Beirut yapigwa tena huku Israel ikitanua operesheni Gaza – DW – 07.11.2024

Kiongozi wa Hezbollah, Naim Kassem, alisema katika hotuba iliyorushwa jana Jumatano kwamba kundi hilo litakuwa tayari kujadiliana usitishaji vita pale tu adui atakapositisha uvamizi wake, hotuba ambayo ilikuwa inaashiria kumalizika kwa kipindi cha maombolezo ya siku 40 tangu kuuawa kwa kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah, mjini Beirut.

Aidha, kiongozi wa juu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amesema muungano wa makundi yanayoipinga Israel unaendelea kuwa imara licha ya kuuawa kwa viongozi wao wengi, na amesisitiza kuwa ulimwengu utaona siku utawala wa Kizayuni utashindwa, akiongeza kuwa Hamas na viongozi wengine wa upinzani wanaendelea kupigana licha ya mashambulizi makali ya Israel.

“Adui hajaweza kulishinda shirika hili na hatoweza, Mungu akipenda. Ulimwengu na kanda hii watashuhudia siku ambayo utawala wa Kizayuni utashindwa waziwazi na wapiganaji katika njia ya Mwenyezi Mungu,” alisema Kahamenei.

Soma pia:Maelfu ya watu waandamana Israel kupinga kufutwa kazi kwa waziri wa ulinzi

Mashambulizi na operesheni za kijeshi za Israel katika miezi ya karibuni yameua viongozi wa juu wa Hamas Gaza na Hezbollah nchini Lebanon, pamoja na makamanda wao wao wa juu.

Makundi yote mawili ni sehemu ya mhimili wa upinzani unaojumuisha makundi mengine yanayoungwa mkono na Iran nchini Syria, Iraq, na Yemen.

Iran na washirika wake wameshambuliana mara kwa mara na Israel na Marekani katika kipindi cha mwaka mmoja uliyopita, kufuatia shambulio la Hamas la Oktoba 7, 2023, hali ambayo imeongeza hofu ya vita vya kikanda.

Jeshi la Israel lawataka wakazi wa Gaza kaskazini kuondoka ‘eneo la mapigano’

Jeshi la Israel limepanua operesheni yake ya ardhini kaskazini mwa Gaza hadi mji wa Beit Lahiya, ambao umepigwa mabomu tangu mwanzo wa vita.

Israel yazidisha mashambulizi katika ukanda wa Gaza

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Katika taarifa siku ya Alhamisi, jeshi lilisema vikosi vyake vimeanza kufanya operesheni katika eneo hilo baada ya taarifa za intelijensia kuonyesha uwepo wa wapiganaji.

“Tunawajulisha kuwa eneo lililotajwa linachukuliwa kuwa eneo hatari la mapigano. Kwa usalama wenu, hamieni kusini mara moja,” msemaji wa jeshi Avichay Adraee, alisema katika chapisho kwenye mtandao wa X, sambamba na ramani ya eneo hilo lililoko kaskazini-magharibi mwa mji wa Gaza.

Soma pia:Uchaguzi Marekani: Harris na Trump katika kampeni za mwisho

Wito huo wa karibuni zaidi unafuatia msururu wa maagizo ya kuhama kutoka maeneo makubwa ya kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, ambapo majeshi ya Israel yameongeza operesheni tangu mapema Oktoba.

Msemaji wa serikali ya Israel David Mencer aliwaambia waandishi wa habari kuwa “tunawatenga raia wa Gaza mbali na magaidi wa Hamas ili tuweze kuwapata magaidi” ambao bado wako katika eneo hilo.

“Hivi sasa, kuna wakazi wa eneo la kaskazini mwa Gaza ambao wamehamishwa hadi maeneo salama,” aliongeza.

Sheria mpya ya Israel inaweza kupeleka ndugu wa washambuliaji Gaza

Bunge la Israel (Knesset) limepitisha sheria Alhamisi inayoweza kuwafukuza ndugu wa watu wanaoshukiwa kwa mashambulizi ya “kigaidi” na kupelekwa katika Ukanda wa Gaza, hatua ambayo imeibua wasiwasi miongoni mwa wanaharakati wa haki za wachache wa Kiarabu.

Israel I Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akiwa Bungeni Picha: Maya Alleruzzo/AP/picture alliance

Sheria hiyo inamruhusu waziri wa mambo ya ndani kuwafukuza ndugu wa karibu wa mshukiwa kwa muda wa hadi miaka 20 ikiwa walijua mipango ya mashambulizi lakini hawakufanya kila lililowezekana kuzuia mashambulizi hayo.

Wanasiasa wa mrengo mkali wa kulia wamekuwa wakishinikiza sheria hii kwa miaka, wakiamini itawazuia raia wa Kipalestina wa Israel na wakazi wa Jerusalem ya mashariki iliyonyakuliwa kufanya mashambulizi dhidi ya Waisraeli.

Shirika la kutetea haki za jamii ya wachache wa Kiarabu nchini Israel la Adalah, limeielezea sheria hiyo kama uchochezi wa hatari hatari katika ukandamizaji wa kisheria wa haki za Wapalestina, ukifunikwa chini ya kivuli cha kupambana na ugaidi.

“Hatua hizi zinaiwezesha serikali kutoa adhabu ya pamoja kwa Wapalestina kwa kuidhinisha uhamishaji wa familia nzima,” ilisema Adalah katika taarifa.

Sheria hiyo, iliyowasilishwa na mbunge Almog Cohen, haijabaini mahali watu hao watapelekwa, lakini msemaji wa mwanasiasa huyo wa mrengo wa kulia aliiambia AFP kwamba uhamishaji utafanyika kuelekea Gaza, ambapo Israel iko katika vita na kundi la wapiganaji wa Kipalestina, Hamas.

Soma pia:Mashirika ya kimataifa yaonya juu ya kitisho cha njaa zaidi

Waziri wa mambo ya ndani pia atakuwa na mamlaka ya kuwafukuza wanachama wa familia wanaoonyesha kuunga mkono shambulizi au kuchapisha maneno ya kusifu au kutia moyo kitendo hicho au kwa kundi lolote la wapiganaji linalodaiwa kuwa nyuma yake.

Chini ya sheria hiyo mpya, raia wa Israel wanaweza kufukuzwa kwa muda usiopungua miaka saba hadi miaka 15, wakati wakazi wa kudumu au wa muda — kama Wapalestina wengi katika Jerusalem ya mashariki — wanaweza kufukuzwa kwa kipindi cha kati ya miaka 10 na 20.

Waziri wa Usalama wa Taifa, Itamar Ben Gvir, alisifu sheria hiyo na kuitaja kama “nguzo muhimu katika vita vyetu dhidi ya ugaidi.” Alisema katika taarifa kwamba inatuma “ujumbe wa wazi” kwa “familia za wahalifu.”

Related Posts