Ajali ya ‘kipanya’ yaua 14 Tabora, tisa wajeruhiwa

Tabora. Jinamizi la ajali limeendelea kutikisa nchini baada ya watu 14 kufariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa katika ajali iliyotokea Barabara ya Itobo – Bukene, Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora.

Ajali hiyo imetokea leo Alhamisi, saa 2:20 asubuhi Novemba 7, 2024 katika Kijiji cha Mwasengo Kata ya Itobo baada ya gari dogo ya abiria aina ya Toyota Hiace kuligonga kwa nyuma lori na kuingia chini ya uvungu wa lori hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao akizungumza na waandishi wa habari amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva ambaye hakuchukua tahadhari za usalama barabarani.

Kamanda Abwao amesema dereva wa gari hilo dogo aliligonga kwa nyuma gari aina ya Mitsubishi Fuso na kusababisha vifo vya watu 14 wakiwamo wanaume wanane, wanawake wanne, watoto wawili na majeruhi tisa.

Amesema dereva huyo alikimbia na wanaendelea kumsaka, “chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa Hiace aliyekuwa akijaribu kulipita lori hilo lililokuwa mbele yake na kushindwa kulimudu gari lake na kuligonga kwa nyuma upande wa kulia na kuingia chini ya uvungu wa lori jambo lililosababisha vifo na majeruhi.”

Amesema miili imehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Nzega, huku tisa ikitambuliwa na ndugu.

Kamanda Abwao amesema majeruhi wawili wanapatiwa matibabu hospitalini hapo na majeruhi saba wamepewa rufaa kwenda kutibiwa Hospitali ya Rufaa ya Nkinga iliyopo Jimbo la Bukene wilayani Nzega.

Kamanda huyo amesema kuelekea kipindi cha mwisho wa mwaka wataendelea kufanya doria na ukaguzi wa kina kwa lengo la kupunguza ajali zinazoweza kuepukika katika mkoa huo hasa kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka.

“Tutakuwa wakali kwa gari ndogo zinazoelekea vijini watakapojaza abiria kupita kiasi wala hatutakuwa na huruma,” amesema Abwao.

Ajali hiyo imetokea takribani wiki mbili zimepita tangu wanakwaya watano wa Kwaya Kuu (Umoja) wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Wazo Hill, jijini Dar es Salaam wafariki dunia ajalini na wenzao 20 kujeruhiwa.

Ajali ya wanakwaya ilitokea usiku wa kuamkia Oktoba 22, 2024, eneo la Kirinjiko, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, baada ya gari dogo aina ya coaster kuacha njia na kupinduka wakati wakienda kumzika mwenzao wa kwaya ya Tarumbeta ya kanisani hapo, Hapiness Nkya, Mkoa wa Kilimanjaro.

Ajali hizo zimetokea takribani miezi miwili imepita tangu ajali nyingine iliyoua watu 12 ikihusisha Basi la Kampuni ya AN Coach lililokuwa linatoka Mbeya kwenda Tabora, kupata ajali eneo la Luanjiro, Mbeya Vijijini.

Miongoni mwa waliofariki dunia katika ajali hiyo ya Septemba 4 mwaka huu ni mmiliki wa kampuni hiyo, Amduni Nassor huku wengine zaidi ya 36 wakijeruhiwa.

Hata hivyo, ajali hiyo ilitokea siku mbili baada ya nyingine kutokea Septemba 4, katika Kata ya Chimala, wilayani Mbarali mkoani Mbeya ikihusisha Basi la Kampuni ya Shari Line iliyosababisha vifo vya watu tisa na kujeruhi wengine 18.

Kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi Tanzania – Kikosi cha usalama barabarani ajali zilizorekodiwa kati ya mwaka  2019 na 2023 zilikuwa 10,174 sawa na wastani wa ajali 2035 kila mwaka.

Takwimu hizo zinaonyesha zaidi ya nusu za ajali (asilimia 53) zilisababisha kifo cha angalau mtu mmoja, huku mmoja alijeruhiwa.

Taarifa hiyo inabainisha, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Watanzania wanne hadi watano walifariki dunia kila siku kutokana na ajali za barabarani, wakati wengine saba hadi wanane wakijeruhiwa kila siku.

Related Posts