Kiongozi huyo mwenye mtazamo wa kizalendo anatarajiwa kuongoza nchi hiyo tena kwa kipindi cha miaka minne, ambapo atakuwa karibu na washirika wake wa kisiasa na kupambana na maadui wa ndani na nje. Ingawa Trump anaweza kuwa na mipango mahsusi ya kukuza maslahi ya Marekani, historia yake inaonyesha kwamba masuala ya Afrika mara nyingi hayajapewa kipaumbele.
Ushindi wa Trump dhidi ya Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris umepokelewa kwa mitazamo tofauti barani Afrika, huku wengine wakiwa na matumaini kwa kuuzungumzia uongozi wake madhubuti, na wengine wakiwa na mashaka kuhusu namna ushindi huo utakavyokuwa ulimwenguni.
Wachambuzi wanasema hakuna uwezekano kwamba Trump ataongeza Mkataba wa Ukuaji na Fursa za Kibiashara Afrika, AGOA mwaka ujao, mkataba muhimu wa kibiashara na kipaumbele kwa bara hilo, ingawa wabunge wa chama chake cha Republican wanaunga mkono uidhinishaji mpya.
Wasiwasi wa Afrika na mikataba ya kibiashara
Mkataba huo ambao unaziruhusu nchi za Afrika kusafirisha bidhaa zao Marekani bila kutozwa ushuru, unamalizika mwishoni mwa mwaka ujao wa 2025.
Prasan Nundlal raia wa Afrika Kusini ana wasiwasi na Trump linapokuja suala la mikataba ya kibiashara. “Nina wasiwasi kuhusu mambo kama mikataba yetu ya kibiashara na Marekani kukataliwa, au kufungwa kwa sababu ya Trump,” alisema Nundlal.
Wafuatiliaji wa mambo barani Afrika, wanakisia kuwa utawala wa Trump utachukua mtazamo wa kimaadili na wa vitendo, wakisema ana uwezekano mkubwa wa kuzingatia masuala ya kiuchumi yanayohusiana na bara hilo.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanabainisha kuwa hali ya kutofuatiana ya mtazamo wa Marekani, inategemea kulingana na upande gani unoashinda urais.
Hata katika eneo ambalo limeshuhudia kuongezeka kwa utawala wa kimabavu na kukwamisha demokrasia, baadhi ya wakaazi wake waliliambia shirika la habari la Reuters kwamba wanaamini utawala wa Trump utakuwa mzuri.
“Trump hana tatizo na Afrika. Ni mtu mzuri sana linapokuja suala la kushirikiana na marais wengine au mataifa mengine, ni mzuri sana katika hilo, na tunahitaji kiongozi wa aina hiyo,” anabainisha David Ilembo raia wa Afrika Kusini.
Demokrasia na haki zaondoa nchi 7 AGOA
Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, utawala wa Joe Biden uliziondolea nchi 7 za Afrika stahiki zao katika mkataba wa AGOA kwa kutozingatia demokrasia. Nchi ya Uganda iliondolewa kwenye mkataba huo, kutokana na kuidhinisha sheria inayopinga watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.
“Waafrika wanampenda Trump, kwa sababu haungi mkono haki za LGBTQ, na wengineo. Na pia ni mtu mwenye misimamo na kanuni. Anazungumza kilichoko moyoni mwake,” alifafanua Oni Abiodun, raia wa Nigeria.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa Trump anapaswa kubuni tena sera mpya kuelekea Afrika. Iwapo hatofanya hivyo, Marekani ina hatari ya kulipoteza bara la Afrika kwa nchi za Mashariki.
(AFP, Reuters)