Siku moja nilidamka kwenda kwenye harakati zangu za kawaida. Lakini kabla sijatoa mguu wangu nje, mvua ikanya. Nikatoka lakini baada ya kujiandaa na mwavuli na viatu vya mvua. Nilipofika mjini hali ilikuwa tofauti kabisa na ile niliyoachana nayo nyumbani; jua lilikuwa kali na hakukuwa na dalili yoyote ya mvua. Hii ndiyo Dar es Salaam ambako kilomita mbili tu mbele majira yanakubadilikia.
Watu wa mikoa ya Pwani si wageni wa mabadiliko mafupi mafupi ya hali ya hewa. Kipande kimoja kina fukuto, lakini cha pili kilicho umbali mfupi kutoka hapo kina ubaridi. Wakati mwingine watu wanaweza kukudhania uchawi ukikatiza na mwavuli na koti la mvua mahala pakavu na penye joto la kuivisha kiazi kitamu. Ni mambo ya ajabu ingawaje wenyeji tunayaona kuwa ya kawaida.
Kule mkoani Mbeya kulikuwa na mto kwenye maeneo ya Kaporogwe, sijafuatilia kama maeneo hayo bado yangalipo au yamekwishatoweka. Mto Kaporogwe ulitengeneza bwawa kubwa ambalo wenyeji walifika hapo kufua na kupata mahitaji mengine ya maji. Cha ajabu kwenye bwawa hilo ni chemchemi ya maji ya moto wa sentigredi mia moja. Amini usiamini, kiazi kiliiva kwa dakika tano baada ya kuwekwa hapo.
Haya ni machache katika maajabu ya nchi ya Tanzania. Hii ndiyo nchi yenye upendo wa mshumaa, kwani ndiyo iliyowapigania wageni wapate haki na amani ya mioyo, wakati wenyeji wakiilalamikia kuwa tofauti na nchi yao inavyotajwa. Ni nchi inayosifika duniani kwa kuzingatia utawala wa haki na sheria, wakati wenyewe wanalalamikiana kwa rushwa ya pesa na ngono kama kipaumbele cha kupata ajira.
Madai ya wenyeji wa bongo yanafikirisha. Pamoja na sifa zote za urembo na utajiri wa nchi yao, Watanzania wamekuwa wakiogelea kwenye dimbwi la umasikini uliokithiri. Kadhalika nchi yetu inazo sifa nyingi za amani na utulivu uliodumu kwa muda unaokaribia karne nzima tokea tupate uhuru kutoka kwa wakoloni bila kumwaga damu, lakini wakati huohuo kuna malalamishi mengi ya ukiukwaji wa sheria na kanuni za maisha.
Kama ilivyo kwenye mabadiliko ya hali ya hewa, watu hulalamika pale changamoto zinapoonekana kuzidi badala ya kupungua. Kila msimu wa mvua husema “haijawahi kutokea mvua kama hii”. Na wakati wa kiangazi wanaona jua likiwa kali kuliko nyakati zilizopita.
Hivi sasa huku mtaani wazee wa mtaa wanasikika wakitoa mshangao kwa jinsi kila uchaguzi unapokuja na sura tofauti na ile iliyotangulia: “Haujawahi kutokea uchaguzi kama huu”.
Wapigakura watakiri kushangazwa mapokezi ya vijimambo vipya ndani ya kila uchaguzi mpya kila mwaka. Rushwa, wizi wa kura na mipangilio mibovu inalalamikiwa kila kukicha. Mengine yanaonekana kama yanayofanywa kwa makusudi.
Ni lazima changamoto ziwepo kwenye kila jambo. Lakini changamoto zisizotafutiwa ufumbuzi na zinazoachiwa ziendelee wakati zinaweza kuzuilika zimekuwa kidonda cha mazoea. Haiwezekani tusijifunze kutokana na makosa yaliyopita na kuyatatua, haya ndio ninayoyaita kidonda cha mazoea kama kuanzisha michubuko kwenye kovu la zamani.
Mwaka huu pamoja na Tume ya Uchaguzi kuja na jina jipya la Tume Huru ya Uchaguzi, bado hali inaonekana kuwa mbaya zaidi kuliko pale kabla haijaitwa huru. Vitendo kama uandikishaji wa majina hewa, kufunga ofisi wakati wa kazi na kadhalika kumeifanya kambi ya upinzani kudhani ni jitihada za makusudi za kuvuruga uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Yaani kama wanamlazimisha bubu kusema.
Kwa maoni yangu, mambo haya hayakuwa na sababu hata kidogo. Yanapofanyika au kutofanyika hayawezi kuleta tofauti kubwa kwenye matokeo, ila tu kusababisha migomo, maandamano na malalamiko yasiyo na sababu yoyote kwa Serikali. Haya ndiyo yanayosababisha Msumbiji pasikalike, na nchi izidi kudidimia kiuchumi wakati ilishajipata kiasi cha Watanzania kwenda kujitafutia huko.
Kuendelea na makamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwenye Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi hakuoneshi mabadiliko ya kuboresha Tume ya Uchaguzi. Wanaonekana kuendeleza yaleyale yaliyoonekana kutofaa kama vile hawana mawazo mapya ya uboreshaji.
Ndio kwanza kumeonekana kuzaliwa kwa matatizo mapya, kama wapiga kura kujiandikisha bila kufuata utaratibu wa utambulisho sahihi.
Mpaka hapa tulipo kumeshaonekana kukosekana kwa sheria maalumu za kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hali inayoibua wasiwasi kuhusu uhalali na uwazi wa uchaguzi huo.
Hata kutumia watumishi wa umma kwenye shughuli za uchaguzi kunashusha imani juu ya uadilifu wa uchaguzi.
Kwenye maeneo mengine wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi walitajwa kuwapatia fomu ya kugombea watu wasiotambulishwa na vyama kuwa mgombea wao.
Hili nalo ni neno kubwa, kwani inadhaniwa kuwa chama tawala kinatengeneza njia yake ndani ya wapinzani.
Wapinzani hawa wamedai kuwatafuta wahusika ambao walionesha wazi kutokuwa tayari kutoa ushirikiano au kuwakatia simu.
Kwenye hali hii Serikali inabeba mzigo wa lawama na bila shaka ni lazima ijisafishe kabla mambo hayajaharibika. Kuharibika kwa mambo kunaweza kuifanya nchi yetu kuwa zaidi ya Msumbiji, iliyokwisha kujichimbia kaburi lake yenyewe.