Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani, Boniface Jacob amesema chama hicho hakitakubali wagombea wa uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, kujiondoa kwa visingizio mbalimbali.
Jacob maarufu kwa jina la Boni Yai amesema wanajua kinachoendelea kuhusu uchaguzi huo na kuna kila dalili za wagombea wa upinzani kutafutwa ili kushawishiwa kujiondoa kwenye mbio hizo.
Hata hivyo, amewataka kutoingia kwenye mtego huo kwa sababu Chadema haitawavumilia.
Meya huyo wa zamani wa manispaa za Kinondoni na Ubungo, amesema hayo leo Alhamisi Novemba 7, 2024 wakati akizungumza na wagombea wa Dar es Salaam wa nafasi za uongozi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa katika uchaguzi utakaofanyika Novemba 27, 2024.
“Kwa hatua tuliofikia hatutakubali ujiondoe wakati huu, kwa sababu yoyote…ukijiondoa kwenye mchakato kisha kukimbilia sehemu fulani basi utatukuta huko huko, ukijiondoa Kinondoni na kukimbilia Bunju utatukuta hukohuko, tutakurudisha kwa gharama yoyote,” amesema Boni Yai ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema.
Amesema ingawa katika uchaguzi wa hivi sasa hakuna kupita bila kupingwa, amewataka wote waliopitishwa na chama hicho, kujiheshimu, kuacha tamaa na wale wenye njaa wavumilie.
“Kama ulichukua fomu kugombea, ukadhani nafasi hii ni ya biashara, basi biashara hii ni ya hatari acha. Ukiamua kuifanya tusilaumiane, maana kuna wanachama wenye uchungu hawakubali ujiondoe kirahisi au kukubali Chadema kuchezewa.
“Chonde chonde tusirudishane utumwani kama umeamua kulikoroga, basi utalinywa. Watu wa Dar es Salaam, hawana hiyana kama huna fedha za kampeni watakuchangia, hata ukiumwa watakupigia kura, kama mimi nilikuwa jela nikashinda uchaguzi wewe kwanini usishinde?,”amesema.
Pia, amesema hataki kusikia habari ya mgombea amefikiria au mke wake amemtaka ajiondoe kugombea, akisema muda huo kwa sasa haupo tena bali waingie kwenye uchaguzi kama kawaida.
“Hapa tulipofika sio muda wa kurudi nyuma bali kusonga mbele, tukimuona mwenzetu hatumuelewi tutaanza kumwekea alama ya kuuliza. Kura za maoni hakuwa ‘busy’, sasa hivi kampeni yupo busy haonekani kuna nini?,” amesema Boni Yai.
Katika hatua nyingine, Boni Yai amesema wapo tayari kwa ajili ya uchaguzi na watahakikisha wanafanya kampeni za kistaarabu zenye amani.
Amesema ustaarabu ndio jadi ya Chadema na hauwezi ukasikia vurugu kwenye mchakato wa kura za maoni za kuwapata wagombea watakaopeperusha bendera ya chama hicho.
“Ujumbe wangu wa leo kwa Watanzania tupo tayari kwa uchaguzi, tupo tayari kwa kampeni za amani na kistaarabu, lakini wakiamua kuhujumu uchaguzi, Chadema Mkoa wa Dar es Salaam hatutakubali,” amesema Boni Yai.
Kwa nyakati tofauti, Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa wamekuwa wakiwahakikishia Watanzania uchaguzi utakuwa huru na haki ukiongozwa na falsafa za Rnne (ustahimilivu, maridhiano, kujenga upya na mabadiliko).
Katika kikao hicho, Boni Yai aliwapokea makada kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao baadhi yao walienguliwa katika mchakato wa kura za maoni za chama hicho tawala uliofanyika Oktoba 23 hadi 24 mwaka huu.
Hata hivyo, Novemba 4, 2024, akizungumza na viongozi wa CCM wa Wilaya ya Kinondoni, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makalla aliwatakia kila la heri wanachama walioondoka baada ya kutopitishwa kwenye uteuzi.
