SIMBA leo inacheza mechi ya 10 katika Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC huku matarajio ya wengi ni kuona nyota wa kikosi hicho, Kibu Denis maarufu Mkandaji akifungua ukurasa mpya wa kucheka na nyavu.
Kibu ambaye alijiunga na Simba msimu wa 2021/22 akitokea Mbeya City, amecheza mwaka mzima bila kufunga bao katika Ligi Kuu Bara.
Rekodi zinaonyesha mara ya mwisho alifunga Novemba 5, 2023 wakati Simba ikifungwa 5-1 na Yanga. Hadi leo, Novemba 6, 2024 ni siku 366, takribani mwaka mmoja umepita hajafunga. Inashangaza.
KWANINI KIBU?
Kwa leo Kibu anaweza kuwa na madhara makubwa mbele ya KMC kutokana na rekodi nzuri aliyojiwekea dhidi ya timu hiyo katika misimu mitatu iliyopita.
Katika mechi sita zilizopita dhidi ya KMC, Kibu amefanikiwa kufunga mabao matatu na kutoa asisti moja, jambo linalomfanya awe mchezaji hatari zaidi wa Simba kwa wapinzani hao wa Kinondoni.
Hiyo inampa nafasi ya kipekee ya kuisaidia Simba kuvuna ushindi mwingine muhimu dhidi ya KMC kutokana na namna anavyoifahamu safu ya ulinzi ya timu hiyo.
Katika msimu wa 2021/22 mechi ikichezwa Desemba 24, 2021, Kibu aliisaidia Simba kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya KMC, ambapo alifunga mabao mawili.
Ushindi huo ulidhihirisha uwezo wake wa kufunga, huku pia mabeki wa Simba, Joash Onyango na Mohammed Hussein wakifunga mabao mengine mawili.
Mchango wa Kibu kwenye mchezo huo ulikuwa muhimu sana, ikizingatiwa kuwa ni wakati ambao alionyesha ufanisi wa hali ya juu kwa kutumia nafasi alizozipata kwa ustadi mkubwa.
Mchezo mwingine wa kipekee kwa Kibu dhidi ya KMC ulikuwa Juni 19, 2022, ambapo alifunga bao moja na kutoa asisti kwa Pape Ousmane Sakho.
Bao na asisti katika mchezo huo viliihakikishia Simba kuondoka na ushindi wa mabao 3-1, hivyo kuendeleza rekodi ya kuisaidia timu yake kupata ushindi dhidi ya wapinzani hao.
Mchezo huo ulionyesha sio tu uwezo wa Kibu wa kufunga, bali pia ujuzi wake wa kutoa msaada wa mabao kwa wachezaji wenzake, jambo linaloongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ya Simba.
Katika misimu miwili iliyopita, Simba imefanikiwa kuvuna alama nane kati ya 12 kwenye mechi nne dhidi ya KMC, hata kama Kibu hakufunga katika michezo minne ndani ya kipindi hicho. Hii inaashiria kuwa mchango wake haupo tu kwenye ufungaji, bali pia kwenye jinsi anavyochangia kwa jumla katika mipango ya kushambulia ya timu.
Kwa kuwa mchezaji wa Simba aliye na rekodi bora zaidi dhidi ya KMC kwa sasa, kuna matarajio makubwa kuwa atatumia vyema uzoefu wake kuwapa Simba faida katika mchezo huu.
KMC inapaswa kuwa makini katika kumzuia Kibu ambaye ana kiu kubwa ya kufunga baada ya kukaa mwaka mzima bila ya kutikisa nyavu za wapinzani ndani ya ligi.
Ikiwa Kocha Fadlu Davids atampa nafasi Kibu kucheza leo na akawa bora kama kawaida yake, kuna uwezekano akawa na madhara makubwa na chachu ya ushindi kwa Simba.
MCHEZAJI MUHIMU
Wakati wa maandalizi ya msimu huu, Kibu hakuwa na timu kambini nchini Misri, lakini alipoungana na wenzake jijini Dar, akaanza taratibu kujitengenezea ufalme wake na sasa amejihakikishia namba.
Simba ikiwa imecheza mechi tisa za ligi msimu huu, Kibu amefanikiwa kucheza nane huku mara sita akianza kikosi cha kwanza. Mechi mbili pekee za kwanza dhidi ya Tabora United na Fountain Gate ndiyo alianzia benchi na kuingia baadaye, hiyo ilitokana na kwamba hakuwa fiti baada ya kuchelewa kujiunga na wenzake. Lakini pia hakucheza dhidi ya Namungo. Jumla ametumika kwa dakika 542 katika mechi nane zenye dakika 720.
Licha ya kwamba msimu huu hajafunga, lakini alihusika kupatikana kwa bao pekee dhidi ya Tanzania Prisons Simba iliposhinda 1-0 kwani alifanyiwa madhambi nje kidogo ya boksi, akapiga faulo mwenyewe iliyomkuta mfungaji Che Malone Fondoh.
Uchezaji wake katika kusaidia mashambulizi na kurudi nyuma kukaba, ndiyo silaha inayombeba zaidi Kibu ambaye amekuwa kipenzi cha makocha saba waliomfundisha ndani ya Simba ambao ni Didier Gomes, Pablo Franco, Zoran Maki, Juma Mgunda, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, Abdelhak Benchikha na sasa Fadlu Davids.
