Simba vs KMC, vita iko hapa

Dar es Salaam. Nafasi ya Simba kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara leo ipo mikononi mwao wakati timu hiyo itakapokabiliana na KMC kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam.

Hadi kufikia leo, zimepita takribani siku 56 tangu mara ya mwisho Simba kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kuanza ligi vizuri kwa kushinda 3-0 dhidi ya Tabora United kisha 4-0 mbele ya Fountain Gate.

Baada ya hapo, Simba ililazimika kucheza mechi mbili za Kombe la Shirikisho Afrika ambapo iliiondosha Al Ahli Tripoli ya Libya na kufuzu makundi. Kitendo cha kucheza mechi za kimataifa huku ligi ikiendelea ndiyo iliwatoa kileleni.

Rekodi zinaonyesha mara ya mwisho Simba kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi ni Septemba 11 mwaka huu, leo timu hiyo ina nafasi ya kurejea hapo juu endapo ikipata ushindi utakaowafanya kufikisha pointi 25, moja zaidi ya Yanga.

Ni mchezo mgumu kwa pande zote mbili kutokana na kila mmoja kuhitaji ushindi ili kujiweka kwenye mazingira mazuri kunako msimamo wa ligi hiyo.

KMC ambao ni wageni wa mchezo huo kikanuni, lakini kiuhalisia ni wenyeji kwa sababu uwanja unaotumika ni wao, watakuwa na kazi kubwa mbele ya Simba.

Kazi kubwa ya KMC katika mchezo wa leo ni kuhakikisha wanapata ushindi wa kwanza mbele ya Simba tangu timu hizo zianze kukutana katika michezo ya Ligi Kuu Bara.

Rekodi zinaonyesha kwamba, KMC iliyoanza kushiriki Ligi Kuu Bara msimu wa 2018/19, haijawahi kushinda mbele ya Simba katika mechi 12 mfululizo.

Katika mechi hizo, imeshuhudiwa mara mbili pekee KMC ikiambulia sare tena zote ni matokeo ya 2-2, ilikuwa Septemba 7, 2022 na Desemba 23, 2023.

Kabla ya hapo, Simba iliifunga KMC mechi nane mfululizo za ligi kabla ya kuwasimamisha mechi ya tisa ambayo waliambulia pointi ya kwanza kutokana na kupata sare. Kisha wakafungwa, halafu wakajiuliza tena na kuambulia sare, huku mechi ya mwisho wakifungwa tena 1-0.

Ni mara moja pekee ambayo mchezo baina ya Simba na KMC ulimalizika kwa kadi nyekundu aliyoipata beki wa KMC, Andrew Vicent wakati timu hizo zilipokutana Julai 7, 2021 na Simba kushinda 2-0.

KMC ikiwa imefunga mabao nane na kuruhusu 12 katika mechi kumi, inaonekana benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha mkuu, Abdihamid Moallin, lina kazi ya kufanya kuboresha maeneo hayo.

Wapinzani wao Simba, katika mechi tisa, wamefunga mabao 17 na kuruhusu matatu hivyo Kocha Fadlu Davids na wasaidizi wake kwa kiasi fulani wameifanya kazi nzuri kuzipa makali safu hizo.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids amesema wapinzani wao wana kikosi bora, hivyo wamejiandaa kukabiliana na timu itakayowapa ushindani mkubwa.

“KMC wana kikosi bora pamoja na kocha wao, tunatarajia kuwa na mchezo mgumu lakini tumejiandaa vizuri kuwakabili na kuondoka na alama zote tatu.

“Kila mechi inakuwa tofauti, tunawaheshimu wapinzani ambao siku si nyingi wametoka kucheza dhidi ya Yanga na kuonyesha mchezo mzuri, nafahamu watakuja na mbinu zao nzuri kuhakikisha wanapata ushindi.

“Kagoma (Yusuph) na Mashaka (Valentino) hawatakuwepo, Hamza (Abdulrazack) ameanza mazoezi lakini hayupo tayari kwa kucheza lakini wachezaji wengine wapo vizuri,” alisema Fadlu.

Naye Kocha wa KMC, Abdihamid Moallin amesema: “Simba wana timu nzuri, tutajaribu kupunguza makosa ili kuwanyima nafasi ya kufunga, kikubwa tunataka kila mtu afurahie mchezo kesho (leo) huku malengo yetu yakiwa ni kupata ushindi.”

Wakati Simba ikisaka ushindi ili kukaa kileleni, KMC yenyewe inahitaji kujiimarisha kwenye msimamo kwani hivi sasa inashika nafasi ya sita ikiwa na pointi 14, ikishinda inafikisha pointi 17 ambazo inazifikia zile za Fountain Gate ilizokuwa nazo kabla ya jana kucheza dhidi ya Pamba Jiji.

Related Posts