UCHUMI WA BULUU UNA FAIDA KUBWA

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohamed Sheikh akifunga kikao kazi cha kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa Uchumi wa Buluu kwa mwaka wa fedha 2024/25 na 2025/26 kilichofanyika Arusha kwa siku mbili.

Sehemu ya washiriki wakifuatilia kikao kazi cha kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa Uchumi wa Buluu kwa mwaka wa fedha 2024/25 na 2025/26 kilichofanyika Arusha kwa siku mbili.

….

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohamed Sheikh amesema Uchumi wa Buluu unafaida kubwa katika kuinua uchumi wa taifa hivyo kila mmoja anapopata fursa ya kutoa ujuzi wake anatakiwa kufanya hivyo kwa faida ya nchi.

Ameyasema hayo Novemba 5, 2024 wakati akifunga kikao kazi cha kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa Uchumi wa Buluu kwa mwaka wa fedha 2024/25 na 2025/26 kilichofanyika Arusha kwa siku mbili.

Amesema nafasi waliyopewa wataalamu kukutana na kuandaa mpango kazi ni mwanga mzuri na ni mwanzo wa kuhakikisha taifa linakwenda kutumia utaalamu wao katika kushauri viongozi ili kuinua uchumi wa nchi.

“Tunapozungumzia Uchumi wa Buluu tunaangalia kitu kikubwa ambacho kina faida kwa nchi kwa vizazi vya sasa na vijavyo hivyo kila mmoja ahakikishe anasimama vyema katika nafasi yake na kushauri vizuri.

“Kama tutaweka mkazo kwenye Idara ya Uvuvi tutaona matokeo yake haraka hasa pale tunapoanza kutekeleza haya ambayo tumeanza kuyajadili hapa wataalamu kwa kuwa Uchumi wa Buluu ndani yake kuna vitu vingi ambavyo ni faida kwetu,” amesema Prof. Sheikh.

Ameongeza katika kuhakiksha hilo serikali inaweka uwanda mpana katika uvuvi na tayari imejengwa Bandari Kilwa na Februari mwaka ujao itazinduliwa wakati ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ikiendelea na mchakato.

Prof. Sheikh amesema unapoangaliwa Uchumi wa Buluu isiangaliwe uvuvi wa Samaki pekee bali ndani yake kuna vitu vingi ambavyo vinapatikana kama vile madini na kilimo.

Pamoja na uwekezaji wa Serikali katika miundombinu na huduma mbalimbali, bado kuna umuhimu wa kujenga uelewa wa fursa zilizopo na kuweka vivutio stahiki ili kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi.

Related Posts