Majukumu yake ndani ya uwanja si kufunga pekee, bali ana jukumu la kusaidia mashambulizi na ulinzi.
TATIZO NINI?
Kukaa mwaka mmoja bila ya kufunga bao katika ligi kunaonekana inachangiwa na namna majukumu anayopewa na kocha wake kwani huu ukiwa ni msimu wake wa nne, amefunga jumla ya mabao 11 pekee.
Takwimu zinaonyesha kwamba, Kibu katika msimu wake wa kwanza ndani ya Simba 2021/22 alimaliza na mabao manane akiwa kinara ndani ya kikosi hicho akimzidi Meddie Kagere aliyefunga saba.
Msimu wa pili 2022/23, alimaliza na mabao mawili, kisha 2023/24 akafunga moja dhidi ya Yanga.
Nyota wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel alisema kinachosababisha hayo yote kutokea kwa Kibu anakaa mbali na goli hivyo inakuwa ngumu kufunga.
“Anatumia vizuri nguvu, pumzi ndio maana unamkuta yupo mbali na goli, anakaba na kusaka mipira, pamoja na hayo yote jukumu lake uwanjani ni kufunga, hivyo ajirekebishe aanze kukaa eneo linalotakiwa ili afunge.
“Mfano uchezaji wa Mohamed Salah anatokea pembeni ila ana uwezo wa kucheza 1V1 anapata balansi ya umiliki mpira na anafunga, hivyo Kibu afanye sana mazoezi ya kufunga ili awe anaingia ndani ya boksi itamsaidia.”
Nyota mwingine wa zamani wa Simba, Steven Mapunda alisema: “Kibu ana bodi nzuri, nguvu na pumzi, kitu anachotakiwa akifanyie kazi awe anaingia ndani ya boksi la wapinzani, akifanya hivyo atafunga sana mabao na hilo anapaswa kulifanyia sana mazoezi ya timu na binafsi, akizingatia hayo atakuwa hatari zaidi.”
Nafasi ya Simba kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara leo ipo mikononi mwao wakati timu hiyo itakapokabiliana na KMC kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam.
Hadi kufikia leo, zimepita takribani siku 56 tangu Simba kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kuanza ligi vizuri kwa kushinda 3-0 dhidi ya Tabora United kisha 4-0 mbele ya Fountain Gate.
Baada ya hapo, Simba ililazimika kucheza mechi mbili za Kombe la Shirikisho Afrika ambapo iliiondosha Al Ahli Tripoli ya Libya na kufuzu makundi. Kitendo cha kucheza mechi za kimataifa huku ligi ikiendelea ndiyo iliwatoa kileleni. Rekodi zinaonyesha mara ya mwisho Simba kukaa kileleni ni Septemba 11 mwaka huu, leo ina nafasi ya kurejea endapo ikipata ushindi utakaoifanya kufikisha pointi 25, moja zaidi ya Yanga. Ni mchezo mgumu kwa pande zote mbili kutokana na kila mmoja kuhitaji ushindi ili kujiweka kwenye mazingira mazuri kunako msimamo wa ligi hiyo.
KMC ambao ni wageni wa mchezo huo kikanuni, lakini kiuhalisia ni wenyeji kwa sababu uwanja unaotumika ni wao, watakuwa na kazi kubwa mbele ya Simba. Kazi kubwa ya KMC katika mchezo wa leo ni kuhakikisha wanapata ushindi wa kwanza mbele ya Simba tangu timu hizo zianze kukutana katika michezo ya Ligi Kuu Bara. Rekodi zinaonyesha KMC iliyoanza kushiriki Ligi Kuu msimu wa 2018/19, haijawahi kushinda mbele ya Simba katika mechi 12 mfululizo.
Katika mechi hizo, imeshuhudiwa mara mbili pekee KMC ikiambulia sare tena zote ni matokeo ya 2-2, ilikuwa Septemba 7, 2022 na Desemba 23, 2023.
Kabla ya hapo, Simba iliifunga KMC mechi nane mfululizo za ligi kabla ya kuwasimamisha ya tisa ambayo waliambulia pointi ya kwanza kutokana na kupata sare. Kisha wakafungwa, halafu wakajiuliza tena na kuambulia sare, huku mechi ya mwisho wakifungwa tena 1-0.
Ni mara moja pekee ambayo mchezo baina ya Simba na KMC ulimalizika kwa kadi nyekundu aliyoipata beki wa KMC, Andrew Vicent wakati timu hizo zilipokutana Julai 7, 2021 na Simba kushinda 2-0.
KMC ikiwa imefunga mabao nane na kuruhusu 12 katika mechi kumi, inaonekana benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha mkuu, Abdihamid Moallin, lina kazi ya kufanya kuboresha maeneo hayo.
Simba katika mechi tisa, wamefunga mabao 17 na kuruhusu matatu hivyo Kocha Fadlu Davids na wasaidizi wake kwa kiasi fulani wameifanya kazi nzuri kuzipa makali safu hizo.
Akizungumzia mchezo huo, Fadlu alisema wapinzani wao wana kikosi bora, hivyo wamejiandaa kukabiliana na timu itakayowapa ushindani mkubwa, huku Kocha wa KMC, Abdihamid Moallin akisema: “Simba wana timu nzuri, tutajaribu kupunguza makosa ili kuwanyima nafasi ya kufunga