Dar es Salaam. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limesema vyombo vya habari nchini humo vinapaswa kufanya kazi na kuacha kulialia kwasababu ya uchumi.
Pia, limesema vyombo vya habari havitabadilisha hali zao za kiuchumi kwa kulialia hadharani. Amesema vyombo vinapaswa kuangalia namna ya kubadili hali vinavyopitia na si kulia kila siku.
Msingi wa kuyasema hayo unatokana na malalamiko yanayowasilishwa mara kwa mara kuhusu hali ya kiuchumi ya vyombo hivyo kuwa mbaya.
Hayo yamesema leo Jumatano, Novemba 6, 2024 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile wakati akitoa taarifa ya Mkutano Mkuu wa mwaka wa jukwaa hilo utakaofunguliwa kesho Alhamisi huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa.
“Tuache kulialia hadharani kuwa tuna hali mbaya. Tufanye kazi kubadili hali hiyo kuwa nzuri. Kwasababu vipo vyombo vinavyolipa wafanyakazi wake kwa wakati,” amesema.
Amesema katika mkutano huo wa kesho Alhamisi watabadilishana na kuunganisha ujuzi kati ya vyombo hivyo vinavyofanya vizuri kwenye malipo kwa wakati pamoja na Bima.
“Kwa sasa tumeazimia kuacha kulialia tunatakiwa kujitokeze kuonesha mikakati ya kufanya biashara ili vyombo vifanye biashara na kutoa huduma ya habari kwa umma,” amesema.
Aidha, Balile ameongeza kwamba kaulimbiu ya mkutano huo ni ‘Weledi wa kitaaluma kwa uhimilivu wa vyombo vya habari.’ Amesema watakwenda kuijadili kama mada.
“Weledi ukipotea kwenye taaluma basi tutajikuta tunafanya mambo yasiyostahili, tunajikuta kwenye hali ngumu ya kiuchumi na mazingira magumu iwapo hatuna weledi wa kitaaluma,” amesema.
Ametoa rai kwa waandishi wa habari kufanya kazi kwa weledi ili walaji waone nguvu inayotumika kufanya kazi. Amesema waandishi wanapaswa kufanya kazi kwa kuendana na teknolojia ya sasa.
Amesema waandishi lazima wajue na wafuate misingi ya uandishi wa habari katika kazi zao za kila siku kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza endapo akienda kinyume.
“Pia, hata suala la uchaguzi wa Serikali za mitaa unaokuja haki na ukweli utawale kwenye kufanya habari zinazohusu uchaguzi huo ikiwemo kutovaa sare za vyama vya kisiasa,” amesema Balile.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na Mwanachama wa TEF, Salim Said Salim amesema changamoto iliyopo kwa waandishi wa habari wa Tanzania wanaandika ya wenzao na wanajikuta wanaacha ya kwao.
“Tunaomba mtoe na habari zenu ili msaada utolewe kwa mashirika ya umma. Pia maadili ni muhimu kwa waandishi, kuwa na lugha ya upole, kusoma maandiko mbalimbali pamoja na tabia njema kwani ni muhimu kuanzia mavazi,” amesisitiza.
Pia, katika mkutano huo amesema watazungumzia utendaji wa vyombo vya habari kwa kujifanyia tathmini ya utendaji kazi wake kwa ujumla.