatikana haitawezekana kujenga mifumo mikubwa ya kuyasambaza eneo hilo.
Kutokana na hali hiyo amesema kwa sasa wana mpango wa kutoa maji Tegeta A ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa Mbezi Msumi.
Akizungumzia adha hiyo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbezi Msumi, Ismail Mbinda amedai alishindwa kwenye kura za maoni ndani ya chama chake cha CCM kutokana na malalamiko ya wananchi kukosa maji.
“Nimeshidwa kutetea nafasi yangu kutokana na malalamiko ya wananchi juu ya huduma hizo, maana imekuwa kila siku ni kuzungumza tutaleta kitu fulani siku fulani, sasa wananchi wamefika mahali wamechoka,” amedai.
Kero ya maji si kwa maeneo hayo pekee
“Huku kwetu Makabe Kavimbirwa tumeshakata tamaa kabisa, ni mwendo wa kununua tu maji, kila mtu anapambana na hali yake,” ameandika Frank Tarimo katika mtandao wa kijamii wa Whatsapp.
Mkoani Kilimanjaro, baadhi ya wananchi katika Kata ya Msaranga, Manispaa ya Moshi wamelalamikia uhaba wa maji unaowalazimu kuamka usiku wa manane kutafuta huduma hiyo.
Mkazi wa Msaranga, Dotto Shayo, amesema imekuwa ni kero ya muda mrefu na wamekuwa wakitoa malalamiko kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (MUWSA) lakini changamoto hiyo haijapatiwa ufumbuzi wa kina.
“Changamoto ya maji imekuwa ni tatizo kubwa kwetu, inafika mahali mtu ukisahau kuamka saa 10 alfajiri ukaamka saa 11 maji hupati bombani, hali hii imekuwa kero ya muda mrefu na haipatiwi ufumbuzi licha ya kwamba MUWSA wako hapahapa mjini,” amesema.
Hellena Mlunga, amesema kila siku huamka saa tisa usiku kwenda kuchota maji bombani kutokana na changamoto iliyopo.
Alipotafutwa ofisa uhusiano wa mamlaka hiyo, Florah Nguma ametaka apewe muda wa kufuatilia changamoto hiyo.
Wakati maeneo mengine wakilalamika kuhusu ukosefu wa maji ambao pia unaelezwa unachangiwa na kupungua kina cha maji kwenye vyanzo husika, wananchi wengine wanaendelea kufurahia huduma hiyo.
Hivi karibuni Serikali imetoa Sh4.8 bilioni kutekeleza mradi wa maji wa Mto Ilunga wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 10 kwa siku kwa lengo la kuwaondolea adha ya maji zaidi ya wananchi 110,000 wa vijiji vitatu na kata nne za Wilaya ya Mbeya waliokosa huduma hiyo tangu nchi ipate uhuru. Vijiji vilivyopata huduma ni vya Ihombe, Itimba na Idungumbi.
Mradi huo umetekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya- UWSA).