Medo kuanza na straika Kagera

KOCHA mpya wa Kagera Sugar, Melis Medo amenogewa na ushindi wa mabao 2-1, alioupata akikiongoza kikosi hicho kwa mara ya kwanza mbele ya Dodoma Jiji na anatarajia kufanya maboresho makubwa dirisha dogo hasa eneo la ushambuliaji alililobaini ndilo lenye tatizo.

Wakati kocha Medo akifunguka hayo, Mwanaspoti linafahamu tayari mkononi mwake ana jina la mshambuliaji Raizin Hafidh ambaye amekuwa akizunguka naye kila timu anapohamia timu mpya, pia eneo la beki ana faili la Amani Kyata ambaye amefanya naye kazi Dodoma Jiji, Coastal Union na Mtibwa Sugar.

Medo  aliyejiunga na Kagera, Oktoba 17 mwaka huu akitokea Mtibwa Sugar ameiongoza timu hiyo katika mechi tatu ameshinda moja, sare moja na kipigo kimoja.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo raia wa Marekani alisema wachezaji wa Kagera wameanza kumuelewa na wanaingia mdogo mdogo katika mfumo lakini shida kubwa ni kukosekana kwa mshambuliaji ambaye anaweza kutumia nafasi.

“Nawapongeza wachezaji wangu walikuwa bora ndio maana tumepata matokeo naamini kadri muda unavyokwenda tutaendelea kuwa bora lakini kuna shinda ambayo naamini nitaitatua dirisha dogo hasa eneo la ushambuliaji,” alisema Medo na kuongeza;

“Ni maeneo mengi ya kuboresha kwenye kikosi changu lakini eneo la ushambuliaji ndiyo changamoto kubwa timu inacheza vizuri lakini inakosa mtu wa kumalizia.”

Medo alisema ametengeneza timu kwenye muunganiko mzuri na wachezaji tayari wameanza kuelewana uwanjani makosa madogo madogo ndiyo yanawaangusha likiwemo suala la umaliziaji.

“Kujenga timu nzuri na ya ushindani unatakiwa kuwa na safu bora ya ushambuliaji na ulinzi lakini ukikosa ubora maeneo hayo yote huwezi kuwa na timu shindani naamini baada ya dirisha dogo tutakuwa na mengi ya kufanya kwa usahihi.”

Related Posts