Dodoma/Dar. Wakati mgombea urais wa Republican nchini Marekani, Donald Trump amerejea Ikulu, ushindi wake wake umeelezwa kuwa na athari mpya kwa Afrika, hasa katika masuala ya biashara, uhamiaji na msaada wa kimataifa.
Sera zake za “America First” zinaibua wasiwasi kuhusu mustakabali wa Mpango wa Ukuaji na Fursa za Kiuchumi kwa Afrika (AGOA), misaada ya PEPFAR na uhusiano wa kiuchumi baina ya Marekani na Afrika.
Wataalamu wa masuala ya siasa na uchumi wanashauri nchi za Afrika kujiandaa kwa kipindi kigumu cha kujitegemea na kuchagua ajenda zinazoendana na mabadiliko haya ya kisera, huku wakitaja mambo kadhaa, yakiwamo ya wahamiaji na kusisitiza utoaji mimba, kuwa ndiyo yamemwangusha mpinzani wake wa Democrats, Kamala Harris.
Wamarekani wameonekana kuvutiwa zaidi na sera ya Trump ya tangu uchaguzi wa mwaka 2016 ya MAGA -Make America Great Again (ikimaanisha kurejesha ukuu wa Marekani duniani), suala ambalo ni kilio kwa Bara la Afrika.
Trump aliwahi kuziita nchi za Afrika, Haiti na El Salvador kuwa ‘shithole countries’ akilalamika kuwa kuna wahamiaji wengi wanatoka kwenye nchi hizo kuingia nchini mwake.
Ushindi wake unatajwa kuwa na athari kwa AGOA iliyozinduliwa mwaka 2000 na Rais wa wakati huo, Bill Clinton, ikilenga kutoa fursa kwa nchi za Afrika zinazokidhi vigezo kuuza bidhaa katika soko la Marekani bila kutozwa ushuru.
Fursa hiyo inafikia tamati Septemba mwakani na tayari Umoja wa Afrika umeliomba Bunge la Marekani kuongeza muda walau miaka 10 kuendeleza mpango huo, ombi ambalo huenda likagonga mwamba.
Hofu nyingine kwa nchi za Afrika ni kuvurugika kwa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR).
Mfuko huu ulianzishwa mwaka 2003, chini ya utawala wa Rais George W. Bush, ambao Serikali ya Marekani imewekeza zaidi ya Dola 100 bilioni katika kupambana na VVU/UKIMWI duniani.
Trump alipoingia madarakani mwaka 2016 aliwaita Waafrika ni wavivu na wapumbavu, akieleza wanachojua ni kula, kufanya mapenzi na uhalifu.
Mbali na sera ya MAGA inayokosolewa kwa kupalilia ubaguzi wa rangi ndani yake hasa kwa Waafrika, Trump ana sera ya kuzuia utoaji mimba akipania kuacha kutoa misaada kwa taasisi zote zinazochochea utoaji mimba na anapinga vitendo vya ndoa za jinsia moja.
Mambo yaliyosababisha Kamala Harris kushindwa uchaguzi ni pamoja na yeye kujiweka ni ‘kizazi kipya cha uongozi’, mwenye maono ambaye atafanya kazi ikiwamo kutafuta suluhu badala ya vita vya kisiasa, kushughulikia masuala ya kupanda kwa gharama za maisha na uwezo wa kumudu gharama za makazi.
Wamarekani waliona maneno yake si kama mwenye kutaka kufanya mabadiliko, badala yake aliendelea kuwa mwaminifu kwa Rais Joe Biden aliyempisha ili agombee.
Wamarekani waliona Biden ni mtu ambaye hakuweza kushughulikia mfumuko wa bei na uhamiaji haramu.
Kamala kwenye kampeni zake za mwishoni alionekana kumshambulia Trump kuwa hana msimamo.
Trump ameshinda kura za uamuzi ‘electoral college’ 279 dhidi ya Kamala aliyepata kura 224. Mshindi anatakiwa apate kura 270.
Vilevile Trump ameshinda kura za umma 72,221,423 sawa na asilimia 51.05, huku Kamala akipata kura 67,141,073 sawa na asilimia 47.5 (hadi tunakwenda mitamboni).
Katika Bunge la Seneti chama cha Trump cha Republican kimepata viti 52 dhidi ya viti 42 vya chama cha Kamala cha Democrats.
Kwenye Baraza la Wawakilishi hadi tunakwenda mitamboni Republican ilikuwa imeshinda kwa viti 198 dhidi ya viti 180 vya Democrats.
Uchaguzi wa magavana Trump ameendelea kushinda kwa kupata magavana 27 dhidi ya 23 wa chama cha Kamala cha Democrats.
Kwenye uchaguzi wa mwaka 2016 Hillary Clinton alipata kura nyingi za umma zaidi ya milioni 2.9 dhidi ya Trump, lakini alishindwa kwenye kura za uamuzi ‘electoral college’ ambazo Trump alipata 306 huku Clinton akipata 227.
Kwenye uchaguzi wa 2020 Trump alishindwa na Joe Biden ambaye kwenye kura za umma alishinda kwa kura 81,284,666 na Trump alipata kura 74,224,319. Biden bado alishinda kura za uamuzi kwa kupata kura 306 huku Trump akipata 232.
Mpambano kati ya Trump na Kamala ulikuwa kwenye majimbo saba ambayo vyama vyote hivyo havina ngome ya Arizona, Georgia, Michigan, Nevada, North Carolina, Pennsylvania na Wisconsin. Kwenye majimbo hayo mwaka 2016 alipata kura za umma 66,282,873 sawa na asilimia 47.5.