Pia, Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Sheikh Ally Kadogoo amesema uchaguzi huo sio lelema kama ambavyo watu wanavyofikiria na ushindi hauwezi kuja kama kwenye sahani ya dhahabu pasipo watu kupambana.
“Tujiandae kwa mapambano hayo, kuelekea katika uchaguzi huu, kuanzia kupiga kura, kuzilinda aliyeshinda anatangazwa, hilo ndio jambo la muhimu.
“Adui tunayeshinda naye hana aya wala hofu yoyote, tusitegemee kupata huruma kwa kulalamika, sio wakati huu sasa,” amesema Kadogoo.
Kinachoendelea ACT-Wazalendo, CUF
Wakati huohuo, Chama cha ACT-Wazalendo kimedai wagombea wake kufuatwa na baadhi ya watu wanaowashawishi na kuwashinikiza kujiondoa kugombea nafasi hizo.
ACT-Wazalendo kupitia msemaji wa sekta ya Tamisemi, Rahma Mwita imedai watu hao wamekuwa wakishiriki vitendo hivyo kwa kupiga simu kwa wagombea wa chama hicho.
Mwita ametaja maeneo ambayo wagombea wanasumbuliwa ni Tandahimba (Mtwara) Kondoa Mjini, Kondoa Vijijini, (Dodoma) Kilwa, (Lindi) Chalinze, (Pwani) Kigoma Mjini, Nyamagana (Mwanza)
“Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi mgombea hawezi kujitoa kabla ya uteuzi, hivyo barua yoyote ya watu kujitoa kabla ya siku ya uteuzi ni batili na kinyume na kanuni za uchaguzi,” amesema Mwita.
“ACT Wazalendo hatutakubali, uwekezaji mkubwa tulioufanya katika kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uharibiwe na wasimamizi, wasikubali kupokea barua za wagombea kujitoa kabla ya uteuzi kufanyika.”
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu wa CUF- Bara, Magdalena Sakaya amesema chama hicho kimepokea malalamiko ya wagombea wao kutishwa na kutakiwa kujitoa katika uchaguzi huo.
“Hapa natoka ofisini kujadili masuala hayo, hili limekuwa tatizo kubwa kila sehemu tuliosimamisha wagombea, kuna maeneo wanaitwa na kulazimishwa kujaza fomu ya kujitoa pasipo wao kujua, hiki ni kitu cha aibu kinachofanyika.
“Leo tuna siku ya nne tunapambana nayo haya malalamiko kila sehemu wagombea wetu wanatishwa ili kujitoa,” amesema Sakaya.
Amesema kabla ya mchakato huo kuanza walishawajengea uwezo wagombea kuhusu namna watakavyoshiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.
“Huwa tuna utaratibu wa kuwajengea uwezo wagombea na mawakala kuhusu mwenendo mzima wa uchaguzi huu ili kujua wajibu wao. Mahali ambako wagombea wetu watafanikiwa kupenya, tutapeleka timu ya vijana wetu ili kuendesha vema kampeni zao na namna ya kuomba kura,” amesema Sakaya.
Wakati kesho Ijumaa Novemba 8 ndiyo siku ya uteuzi wa wagombea watakaoshiriki huo uchaguzi huo, Boni Yai amewataka watia nia wa Chadema kujitokeza kwenye ofisi za mitaa kuangalia orodha ya majina yatakayobandikwa na Serikali kama wao.
“Safari hii hakuna mgombea wa Chadema aliyejaza fomu peke yake, tulikuwa na wanasheria wa kanda waliokuwapo kila kata kutoa usaidizi. Kisingizio chochote kwamba fomu imekosewa kujazwa, maana itakuwa uongo hatutakubali.
“Tutakuwa tayari kukubali endapo mgombea wetu, atakatwa kwa matakwa ya Katiba au kukosa ikiwamo umri, akili timamu, Mtanzania. Hizi sifa zote tulilizingatia kabla ya kutoa fomu, kinyume cha hapo, hatutakubali mgombea kukatwa,”amesema Boni Yai.