Minnesota. Huldah Momanyi Hiltsley, mzaliwa wa Kenya, ameweka historia kwa kushinda kiti katika Baraza la Wawakilishi la Minnesota kwa zaidi ya asilimia 64 ya kura.
Hiltsley alishindana na Wynfred Russell, kiongozi wa jumuiya ya wazaliwa wa Liberia na mjumbe wa zamani wa Baraza la Jiji la Brooklyn Park.
Katika hotuba yake ya baada ya kuchaguliwa, Hiltsley amesema: “Ninasimama hapa kama mtu wa kwanza mzaliwa wa Kenya kuwahi kuchaguliwa nchini Marekani. Ushindi huu ni wetu sote; ni ushahidi wa ujasiri na nguvu za wahamiaji.”
Ushindi wake unaashiria hatua kubwa na kumfanya kuwa miongoni mwa wahamiaji wachache waliozaliwa Afrika kufikia ngazi hii ya wadhifa wa kisiasa nchini Marekani.
Akitokea Kaunti ya Nyamira, Kenya, Hiltsley alihamia Minnesota akiwa na umri wa miaka tisa na tangu wakati huo amejijengea sifa kubwa katika utumishi wa umma na utetezi wa jamii.
Kampeni yake ilitanguliza mbele masuala muhimu kama vile usalama wa umma, makazi sawa na upatikanaji wa huduma ya afya ambayo inawahusu wapigakura mbalimbali wanaojumuisha idadi kubwa ya wahamiaji.
Mtazamo wake wa chini na uhamasishaji wa kimkakati wa wapigakura ulikuwa muhimu kwa mafanikio yake.
Akigombea kupitia chama cha Democratic-Farmer-Labor, Hiltsley atawakilisha jumuiya za kusini magharibi mwa Brooklyn Park na Osseo.
Ushindi wake unaonekana kuwa hatua muhimu mbele kwa uwakilishi wa wahamiaji katika siasa za Marekani hasa huko Minnesota ambapo jamii nyingi za wahamiaji huhisi kutowakilishwa vizuri serikalini.