Mtama. Polisi mkoani Lindi, linamtafuta dereva wa basi la Kampuni ya King Yasin alietambuliwa kwa jina la Mzee Simba kwa kosa la kusababisha ajali katika eneo la Ruhokwe Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi.
Akizungumza akiwa eneo la tukio leo Jumatano Novemba 6, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, John Imori amesema ajali hiyo imetokea saa 5:00 asubuhi katika Kata ya Monela, Kijiji cha Ruhokwe.
Amesema basi hilo la King Yasin lilikuwa linatokea mkoani Mtwara likielekea jijini Dar es Salaam, limegongana na lori lililokuwa linatokea Masasi kuelekea Mtwara na kusababisha majeruhi watatu ambao wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Nyangaoni iliyopo Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi.
Kamanda huyo amesema baada ya kulipita lori jingine ndipo akakutana na lori hilo ambalo lililokuwa linatokea Masasi kuelekea Mtwara na kugongana nalo uso kwa uso.
“Basi hilo lilibeba abiria 53 na kwenye lori kulikuwa na watu wawili, baada ya kutokea ajali watu wawili wa kwenye basi ambao ni utingo na wakala wameumia na kwenye lori ameumia abiria aliyekuwa anasindikiza mzigo wake, hao wote wamepelekwa Hospitali ya Nyangao,” amesema Kamanda Imory.
Amewataja majeruhi kuwa ni Mohamed Damla (28) mkazi wa Lindi ambaye amevunjika mguu wa kulia, Mohamedi Utali (48) mkazi wa Mtwara ameumia kichwani na Athumani Mote (48) utingo wa lori ameumia mkono na mguu wa kulia.
Akizungumzia ajali hiyo, shuhuda wa ajali hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Rukiya Shabani mkazi wa Mnolela, amesema dereva wa basi alikuwa analipita gari jingine ndipo akajikuta akigongana na lori hilo uso kwa uso.
“Shida madereva wanapokuwa njiani hawana tahadhari kabisa, huyu dereva wa basi hakuwa makini na ndiye amesababisha hii ajali, tumemshudia watu wote tuliokuwa hapa,” amesema Shabani.
Wakati huohuo Kamanda Imori amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi la King Yasin ambaye alikuwa anajaribu kulipita lori jingine bila kuchukua tahadhari.