Rais mwenye kesi za jinai
Trump ameweka historia kwa kuwa Rais wa kwanza wa zamani na Rais mteule wa Marekani kutiwa hatiani kwa mashtaka ya jinai, baada ya jopo la mahakama maalumu mjini New York kumtia hatiani kwa mashtaka yote 34 dhidi yake.
Mashitaka hayo yanahusiana na kughushi rekodi za biashara ili kuficha malipo aliyotoa kwa nyota wa zamani wa filamu za ngono, Stormy Daniels, kama njia ya kumzuia kutoa taarifa kuhusu uhusiano wao kabla ya uchaguzi wa urais wa 2016.
Malipo hayo, yaliyo chini ya kile kinachojulikana kama ‘hush money’ yanadaiwa kufanywa kwa siri kulinda taswira yake na kuhakikisha suala hilo halingetibua kampeni zake.
Hata hivyo, mashtaka hayo hayakumzuia kugombea urais kwa sababu Katiba inasema mgombea urais lazima wawe na umri wa angalau miaka 35, awe raia wa asili wa Marekani, na awe ameishi nchini humo kwa angalau miaka 14.
Hakuna sheria inayozuia mtu mwenye rekodi ya uhalifu kugombea urais na ndiyo maana Trump amegombea na hatimaye kushinda.
Mchambuzi wa masuala ya kimataifa, Ibrahim Rabby amesema ushindi wa Trump una tafsiri nyingi kwa Afrika, swali kubwa likiwa kama atakuwa yuleyule wa awamu yake ya kwanza ya 2016 hadi 2020 au atakuwa mpya.
“Afrika inatakiwa kufahamu kuwa sera za Trump haziwezi kubadilika kwa sababu tangu kwenye mchakato wa kampeni zake hakuonyesha kubadilisha chochote na hasa linapokuja suala la nje, anaangalia zaidi Marekani na slogan (kaulimbiu) yake America Great Again (ikimaanisha kurejesha ukuu wa Marekani)” amesema.
Rabby amesema kama Marekani haiwezi kupata chochote kutoka Afrika, basi haiwezi kuifuatilia nchi yoyote, bali atakachofanya ni kulifungua taifa kwa kuzingatia uhusiano na faida zaidi.
“Mfano, Mashariki ya Kati ataendelea na nchi zinazoipa faida Marekani ikiwemo Saudi Arabia, Falme za Kiarabu na atakata uhusiano na nchi zinazotaka kulitegemea taifa hilo.
“Trump anakwepa kile ambacho Marekani imekuwa ikikifanya miaka mingi kwa Afrika. Kuna cha kujifunza miaka ya 2016 hadi 2020 tulishuhudia nchi za Afrika zikifanya mapinduzi mengi kwa sababu Marekani aliyeonekana kiranja wa dunia alikwepa majukumu yake na kuacha kuitazama Afrika,” amesema.
Amesema Rais Joe Biden hajaitembelea Afrika zaidi ya Kamala Harris. Kwa ushindi wa Trump anasema ni lazima Afrika iamue kujitegemea kwa sababu maisha hayo ni muhimu zaidi.
“Sera za Trump kwa nje ziko wazi na wala huhitaji kwenda darasani kujifunza kujua anawaza nini, mabadiliko yatatokea hasa kwenye taasisi. Kipindi chake kilichopita taasisi nyingi zilifungwa kwa kukosa ufadhili,” amesema.
Mawazo ya Rabby hayako mbali na ya Innocent Shoo, mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Salim Ahmed Salim anayesema kuwa nchi za Afrika zinatakiwa kufunga mkanda kwa sababu Trump atadhibiti uhamiaji haramu na utoaji misaada.
“Viongozi wa Afrika wanatakiwa kuja na ajenda ya kudhibiti vijana wanaozamia kwenda Ulaya na Marekani kusaka maisha mazuri. Trump amechoka, amesema akiingia anakwenda kufukuza wahamiaji wote haramu,” amesema.
Shoo amesema mtazamo wa Trump ni kuiponya Marekani na anataka kurudisha uwezo wa taifa hilo. Ameeleza Afrika inapaswa kujipanga kwa kuwa ameshapiga kengele.
“Tunatarajia vita vya Gaza na Israel, na upande wa mashariki ya kati labda vitaisha, ikiwemo pia Sudan. Atajaribu kumaliza vita hivyo kwa kuongea na viongozi wa nchi hizo hivyo itasaidia bei ya mafuta kupungua,” amesema.
Wenye mawazo hayo si hao wawili tu, hata Dk Balozi Morwa, mhadhiri katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Kikatoliki Mbeya (CUCoM) amesema Trump amechaguliwa kwa lengo la kumaliza vita vinavyoendelea katika maeneo mbalimbali duniani.
“Raia wengi wa Marekani wamekuwa wakilalamika fedha zao za kodi zinatumika kuendesha vita Ukraine na Russia. Kumalizwa vita hivyo, Afrika itanufaika na rasilimali za mafuta kupungua bei,” amesema.
Dk Morwa amesema vita hivyo vimepandisha bei ya mafuta kwa kuwa wanatumia nishati hiyo kwa kiwango kikubwa, hivyo kwisha kwake neema kubwa itajitokeza na mataifa ya Ulaya wataanza kuitazama Afrika.