Baresi awakingia kifua mastaa Mashujaa

BAADA ya vipigo viwili mfululizo, Kocha wa Mashujaa FC, Abdallah Mohamed ‘Bares’ amewakingia kifua wachezaji wake, uchovu ndiyo sababu ya kushindwa kuendana na kasi ya ushindani kutokana na kucheza mechi mfululizo.

Mashujaa imepoteza mbele ya Simba bao 1-0 nyumbani na imekubali kipigo cha pili dhidi ya Tabora United ugenini ikilala bao 1-0.

Akizungumza na Mwanaspoti, Bares alisema wachezaji wake wamecheza mechi zote kwa ubora aliouzoea kutokana na kufuata maelekezo yake na kilichowaangusha ni uchovu wa kucheza mechi mfululizo bila ya mapumziko.

“Tumetoka kucheza na Simba nyumbani tukasafiri kwenda kuifuata Tabora United, sio rahisi, nawapongeza wachezaji wangu na naamini tutarudi kwa nguvu baada ya mapumziko ya muda kupisha mechi ya Taifa Stars kufuzu Afcon 2026,” alisema na kuongeza;

“Mipango sio kupoteza, ilikuwa ni kukusanya pointi kwenye mechi zote lakini mbinu nzuri za wapinzani wetu zimetuadhibu. Tutarudi imara na kuendeleza ubora tulionao kwa kiasi kikubwa nina kikosi kizuri na kinapambana.”

Akizungumzia suala la usajili dirisha dogo alisema ni mapema sana kuzungumzia hilo lakini ikitokea nafasi ya kuongeza wachezaji atafanya hivyo lakini hadi sasa maeneo mengi ya kikosi chake yanafanya vizuri.

“Usajili ni Januari bado nina nafasi ya kupambana kukusanya pointi hapa katikati kabla ya dirisha kufunguliwa nawaamini wachezaji nilionao na wanafanya kazi nzuri hadi hapa tulipo licha ya kupoteza mechi tatu kati ya 10 tulizocheza.”

Related Posts