TBS, Unido kukarabati mfumo wa maabara

Morogoro. Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Viwanda (Unido), limeanzisha ukarabati wa mfumo wa uendeshaji maabara (LIMS) ili kuongeza ufanisi na kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia.

Maboresho haya yanakuja baada ya kutambua umuhimu wa matumizi ya mifumo ya kielektroniki, ambayo inarahisisha utoaji wa huduma mbalimbali ndani ya TBS ikiwamo kupunguza matumizi ya makaratasi katika kuhifadhi kumbukumbu.

Haya yamesemwa leo Jumatano Novemba 6, 2024 mjini Morogoro na Mshauri mwelekezi wa mfumo, Madock Chiwenda.

Amesema bado kuna makaratasi mengi yanatumika, hivyo wanataka kuuboresha mfumo uliopo wa kielektroniki ili kuwa na uwazi zaidi katika vipimo vinavyofanyika ikilenga kukidhi matakwa ya viwango kupitia vipimo vinavyofanyika maabara.

Naye Meneja wa upimaji kutoka TBS, Joseph Makene amesema shirika hilo limefadhiliwa  kupitia mradi wa Qualitan kwa lengo la kuimarisha mifumo yake.

“Lengo hasa ni kuongeza ufanisi zaidi katika maabara sambamba na kupunguza kasoro zinazojitokeza, kutokana na matumizi ya makaratasi ya kuhifadhi kumbukumbu za kitaalam,” amesema Makene.

Amesema kikubwa kinachowasukuma ni kutaka kuboresha mifumo yao hasa ya kimaabara ili kuhakikisha wanakidhi matakwa ya viwango vya kimataifa katika upimaji wa bidhaa nchini.

MJakene amesema uboreshaji wa mfumo huo utaenda kumsaidia mlaji moja kwa moja, kwa kuwa mfumo huo sasa utasaidia kuokoa muda na kumsaidia mlaji kupata majibu ya vipimo vya kimaabara kwa haraka zaidi.

Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria, Candida Shirima amesema shirika limeendelea kuboresha na kuimarisha umahiri wake katika kufanya ukaguzi nchini ili kulinda afya, kuwezesha biashara na kulinda usalama.

Amesema katika kuboresha mifumo, kuimarisha mifumo pamoja na kuzingatia jukumu la ukaguzi, TBS limeona umuhimu wa kuwapa mafunzo wakaguzi wake mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na namna mifumo hiyo inavyofanya kazi, hivyo kuongeza ufanisi zaidi katika zoezi la upimaji bidhaa.

“Ukaguzi ni jukumu la msingi linalofanywa na TBS, Ili kufanikisha kupata bidhaa zenye ubora na usalama, ni lazima idara za ukaguzi na mifumo inayotumika kwenye kaguzi hizo ziwe na uwezo wa kufanya kaguzi kwa wakati na kutoa matokeo ambayo yanatambulika kitaifa, na kuwezesha wazalishaji kuzalisha bidhaa zitakazokuwa na soko ndani na nje ya nchi,” alisema Candida.

Aidha, Meneja wa mradi wa Qualitan, Alejandro Rivera Rojas kutoka Unido amesema Tanzania ni moja ya nchi saba duniani zinazotekeleza mradi huo baada ya kukidhi vigezo.

Rivera ameongeza kuwa lengo kuu la mradi huo, uliogharimu Euro milioni 7 (Sh18.4 bilioni) ni kuhakikisha mfumo wa maabara wa LIMS unasaidia kutoa huduma bora, kupunguza makosa yatokanayo na binadamu na kufikia wahitaji wengi, zikiwamo kampuni na mtu mmoja mmoja.

Amesema kabla ya kuleta mradi huu, shirika lilifanya tathmini ya hali ya ukuaji wa kidijitali katika vipengele mbalimbali vya miundombinu ya ubora, ikiwa ni pamoja na viwango, sayansi ya vipimo, uthibitishaji, tathmini ya ufanisi na ufuatiliaji wa soko.

Related Posts