Donald Trump amewahutubia wafuasi wake na kuwaeleza kuwa ameshida dhidi ya Kamala Harris katika uchaguzi wa rais wa Marekani, huku kura zikiendelea kuhesabiwa katika baadhi ya majimbo yaliyosalia.
Kiongozi huyo wa Chama cha Republican amewaambia wafuasi wake waliokuwa na furaha kubwa huko Florida kwamba wataanzisha “Enzi mpya ya dhahabu kwa Marekani … Huu ni ushindi mkubwa kwa watu wa Marekani ambao utatuwezesha kufanya Marekani iwe kubwa tena.”
Trump atakuwa rais wa kwanza wa zamani kurejea Ikulu baada ya zaidi ya miaka 130. Katika habari nyingine njema kwa Trump, chama chake kinatarajiwa kushinda udhibiti wa wingi wa viti katika Seneti.
Rais wa Marekani anavyopatikana
Rais wa Marekani hupatikana kwa njia ya uchaguzi mkuu, ambao ni mchakato rasmi wa kidemokrasia unaojumuisha hatua kadhaa zilizoratibiwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo.
Mchakato huu huanza na kura za awali za vyama, ambapo vyama vikuu – yaani, Chama cha Republican na Chama cha Democratic – pamoja na vyama vidogo, hufanya kura za uteuzi wa mgombea ndani ya vyama vyao.
Katika hatua ya kwanza, wanachama wa kila chama katika majimbo yote hupiga kura za awali (primaries) au mikutano ya uchaguzi (caucuses) kuchagua mgombea anayewakilisha chama chao.
Baada ya mchakato huu, vyama huandaa mikutano ya kitaifa (conventions) ambako wajumbe waliochaguliwa hukutana ili kutangaza rasmi mgombea wa urais na mgombea mwenza wake.
Baada ya uteuzi wa wagombea, kampeni kuu huanza ambapo wagombea wanajitahidi kuvutia wapiga kura kwa kutoa sera na mipango yao. Wakati wa kampeni, wagombea hushiriki midahalo ya moja kwa moja na kutumia vyombo vya habari kuhamasisha na kueleza mipango yao kwa wananchi.
Siku ya uchaguzi mkuu – kawaida hufanyika Jumanne ya kwanza ya mwezi Novemba katika miaka ya uchaguzi – wananchi hupiga kura kumchagua mgombea wanayemtaka. Mfumo wa Marekani wa uchaguzi hutegemea kile kinachojulikana kama “Electoral College.”
Hii ni taasisi yenye wajumbe ambao kikatiba wanahitajika kumpigia kura mgombea aliyepata kura nyingi katika jimbo lao. Jumla ya wajumbe ni 538, na mgombea anayeweza kupata kura 270 au zaidi ndiye hutangazwa mshindi.
Mchakato wa “Electoral College” unahusisha majimbo kutuma wajumbe wao mwezi Desemba kwenda kupiga kura rasmi za kumchagua rais.
Hatua ya mwisho ni mnamo Januari mwaka unaofuata, ambapo kura za wajumbe hukabidhiwa rasmi kwa Kongresi ya Marekani kwa ajili ya kuhesabiwa, na hatimaye mshindi huapishwa rasmi kuwa Rais wa Marekani.