Wamarekani mmefanikisha ushindi – DW – 06.11.2024

Donald Trump yupo kwenye hatihati ya kutwaa ushindi wa urais leo hii Jumatano baada ya kushinda jimbo la Pennsylvania, matokeo ambayo yanamweka katika nafasi ya kusubiri alama tatu tu ili aweze kutangazwa rasmi kuwa amemshinda mgombea wa chama cha Democrats Kamala Harris.

Hadi sasa Trump ana kura 267 kati ya 270 za wajumbe wa majimbo zinazohitajika kushinda ili aweze kurudi tena kwenye ikulu ya Marekani.

Uchaguzi wa Marekani 2024 | Mgombea Donald Trump
Mgombea urais wa Marekani Donald Trump mke wake Melania Trump na mtoto wao Barron TrumpPicha: Carlos Barria/REUTERS

Ushindi kwenye jimbo la Alaska au katika majimbo yoyote muhimu kwenye uchaguzi huo yanayotoa kura za wajumbe maalum, Electrol College, kama Michigan, Wisconsin, Arizona au Nevada utamfanya rais huyo wa zamani awe mshindi wa kinyang’anyiro hicho kigumu.  

Soma Pia: Harris ama Trump! Wamarekani wamchagua rais wao

Katika hotuba yake mara baada ya kuashiriwa kushinda katika uchaguzi huo Mgombea wa Urais nchini Marekani Donald Trump ameapa kwamba atatetea maslahi ya familia za wamarekani pamoja mustakabali wao. Na amewashukuru wamarekani kwa kumuamini.

Trump amesema: “Ninataka kuwashukuru watu wa Marekani kwa heshima kubwa ya kunichagua kuwa rais wenu wa 47. Nitatetea na kupigania maslahi yenu na familia zenu pamoja na mustakabali wa Maisha yenu. Huu ni ushindi mkubwa sana kwa watu wa Marekani ambao utaturuhusu kuifanya Marekani yetu kuwa taifa kubwa tena.”

Trump kwenye hotuba yake pia amewataka wamarekani kushikama pamoja.

Vyombo vya habari vilitangaza ushindi wa Donald Trump, kwenye jimbo la Pennsylvania ambalo lina kura 19 za wajumbe maalum maarufu kama, electoral college votes. Rais wa Sasa, Joe Biden alishinda katika jimbo la Pennsylvania miaka minne iliyopita, kwa ushindi finyu lakini mgombea wa chama cha Democrats Kamala Harris hakufanya vizuri, amepoteza kura katika karibu kaunti zote za jimbo la Pennsylvania.

Uchaguzi Marekani 2024 | Donald Trump na Kamala Harris
Wagombea urais wa Marekani. Kushoto: Donald Trump. Kulia: Kamala HarrisPicha: AP Photo/picture alliance

Huku matokeo kamaili yakiwa yanasubiriwa kutangazwa shirika la Habari linaloelemea mrengo wa wa kihafidhina Fox News tayari limetangaza kuwa mgombewa wa chama cha Republican Donald Trump ndiye mshindi wa kinyang’anyiro hicho cha urais wa Marekani dhidi ya Kamala Harris, lakini vyombo vingine vya Habari bado havijatangaza ingawa Trump aljiitangaza mwenyewe kuwa ni mshindi katika hotuba yake huko Florida.

Soma Pia: Ufuatiliaji wa Afrika katika uchaguzi wa Marekani

Huku asilimia 96 ya kura zikidhaniwa kuwa tayari zimeshahesabiwa Trump ana asilimia 50.9 na Kamala Harris ana asilimia 47.5 kulingana na taasisi ya Edison inayoongoza kimataifa katika utafiti bora na unaoaminika.

Chanzo: AP

 

Related Posts