Dar es Salaam. Mamlaka za usimamizi wa sheria za usalama barabarani zinalalamikiwa kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo, hivyo kuwa chanzo cha vurugu za madereva wa bajaji na bodaboda.
Lawama zinaelekezwa kwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra) na Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani zinazosimamia Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 (Sura ya 168 ya Sheria za Tanzania, Toleo la 2002).
Kwa mujibu wa Latra, idadi ya vyombo hivyo vilivyopewa leseni nchini kwa mwaka wa fedha 2023/24, bodaboda zipo 46,146 na bajaji zipo 22,408. Mbali ya hao, inaelezwa walio wengi hawana leseni.
Licha ya usimamizi hafifu wa sheria, changamoto hiyo inaelezwa pia inachangiwa na kutokuwapo sheria mahususi ya kuwadhibiti madereva wa bajaji na pikipiki.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhani Ng’azi akizungumza na Mwananchi jana Jumatatu Novemba 4, 2024 anasema sheria ya usalama barabarani ina changamoto, kwani wakati inaanzishwa hawakuweka pikipiki na bajaji kama chombo cha kusafirisha abiria.
“Mkakati mkubwa tunaokuja nao tunakusudia kubadilisha sheria zetu, ili usafiri wa abiria kupitia pikipiki usimamiwe kuanzia kuwatambua nani amenunua na kuwapa vituo maalumu,” anasema.
Anasema lengo la kufanya hivyo ni kutengeneza urahisi wa kuwasimamia na kuwafuatilia, huku lengo likiwa usimamizi uwe katika mfumo wa mtandao ili kuwa rahisi kushughulika na wanaovunja sheria.
Ng’azi anasema wanachofanya sasa Polisi kwa kushirikiana na Latra na mamlaka nyingine za halmashauri, wanakaa ili kuja na mpango wa kudhibiti kundi hilo.
Mkuu wa Idara ya Usafirishaji na Biashara wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, Dk Prosper Nyaki anapendekeza kuundwa sheria kudhibiti bodaboda, kuongeza adhabu, kuboresha miundombinu ya barabara, akiwataka wanasiasa kuacha kuingilia masuala ya kisheria.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Kikatoliki Mbeya (CUCoM), Balozi Mnorwa anasema kukua kwa sekta hiyo ni kiashiria kuwa hakuna ajira na ni sababu wengi wanakimbilia kujiari kwenye bodaboda na walio wengi hawajasomea udereva.
“Ulaya mtu anayeendesha pikipiki anatakiwa kuwa dereva zaidi ya anayeendesha gari, huku mtu anauza shamba lake alilopewa ananunua bodaboda anaingia barabarani,” anasema.
Anasema sekta hiyo itakuwa na tija iwapo itakuwa imerasimishwa, tofauti na ilivyo sasa kwa sababu hata mchango wao kwenye kodi bado haueleweki kwa kuwa hawalipi.
“Bodaboda wengi hawana bima, na ni eneo muhimu la kuongeza wigo wa kodi na mapato, kama itarasimishwa kwa kuwa na mfumo mzuri utaiingizia fedha Serikali.
“Wengi wanaendesha bodaboda wakiwa wamelewa na kuishia kupata ajali, ni eneo ambalo Serikali imeruhusu watu wajiajiri lakini hawajatengeneza mfumo uliokuwa rasmi, ingawa imesaidia kupunguza uzururaji wa vijana mtaani,” anasema.
Mbali ya hayo, wadau wa usalama barabarani waliozungumza na Mwananchi wanaeleza ugumu wa udhibiti kuwa unachangiwa na wanasiasa wanaotumia vyombo hivyo vya moto ambavyo ni chanzo cha ajira kwa vijana katika shughuli za kisiasa, baadhi wakipatiwa sare, kuwekewa mafuta na kupewa fedha, hivyo kuwapa kiburi cha kutofuata sheria wawapo barabarani.
Rajabu Kafwapili, askari mstaafu wa Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani anadai wanasiasa ni kikwazo katika utendaji na usimamizi wa sheria.
“Askari mmoja ana uwezo wa kukamata hata bodaboda 20 kwa siku, lakini wanasiasa watakuja kuzitoa. Mwanasiasa anatunga sheria, lakini akitoka nje anazikana, anasema askari wanawaonea bodaboda,” anasema.
Anasema askari anatekeleza sheria zinazotungwa na Bunge, akitoa mfano wa adhabu kwa wakosaji awali ilikuwa Sh30,000 lakini bodaboda waliwalilia wanasiasa ishushwe bila kujali kuwa ni chambo cha moto.
“Mpanda baiskeli analipa Sh20,000 akifanya kosa inakuwaje huyu wa chombo cha moto apunguziwe? Waendesha baiskeli hawajapunguziwa bodaboda ni kundi kubwa linalopiga kura,” anasema.
Rajabu aliyefanya kazi Mbeya, Dar es Salaam na Arusha anasema kipindi cha uchaguzi wanasiasa hukodi bodaboda, kuwawekea mafuta na kwenda kuwapigia kura, hivyo kutumia hilo kama fursa ya kuvunja sheria.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge anasema nchi inaongozwa kwa mujibu wa sheria na hakuna aliye juu ya sheria.
“Kusema tunawakingia kifua hayo ni maneno tu, wazingatie sheria. Ni kweli wananchi wanahitaji huduma, lakini lazima wazingatie taratibu kama leseni zao zinavyotaka, wanaokiuka vyombo vya kusimamia vipo hakuna mkuu wa mkoa anayesema pita katika taa nyekundu,” anasema.
