Kuelekea uchaguzi Serikali za mitaa viongozi wa dini waguswa

Mwanza. Zikiwa zimesalia siku 21 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa nchini, viongozi wa dini wametakiwa kujitenga na kutoonyesha upendeleo kwa vyama vya siasa wakati wakihamasisha wananchi kushiriki katika uchaguzi huo.

Uchaguzi wa serikali za mitaa umepangwa kufanyika Novemba 27, 2024, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza siku hiyo kuwa mapumziko ili wananchi waliojiandikisha waweze kujitokeza kupiga kura na kuchagua viongozi wa ngazi za mitaa, vijiji, na vitongoji.

Wito huo umetolewa leo Jumatano, Novemba 6, 2024, jijini Mwanza na Askofu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, Oscar Lema kwenye kongamano la viongozi wa dini lililoandaliwa na Shirika la Kivulini kwa lengo la kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi.

Askofu Lema amesisitiza kuwa viongozi wa dini wanapojihusisha hadharani na siasa kwa kuonyesha upendeleo, wanaleta mgawanyiko miongoni mwa waumini na kuathiri maamuzi ya wapiga kura.

Amesema, “Katika Biblia, Mithali 18:18 inasema ‘Kura hukomesha mashindano,’ kwa hiyo ni muhimu kuwaandaa watu kwa mazingira mazuri ya kupiga kura ili kuepuka mashindano baada ya uchaguzi.”

Aidha, amewahimiza viongozi wa dini kuhamasisha wapiga kura na wagombea kukubali matokeo baada ya kutangazwa, akionya kuwa kutokubali matokeo kunaweza kusababisha machafuko.

Mchungaji Daudi Mtumayi ameongeza kuwa jukumu la viongozi wa dini si kuonyesha ushabiki kwa vyama, bali kuhamasisha waumini na wapiga kura kumtambua kiongozi sahihi atakayewaletea maendeleo.

Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke, ameunga mkono kauli hiyo akieleza kuwa kamati ya amani ya mkoa, inayojumuisha viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali, imeanza kutoa hamasa kupitia mahubiri ili kuwahamasisha wananchi kushiriki uchaguzi. Ameonya juu ya wagombea wanaotoa rushwa kwa wapiga kura, akisema kuwa kiongozi anayepata uongozi kwa njia ya rushwa hana nia ya kuleta maendeleo.

Johari Pearson, mkazi wa Mwanza, amesisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kurudi kwenye misingi ya imani, akisema kuonyesha upendeleo wa kisiasa hadharani kumeleta mgawanyiko kwa waumini na kuathiri uamuzi kwenye masanduku ya kura.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema serikali mkoani humo imejipanga kuhakikisha uchaguzi wa serikali za mitaa unafanyika kwa amani na utulivu, huku akionya kwamba mbinu za zamani za wagombea kushindwa na kutoroka na maboksi ya kura hazina nafasi tena katika uchaguzi wa sasa.

Mtanda amesema walitarajia kuandikisha wapiga kura 1,900,000 kwa mkoa wa Mwanza, lakini walioandikishwa ni 2,086,000, sawa na asilimia 106 ya lengo.

Pia, amekemea wagombea wanaotumia mbinu za rushwa kujaribu kuingia madarakani na kuwataka wote watakaoshindwa kukubali matokeo na kuacha vitendo vya kuvuruga uchaguzi.

“Wakati huu wa uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, tumejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uhuru na haki, tukizingatia kanuni na miongozo yote iliyowekwa,” amesema Mtanda.

Amesisitiza umuhimu wa wagombea kuwasilisha hoja zao kwa umma kwa njia za haki ili kuongeza ushawishi kwa wapiga kura, akibainisha kuwa viongozi wenye ushawishi wa kweli ni wale wanaochaguliwa kihalali na wananchi wenyewe. Mtanda pia alikumbusha umuhimu wa “4R” zilizoanzishwa na Rais Samia, zinazojumuisha maridhiano, uvumilivu, mageuzi, na kujenga taifa. Alisema, “Ndiyo maana Rais Samia alikuja na 4R – kama Chadema wanahoja zao na CCM hawazitaki, wakutane wamalize tofauti zao badala ya kuendeleza mivutano. Rais anasisitiza ustahimilivu wa kisiasa ili kujenga taifa letu.”

Kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), mwaka 2019, asilimia 70 ya wapiga kura walishiriki uchaguzi wa serikali za mitaa kutokana na hamasa kutoka kwa viongozi wa dini, jambo lililoongeza idadi ya wapiga kura. Utafiti wa mwaka 2021 wa Taasisi ya Afrobarometer ulionyesha kuwa asilimia 82 ya Watanzania wana imani na viongozi wao wa dini zaidi ya taasisi nyingine, ikiwemo serikali na vyombo vya habari.

Hii inaonyesha nafasi kubwa ya viongozi wa dini katika kuwahamasisha waumini wao kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi.

Related Posts