Mradi kuwezesha wakulima 60,000 kuuza mazao nje

Dar es Salaam. Wakulima wadogo 60,000 wanaozalisha mahindi, mpunga, alizeti na soya wanatarajia kunufaika na mradi utakaowawezesha kuyafikia masoko ya kimataifa.

Mradi huo uliopewa jina la ‘Tukue Pamoja’ unafadhiliwa na Serikali ya Norway unatarajia kutumia Sh27.9 bilioni kwa miaka mitano kuanzia mwaka huu.

Utakelezaji unaanza wakati ambao Tanzania imeendelea kushuhudia ukuaji wa mauzo ya mazao ya chakula katika masoko ya kimataifa yakiwamo mahindi, mchele na maharage.

Akizungumza leo Novemba 6, 2024 wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Bernard Ndolo, meneja mrogramu mwandamizi katika Taasisi ya IDH Transforming Martket, amesema kabla ya kuanza utekekelezaji ulifanyika utafiti kuangalia changamoto za usalama wa chakula nchini Tanzania na mazao ya chakula yanayolimwa sana.

Amesema pia wamezingatia uhitaji wake katika masoko ya nje na ndani, na kiwango cha wakulima wanaojihusisha na kilimo cha mazao hayo.

“Tuligundua ni mahindi, maharage, alizeti na soya. Tanzania ni nchi inayolima mazao ya chakula kwa kiasi kikubwa na wafanyabiashara wengi wadogo, wa kati na wakubwa wanatamani kufanya biashara nje ya Tanzania licha ya kuwapo kwa masoko makubwa lakini walikuwa hawawezi kuyafikia,” amesema.

Ndolo amesema ujio wa programu hiyo utawawezesha kufika wanakohitaji, akieleza kampuni 10 za Tanzania ndizo zitakazotumika kuhakikisha wakulima hao wanafikiwa na kupatiwa msaada wa kiteknolojia na kifedha

“Tunaamini wafanyabiashara wadogo na wale wa kati (SME) ndio wanaweza kuwapa wakulima motisha kulima mazao hayo na baadaye wao ndio wanaweza kuyasambaza katika masoko mengi, jambo ambalo litaongeza usalama wa chakula si tu kwa Tanzania, bali hadi nchi za jirani, zikiwemo za Afrika Mashariki,” amesema.

Amesema wanaamini kwa sasa yapo mashirika mengi yanayofanya kazi katika mazao yaliyochaguliwa na kuhakikisha sehemu ambayo kazi haijafanyika vizuri pengo hilo linazibwa.

“Kama ni mkulima wa mahindi unaweza kuongeza uchakataji au usafirishaji wa mahindi, inaweza kuwa ni soko linalopaswa kutafutwa na hivi ndivyo vitu tunavyotaka kufanya kwa kuangalia nini wanataka kufanya ili mradi waweze kukua,” amesema.

Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Kilimo anayeshughulikia ushirika na umwagiliaji, Dk Suleiman Serera amesema mradi huo utawasaidia wakulima kuzalisha kwa ubora unaotakiwa ili wanapopeleka mazao hayo nje wasikumbane na vikwazo vya ubora.

Hali hiyo itafanya wakulima kupata fedha na kampuni hizo kuendesha shughuli zake kwa ufanisi.

Amesema katika kuhakikisha lengo hilo linafanikiwa, Serikali itaendelea kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji kuhakikisha wakulima wanalima katika vipindi vyote vya mwaka bila kutegemea msimu wa mvua pekee.

“Kitu cha kwanza tunachokitazama katika mradi huu ni kuangalia namna mkulima anavyonufaika, kwa sasa unaweza kukuta mkulima anapata Sh10, Je, wanaokuja watamsababishia mkulima kupata Sh100? Hatutaki azirudishe fedha hizo hadi kufikia Sh9 au Sh8 ,ndiyo maana kila hatua wanayokwenda lazima tuifahamu,” amesema.

Wakati jitihada hizo zikifanyika, taarifa ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2024/2025 inaonyesha mauzo ya mahindi yameongezeka kwa zaidi ya mara 17 katika mwaka 2022/2023 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Mauzo ya mahindi mwaka 2021/2022 yalikuwa zaidi ya Sh35.861 bilioni ambayo yaliongezeka hadi kufikia Sh628.958 bilioni mwaka 2022/2023.

Mauzo ya maharage yaliongezeka kutoka Sh137.453 bilioni hadi kufikia Sh200.03 bilioni mwaka 2022/2023.

Related Posts