Kunenge anasema hakuna kiongozi anayewataka bodaboda wabebe mishikaki, hivyo jambo la msingi wazingatie utawala wa sheria.
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana anasema hakuna kiongozi anayewalinda bodaboda wanavunja sheria ya usalama barabarani.
“Hao wanajitetea kwa sababu chombo chochote cha moto lazima kiwe na leseni na kinatakiwa kuzingatia sheria na taratibu zote zilizowekwa, huwezi kusema viongozi wa kisiasa wa mikoa wanawakingia kifua kitu kama hicho hakipo,” anasema.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Bananga anasema ni kweli bodaboda wanatumiwa na wanasiasa wa vyama vyote.
“Kusema wanasiasa wanawapa kiburi cha kuvunja sheria sikubaliani nalo, kwa sababu wakati mwingine wanavunja sheria hata wanasiasa hawapo na wengine hata kwenye shughuli za kisiasa hawaendi, hiyo ni tabia ya mtu,” anasema na kuongeza.
“Utetezi wetu kwao wapewe nafasi ya kufanya shughuli zao, kwa mfano wakati ule walikuwa hawaruhusiwi kupita mjini, wanasiasa tulipiga kelele wakaingia mjini. Wakati wanatozwa adhabu kubwa tulipiga kelele zilishushwa hadi Sh10,000 kutoka Sh30,000 lakini hatuungi mkono uvunjaji wa sheria,” anasema.
Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini anasema kuwaachia wanasiasa kuingilia mambo yanayohitaji taaluma, nchi inarudi nyuma.
“Tuseme ukweli kama ni wanasiasa wanaivuruga nchi, na wale waliopewa mamlaka ya kuangalia ustawi wa nchi wanatakiwa kuangalia hilo. Hivi sasa miji imevurugika, ajali nyingi za magari zinasababishwa na bodaboda.
“Miji na majiji yatunge sheria ya usimamizi wa bodaboda na ikiwezekana kuwe na njia zake. Mimi ni muathirika wa ajali niliyosababishwiwa na bodaboda,” anasema.
Spika wa Bunge la Wananchi la Chadema, Suzan Lyimo anasema chama hicho kimekuwa kikikemea kikitaka mamlaka kutunga sheria kali.
“Kwamba wanatumika na wanasiasa kuendesha misafara wanalipwa kama ambavyo wanabeba abiria mwingine kwa sababu ni vyombo vya usafiri,” anasema.
Anasema mikutano ya hadhara haifanyiki mara kwa mara, akieleza ajali kila siku hutokea.
“Chadema tumekemea hadharani, kiongozi wetu Godbless Lema amejitokeza mara kadhaa kuzungumzia jambo hili, walimbeza ingawa alitoa sababu wanakufa kwa makosa ya uzembe,” anasema.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya anasema wakati sheria inapitishwa kuhusu bodaboda kuwa chombo cha usafiri alikuwa sehemu ya Bunge hilo.
“Nilisema tusipoweka sheria kuvidhibiti vitaleta maafa kwa sababu yeyote anaweza kutumia. Mwaka 2019 niliikumbusha Serikali takwimu ya maafa na vifo, bodaboda inaongoza.
“Sikatai kuna wakati wanasiasa wanapenda kutetea wananchi wao, inawezekana kuna udhaifu huo siwezi kukataa kwa sababu sijui kinachoendelea nchi nzima,” anasema.
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu anasema wanapowatumia bodaboda katika shughuli zao bado wanawataka kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.
“Sisi ni sehemu ya jamii tumejitungia sheria zetu lazima zifuatwe kuwatumia bodaboda si uchochoro wa kujitetea wasifuate sheria, lazima wafuate sheria wasipate madhara na jamii kwa ujumla,” anasema.
Anasema mamlaka zinapaswa kuwa makini kusimamia sheria, akisema haoni kama kuna utaratibu uliowekwa kuhakikisha bodaboda wanapata mafunzo ya kuwanoa mara kwa mara.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Solomon Mwangamilo anasema: “tunawajengea uwezo kupitia madawati yetu ya elimu na vijiwe vyao. Semina na makongamano tunawakusanya na kuwaelimisha, tunaamini kumuadhibu mtoto kabla ya kujua kosa lake tunakuwa hatumfundishi.”
Anasema wengi hawajui sheria kwa kuwa wanafanya shughuli hizo hawana leseni na kama wangepata wangejifunza sheria na miiko.
“Tunawashauri wanapoendesha kutumia kofia ngumu ili iwasaidie wanapopata ajali wasiumie sehemu ya kichwa na wasipakie watu zaidi ya mmoja, kwani athari zake ni kubwa,” anasema na kuongeza:
“Tunawakamata wanaokiuka sheria, lakini suala la adhabu siwezi kuzungumzia kwa kuwa ni maamuzi ya Bunge, jukumu letu ni kusimamia sheria zilizopo ingawa hata Sh30,000 binafsi naweza kukuambia ni ndogo lakini kwa kuwa imewekwa tunawaandikia vivyo hivyo.”
Kwa mujibu wa takwimu za Hali ya Uhalifu na Matukio ya Usalama Barabarani 2023, kati ya Januari hadi Desemba, 2023 jumla ya matukio 435 ya ajali za pikipiki yaliripotiwa, ikilinganishwa na matukio ya ajali 448 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.