Dodoma. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza ukaguzi wa kampuni zote za urasimishaji ardhi ili kuona uwezo wao wa kutekeleza majukumu ambayo wamekuwa wakienda kuomba katika halmashauri nchini.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi amesema hayo bungeni leo Novemba 7, 2024 alipojibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi.
Mbunge huyo katika maswali amesema Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikishwa Ardhi (KKK) lakini inavyoonekana hakuna ufuatiliaji mkubwa wa fedha hizo kiasi kwamba miradi hiyo haifanyiki kwa ufanisi.
“Je? Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati,” amehoji.
Shangazi pia, amesema wananchi wa Pugu katika Jimbo la Ukonga mkoani Dar es Salaam wengi wao wako katika mpango wa KKK na wameshalipa Sh250,000 kwa kila kaya lakini mpango huo umesimama.
Amehoji ni nini mpango wa Serikali kuhakikisha wananchi wanarasimishiwa ardhi zao.
Ndejembi amesema Serikali imeweka fedha nyingi katika mradi wa KKK na wanashirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa kuwa fedha hizo zinakwenda katika Serikali za mitaa.
Amesema mamlaka ya Serikali za mitaa zilichagua maeneo wanayoyataka kuyapima, kuyapanga na kumilikisha na kwamba, kuna maeneo ambayo hawakutumia fedha hizo kwa yale yaliyokusudiwa, badala yake walipeleka pesa hiyo kwenye shughuli nyingine.
“Niwasifu Tamisemi na kuwapongeza wamekuwa wakishirikiana na sisi kwa karibu sana kupitia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tamisemi kuhakikisha fedha zinarejeshwa,” amesema.
Kuhusu Jimbo la Ukonga, Ndejembi amesema Jiji la Dar es Salaam liliingia mkataba na kampuni za urasimishaji ambazo zilikwenda kuchukua fedha kwa wananchi lakini hazikukamilisha kazi hiyo.
Amesema wizara imeingilia suala hilo ili kuhakikisha wananchi waliotoa fedha zao wanapata urasimishaji.
Waziri amesema wanafanya kazi kwa karibu na Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha wananchi wanapata urasimishaji walioutarajia.
“Vilevile tumeanza kufanya ukaguzi wa hizi kampuni zote za urasimishaji ili tuweze kuona uwezo wao wa kutekeleza majukumu ambayo wanakwenda kuyaomba katika halmashauri,” amesema.
Mwananchi ilipomtafuta Waziri Ndejembi nje ya ukumbi wa Bunge kuhusu hatua watakazochukua kwa kampuni ambazo zitabainika kutokuwa na uwezo wa kazi walizoomba katika halmashauri, amesema katika kukwamua kazi ya urasimishaji makazi baadhi ya kampuni zimechukuliwa hatua.
Amesema kampuni 15 kati ya zilizobainika kukiuka maadili ya taaluma zao, zimechukuliwa hatua ikiwemo kufikishwa kwenye vyombo vya uchunguzi, kufungiwa kufanya kazi na kupewa onyo.
“Hatua hiyo inahusisha kampuni zilizokusanya fedha nyingi za wananchi lakini hazina uwiano na kazi zilizotekelezwa,” amesema.
Amesema kazi ya ukaguzi inashirikisha Serikali za mitaa na imeanza Novemba mwaka huu, akieleza wataongeza kasi katika shughuli hiyo.
Amesema wizara ina mpango wa kukamilisha na kukwamua kazi za urasimishaji ambazo hazikukamilika kama alivyoeleza bungeni.
Katika swali la msingi, mbunge wa Mpendae (CCM), Toufiq Salim Turky amehoji kuna mpango gani wa kudhibiti ukuaji wa makazi katika maeneo ambayo hayajapimwa na kupangwa kuwa makazi ya wananchi.
Waziri amesema wizara kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi na mamlaka nyingine za upangaji katika kukabiliana na ukuaji wa makazi yasiyopangwa, imeendelea kuchukua hatua mbalilmbali.
Amezitaja hatua hizo kuwa ni kuendelea kuandaa mipango kabambe yenye dira ya kusimamia ukuaji wa miji, akieleza 28 imeandaliwa.
Amesema wizara imeanzisha miradi na programu mbalimbali kwa ajili ya kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi nchini na kuandaa Mwongozo wa Upangaji na Ujenzi wa Nyumba Bora Vijijini wa mwaka 2023 ili kudhibiti ukuaji holela wa vitovu vya vijiji kama miji tarajiwa ya baadaye.