Saadun kazi ndo kwanza imeanza

MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Nassor Saadun amesema msimu huu, utakuwa wa kuandika rekodi na kupiga hatua katika karia yake ya soka.

Mshambuliaji huyo ambaye hadi sasa ametupia mabao matatu Ligi Kuu akifunga dhidi ya KMC (KMC 0-4 Azam), Prisons (Prisons 0-2) na Coastal Union (Azam -1-0 Coastal), alisema anafahamu ana kazi ngumu na atahitaji kupambana zaidi, ili kuziishi ndoto zake.

“Natamani uwe msimu utakaobakia katika kumbukumbu za maisha yangu ya soka, ndiyo maana naendelea kupambana siku hadi siku kuona kiwango changu kinazidi kukua, ili niisaidie timu na kujisaidia mwenyewe kukua kiuchezaji.

Aliongeza; “Natambua ligi ni ngumu, inanisaidia  nisijisahau pindi ninapopata nafasi ya kucheza kuona nimeishamaliza kazi, badala yake naendelea kujifunza na kujiongeza katika mazoezi binafsi.”

Mbali na hilo, mashabiki wa Stars kwa sasa wanamtazama Saadun kama tunu kwa Taifa, alilizungumzia hilo, “Kuna kaka zetu waliotutangulia na wamefanya vitu vingi vikubwa, kama vijana tunapaswa kujifunza mengi kutoka kwao, ili kuendeleza walipoishia wao na siyo kuharibu.

Aliongeza; “Najisikia faraja kupewa nafasi katika kikosi cha Stars,  jambo la msingi nitazidi kupambana na kuzidisha nidhamu ili huduma yangu iwe na manufaa kwa Taifa na klabu iliyoniajiri.”

Alisema bado ana safari ndefu ya kufanya mengi,  hasa anavutiwa na hatua za mafanikio alizonazo Mbwana Samatta anayekipiga PAOK ya Ugiriki.

“Samatta ni kioo kwetu, kwani amefanya kila kitu kinawezekana katika karia yetu, tukizingatia nidhamu na kujituma, natamani siku nicheze naye timu ya taifa,” alisema.

Related Posts