HAIKUWA kazi nyepesi kwa viongozi wa Yanga wakiongozwa na Hersi Said kunasa saini ya kiungo Pacôme Zouzoua, nyota mahiri wa Ivory Coast ambaye kwa sasa anawafanya Wananchi watembee vifua mbele.
Uwezo wa kumiliki mpira, kasi na kupenya ngome za wapinzani umemfanya asitoke vinywani mwa mashabiki wa timu hiyo.
Licha ya kuwa na wachezaji hatari kama Clatous Chama, Max Nzengeli na Azizi Ki, Zouzoua anaonekana kuwa ladha tofauti ambayo imezidi kuimarisha safu ya kiungo ya Yanga.
Nyota huyo wa zamani wa Asec Mimosas ni fundi haswa anayeifanya Yanga kuwa timu tishio kwenye viwanja vya ndani na nje ya nchi, lakini kama ulidhani kwamba kwa Wananchi ndo amefika, basi sahau kwani anataka kupatumia kama daraja la mafanikio ili akakipige katika ligi kubwa na bora zaidi duniani, na katika mahojiano haya anazungumza mambo mbalimbali ikiwamo kuacha alama katika Ligi Kuu Bara.
Zouzoua anasema: “Nataka kuisaidia Yanga kushinda mataji, lakini pia nataka kuonyesha kiwango bora ili nifikie ndoto zangu za kucheza katika ligi kubwa zaidi. Naamini kupitia Yanga nitapata fursa ya kuonekana zaidi na kufikia malengo yangu ya kuwa mmoja wa wachezaji bora barani Afrika.”
Zouzoua anasema anatamani kuona Yanga inavuka mipaka ya Tanzania na kuonyesha uwezo katika ngazi ya kimataifa, hususan kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Zouzoua ni mfano wa wachezaji wanaoweka mbele nidhamu, bidii na malengo makubwa. Akiwa bado kijana mwenye kiu ya mafanikio anajua kuwa safari yake ya soka bado ina mengi ya kufanikisha.
“Nataka kuacha alama katika soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla. Ninaamini kuwa kwa msaada wa wachezaji wenzangu na benchi la ufundi, Yanga itafanikiwa kutwaa mataji na mimi pia nitatimiza malengo yangu binafsi.”
Kwa sasa, Zouzoua anaendelea kujituma mazoezini, akijipanga kwa michezo mikubwa inayokuja. Kwa moyo wa ushindani na kujituma, hakuna shaka kuwa fundi huyo anaweza kuwa sehemu ya mafanikio ya Yanga
Akimzungumzia mchezaji mwenzake Stephane Aziz KI, nyota huyo anaonyesha heshima kubwa akisema: “Azizi ni mchezaji wa aina yake. Ana kipaji kikubwa, uelewa wa mchezo na anajituma sana. Uwezo wake wa kucheza nafasi tofauti za ushambuliaji ni silaha kubwa kwa timu yetu.”
Kwa Zouzoua, uwepo wa wachezaji kama Azizi KI kikosini unasaidia timu kuwa na mchanganyiko mzuri wa vipaji, huku kila mchezaji akichangia mafanikio.
Kuhusu safari ya Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu mchezaji huyo anasema imeghubikwa na matumaini makubwa.
“Tuna kikosi chenye ubora wa kushindana. Malengo ni kufika mbali zaidi ya hatua tuliyofikia msimu uliopita. Tunataka kupambana na kutengeneza historia mpya kwa Yanga,” anasema.
Anasema ingawa kuna changamoto nyingi timu imejipanga vilivyo kuhakikisha inawapa furaha mashabiki wake.
“Mwaka huu tuna ari na kikosi bora. Tumejifunza kutoka katika makosa yetu ya nyuma na sasa tuko tayari kupambana na yeyote.”
Zouzoua anasisitiza kuwa licha ya ushindani mkali unaokuja kutoka kwa timu kubwa kama TP Mazembe, Al Hilal na MC Alger, lakini Yanga imejizatiti kuonyesha ubora Afrika.
“Hatua ya makundi itakuwa ngumu, lakini tuna uwezo wa kuvuka na kufika hatua za juu zaidi.”
Mchezaji huyo aliukosa mchezo wa mwisho wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Mamelodi Sundowns msimu uliopita kutokana na majeraha na hilo lilikuwa pigo kubwa kwake, lakini sasa anajiona akiwa na ari mpya.
“Nijisikia vibaya kukosa mechi hiyo. Mamelodi ni moja ya timu bora Afrika na iliniumiza kuona timu yangu inapambana bila mimi. Lakini sasa nipo tayari na nasubiri kwa hamu kuonyesha uwezo wangu dhidi ya timu kubwa kama hiyo,” anasema nyota huyo.
Anasema mechi hiyo ilimfundisha umuhimu wa kuwa tayari wakati wowote kwani majeraha yanaweza kuja bila kutarajia na kwa sasa anafanya kila jitihada kuhakikisha anabaki fiti kuisaidia Yanga katika safari ya kimataifa.
Mchezaji huyo amekuwa akipitia mabadiliko makubwa tangu alipojiunga na Yanga, akiwa amezoea maisha zaidi maisha ya Ivory Coast anaona Tanzania kuwa ni taifa lenye utulivu na shauku kubwa ya mafanikio kisoka.
“Maisha Tanzania ni ya amani sana. Watu hapa wanapenda mpira wa miguu. Hii imenifanya nijisikie kama niko nyumbani, ingawa bado kuna mambo ya kujifunza kuhusu tamaduni zao,” anasema.
Anaongeza kuwa licha ya mazingira kuwa tofauti na kwao, amepata urahisi wa kuzoea kutokana na uungwana wa mashabiki na wanachama wa Klabu ya Yanga.
Akizungumza kuhusu tofauti ya soka kati ya Tanzania na Ivory Coast, anaeleza kuwa Tanzania kuna ufanisi zaidi, lakini inapaswa kupambana kwenye viwango vya kimataifa.
“Tanzania ina wachezaji wenye vipaji vikubwa, lakini kasi ya mchezo ni tofauti na Ivory Coast. Kule soka ni la kasi zaidi na kuna nidhamu kubwa ya kimbinu. Hapa inahitaji mchezaji awe na vitu vyote hivyo pamoja na utimamu.”
Nyota huyo anaonyesha imani kuwa Tanzania inaweza kufikia viwango vya juu zaidi iwapo kutakuwa na uwekezaji mkubwa zaidi kwenye soka la vijana na miundombinu.