KUNA maswali? Ndivyo mashabiki wa Simba walivyokuwa wakihoji kwa furaha kwenye Uwanja wa KMC, wakati timu hiyo ikiikandika KMC kwa mabao 4-0 na kupanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiishusha Yanga, inayoshuka uwanjani jioni ya leo.
Mashabiki walikuwa wakiuliza kwa kejeli kutokana na mabao mawili ya kiungo mshambuliaji, Jean Charles Ahoua yaliyomfanya nyota huyo kutoka Ivory Coast kufikisha matano na kushika nafasi ya pili nyuma ya kinara Seleman Mwalimu wa Fountain Gate, huku Simba ikifikisha pointi 25 na mabao 21.
Mabao matano aliyofunga Ahoua ukichanganya na asisti nne alizotoa, yamemfanya awe mchezaji anayeongoza kuhusika katika mabao tisa, ambayo ndiyo mengi zaidi hadi sasa katika Ligi Kuu Bara ikiwa raundi ya 11 na ikienda mapumziko kupisha michuano ya kimataifa kwa timu za taifa.
Bao la kwanza likafungwa na kiungo mpya Awesu Awesu, ‘Kepteni Lucho’ katika dakika ya 25 kwa shuti kali akiwekewa pasi nzuri na Steven Mukwala, shambulizi lililotengenezwa na winga Ladack Chasambi aliyetangulia kuwakimbiza wachezaji wa KMC huku wekundu hao wakitumia pasi tatu tu kupika bao hilo.
Ahoua aliendeleza makali yake katika msimu wake wa kwanza kwenye soka la Tanzania, kwa kufunga bao lake la kwanza na la pili kwa Simba jana, kwa penalti katika dakika ya 38 kabla ya kuja kuongeza jingine katika kipindi cha pili na kuwapa furaha mashabiki wa klabu hiyo ambao kwa muda mrefu walikuwa hawajaishuhudia timu hiyo ikiwa kileleni.
Penalti ya bao la kwanza la Ahoua jana ilitokana na beki wake wa kulia, Shomari Kapombe kuangushwa kwenye eneo la hatari na kufunga kiufundi tuta hilo na la pili akalifunga katika dakika ya 69 akinufaika na makosa ya beki wa KMC, Ismail Gambo aliyeshindwa kutuliza mpira na kujikuta akimtengea njiani staa huyo aliyeenda kumtungua kipa Fabien Mutombora kiulaini.
Kwenye bao hilo la pili kuna tukio liliwakutanisha Shomari watatu akianza Shomari wa Simba aliyekuwa ameingia na mpira kwenye eneo la hatari, kisha beki wa KMC Rahim Shomari akamuangusha beki huyo wa wekundu kisha mwamuzi Shomari Lawi akaamuru iwe penalti.
Kipindi cha kwanza KMC haikuwa na nguvu yoyote kwenye lango la Simba ikishindwa hata kupiga shuti hata moja lililolenga lango lakini kipindi cha pili kilipoanza wakiwa nyuma kwa mabao 2-0 walirudi na nguvu na kufanya mashambulizi mazuri kuanzia dakika ya 50 -58 lakini wakakosa utulivu wa kuyatumia vyema.
Baada ya mashambulizi hayo Simba ikafanya mabadiliko mawili yaliyokuja kupika bao la nne ilipomtoa Awesu nafasi yake ikichukuliwa na Edwin Balua kisha akatoka Deborah Fernandez nafasi yake ikichukuliwa na Mzamiru Yassin.
Mabadiliko hayo yakalizaa bao la nne lililofungwa na Balua kwa shuti kali akitengenezewa na beki wake wa kushoto Valentin Nouma aliyepokea pasi kutoka kwa Mzamiru.
Sio tu kupanda juu ya msimamo ikiisubiri Yanga ambayo inacheza leo dhidi ya Tabora United, Simba kwa mabao hayo yameifanya timu kufikisha mabao 21 ikiwa ndio timu kinara kwa kuchana nyavu kwenye ligi msimu huu ikifuatiwa na Fountain Gate yenye mabao 20 kisha Yanga, Singida na Azam zikifuata na mabao yao 13 kila moja.
Ahoua ametua Tanzania msimu huu akitokea kuwa MVP wa Ligi Kuu ya Ivory Coast na taratibu ameanza kuichukua Ligi Kuu Bara kwenye himaya yake, akiwa ndiye mchezaji aliyefunika zaidi hadi sasa.
Jana baada kufunga mabao mawili na sasa kuwa amefikisha matano na asisti nne, mwamba huyo alikabidhiwa tuzo yake ya Nyota wa Mchezo baada ya mechi akifanya hivyo kwa mara nyingine.