Mastaa KenGold kikaangoni | Mwanaspoti

WAKATI wadau na mashabiki wa soka nchini wakiitabiria kushuka daraja Ken Gold kutokana na matokeo waliyonayo, uongozi wa timu hiyo umesema unaenda kufanya maamuzi magumu bila kuangalia sura ya mtu.

Maamuzi hayo ni kuachana na zaidi ya wachezaji 10 na kuongeza wengine wapya nane kwa ajili ya kuinusuru timu hiyo na aibu ya kushuka daraja msimu ujao.

Timu hiyo ambayo inashiriki Ligi Kuu kwa msimu wa kwanza, ndio wanaburuza mkia kwa pointi tano na presha imeanza kupanda na kushuka kwa mashabiki wao juu ya hatma ya kubaki salama.

Hata hivyo, baada ya mchezo wao dhidi ya Tanzania Prisons waliopoteza kwa bao 1-0, wachezaji walipewa mapumziko ya siku tatu na leo Alhamisi wanarejea kambini kujiwinda na Coastal Union.

Katibu Mkuu wa timu hiyo, Benson Mkocha alisema hawaridhishwi na mwenendo wa matokeo akieleza kuwa wamekubali raundi ya kwanza liwalo na liwe na badala yake mzunguko wa pili kitaeleweka.

Alisema katika kuhakikisha timu hiyo inabaki salama Ligi Kuu msimu ujao, wanaenda kufanya maamuzi magumu bila kuangalia sura ya mtu kwa kutema wachezaji zaidi ya 10 na kuongeza nane wenye uwezo na uzoefu.

“Bora tubaki wachache lakini wenye kufanya kazi kuliko kuwa na idadi kubwa ambayo inatugharimu bila faida, dirisha dogo tutatema wengi sana, (zaidi ya 10) tuongeze wanane”

“Tutakuwa makini kuangalia wenye uwezo na uzoefu wa ligi ambao wakiingia kikosini kazi iwe ni kusahihisha matokeo yaliyotokea mechi za mzunguko wa kwanza” alisema Mkocha.

Mmoja wa wadau wa soka na mchezaji wa zamani jijini hapa, Charles Makwaza alisema timu hiyo inapaswa kufanya maboresho kwakuwa wachezaji wao wengi ni chipukizi.

“Ligi yetu imebadilika, hao vijana wao walipaswa kuwapo baadhi kwa ajili ya kupata uzoefu siyo kuwakabidhi majukumu makubwa kihivyo, waende Simba, Yanga au Azam waombe wachezaji ambao hawapati nafasi kwa mkopo,” alisema Makwaza

Related Posts

en English sw Swahili