AKILI ZA KIJIWENI: Bora Msuva, Kapombe walivyorudi Stars

MJADALA hapa ni uteuzi wa kikosi cha Taifa Stars ambacho kitacheza mechi mbili za kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 dhidi ya Ethiopia na Guinea hapo baadaye.

Kuchaguliwa kwa Shomari Kapombe na Saimon Msuva ndiyo kumepokelewa vyema na washkaji hapa kijiweni na wanaamini wawili hao walipaswa kuitwa mapema.

Vijana tunaotegemea wabebe mikoba ya Kapombe na Msuva wametuangusha sana, sasa hakuna haja ya kuendelea kuwapa nafasi huku wakishindwa kuonyesha kitu ni bora tuwarudishie wenyewe tu.

Tukianzia kwa Msuva, mmejionea wenyewe namna Stars ilivyokuwa na pengo lake katika mechi mbili zilizopita dhidi ya DR Congo ambazo zote tulifungwa na kujikuta tukiangukia nafasi ya tatu kwenye kundi letu.

Msuva yule ana mbio zinazosaidia kuchosha mabeki wa timu pinzani, pia anajua kutumia nafasi kufunga mabao pale mpira unapomkuta akiwa karibu na goli la timu pinzani na hababaiki na ndiyo maana kaziamua mechi nyingi ngumu za Stars.

Inawezekana Msuva amepungua ubora siku hizi lakini ukiangalia kinachofanywa na vijana tunaowaita katika timu ya Taifa unaona bora nafasi aendelee kupewa huyo huyo kwa vile bado hawamfikii.

Ukija kwa Kapombe wote mmeona bado ameendelea kutamba pale Simba na vijana wanashindwa kumuweka benchi na ubora wake ameulinda licha ya umri kuanza kumtupa mkono.

Kuna wakati ubunifu wa kupika mabao unapaswa kuanzia kwa mabeki sasa ukiangalia kwa hapa nchini kwetu, beki wa kulia ambaye yuko vizuri katika kufanya hivyo, hakuna anayemzidi Kapombe na hatuoni dalili watamfikia lini.

Hapa kijiweni tulitegemea angeitwa Msuva, pia Kapombe kuingizwa kundini, tumefurahishwa zaidi.

Related Posts