PPRA YAENDESHA MAFUNZO MODULI MPYA MFUMO WA NeST MWANZA

MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) inaendesha Mafunzo kuhusu Sheria mpya ya Ununuzi pamoja na Moduli mpya za Mfumo wa NeST kwa watumishi wa umma kutoka kada na Taasisi mbalimbali nchini,

Mafunzo hayo yaliyoanza rasmi Novemba 4, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa jengo la Rock City Mall Jijini Mwanza, yamehudhuriwa na washiriki zaidi ya 180 wa kada mbalimbali wakiwemo Maafisa Ununuzi, Maafisa Sheria, Wakuu wa Vitendo vya Ununuzi, na wengineo.

Meneja wa PPRA kanda ya Ziwa Mhandisi Juma Mkobya amesema, muendelezo wa utoaji mafunzo hayo ni utekelezaji wa jitihada za Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma, ya kuhakikisha wanawajengea uwezo wadau wa Ununuzi wakiwemo Maafisa wa Serikali pamoja na wazabuni ili kuhakikisha weledi na uzoefu wa matumizi ya mfumo unaongezeka ili kurahisisha utendaji kazi katika michakato ya Ununuzi wa Umma Nchini.

“Tunategemea mpaka kufikia mwisho wa mafunzo haya mtakuwa mmenufaika pakubwa katika kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu Sheria hii ya Ununuzi pamoja na hizi Moduli Mpya za Mfumo” Amesema Mhandisi Mkobya

Diana Kingo ni mshiriki wa mafunzo hayo, naye ameipongeza PPRA kwa kuzidi kuleta maboresho ya mfumo yanayotokana na changamoto zinazogundulika na kufanyiwa kazi siku hadi siku, ili kuleta ufanisi katika sekta nyeti ya Ununuzi wa Umma,

“Sisi kama watendaji katika kada hii ya Ununuzi tunazidi kuridhishwa na maboresho ya mfumo pamoja na sheria ya Ununuzi, tunaamini kupitia haya tutaweza kuivusha nchi yetu pakubwa kupitia sekta hii ya Ununuzi”

Mafunzo haya yanatarajiwa kutamatika ifikapo tarehe 8 Novemba, 2024 huku Mamlaka ikiwa inaendelea kuendesha mafunzo hayo siku hadi siku kulingana na ratiba inayopangwa.

Related Posts