Kongamano la kimataifa la madini kufanyika Dar

Dar es Salaam. Zaidi ya washiriki 1,000 wakiwemo wafanyabiashara, wachimbaji wa madini wakubwa na wadogo wanatarajia kuhudhuria kongamano la kimataifa la madini linalotarajiwa kufanyika kwa siku tatu nchini.

Kongamano hilo litakalofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 19 hadi 21, 2024 litahudhuriwa na mabalozi wanaowakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani na wale wanaowakilisha mataifa ya nje nchi.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Yahaya Samamba leo Alhamisi Novemba 7, 2024 kwenye mjadala wa Mwananchi X-Space (zamani Twitter) ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na Wizara ya Madini na Chemba ya Migodi Tanzania wenye mada isemayo: ‘Tulipo, tunapokwenda, kuelekea mkutano wa kimataifa wa uwekezaji katika sekta ya madini Tanzania.’

Amesema mkutano huo pia utahusisha kampuni za madini zilizowekeza Tanzania na ambazo hazijawekeza.

“Mada zitakazozungumziwa ni rasilimaliwatu, sheria na vivutio vingine na kuwahakikishia kuwa nchi iko salama kwa ajili ya kuwekeza, hii ni kwa manufaa ya sasa,” amesema.

Samamba amesema uwepo wa mkutano huo ni fursa kwa wachimbaji waliopo nchini kujifunza kinachofanyika kwa wengine, kukutana na wanaofanya kazi hiyo kwa miaka mingi iliyopita ambao watasaidia kujua namna ya kuwekeza vizuri zaidi.

Amesema anaamini kuna maeneo ambayo yakiwekewa mfumo mzuri, sekta ya madini inaweza kuleta manufaa makubwa kwa nchi.

Miongoni mwa hayo amesema ni ushirikishwaji wa wazawa kupitia kuweka mfumo mzuri wa Watanzania kuajiriwa, bidhaa za Tanzania kununuliwa kwa kuzifungamanisha na maeneo mengine, watu kupata mafunzo na uhamishaji wa teknolojia.

Akizungumzia kaulimbiu ya kongamano hilo inayohamasisha uongezaji wa thamani wa madini, amesema ni muhimu kutokana na faida zake.

“Unapokuwa na rasilimali inayochimbwa na kusafirishwa kama malighafi maana yake ajira zitakwenda kuzalishwa huko. Pia Unaacha madini mengine kama shaba, fedha na unakwenda kukuza uchumi wa nchi hiyo wakati uchumi wa nchi yako ukididimia,” amesema.

Wakati hilo likifanyika, Serikali imeshaanza mchakato wa kuhakikisha madini yanayochimbwa Tanzania yanaongezwa thamani, akieleza siku za usoni hakutakuwa na ruhusa ya kusafirisha madini ambayo hayajaongezwa thamani ndani ya nchi.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Madini Tanzania (Stamico), Deusdedith Magala amesema kupitia kongamano hilo ni vyema kutangaza kuwa nchi ina makaa ya mawe ili kupata uwekezaji.

Amesema miongoni mwa vitu vinavyoweza kufanyika ni kuvutia uwekezaji kuzalishaji umeme kupitia eneo hilo.

“Ili tuweze kuzalisha angalau megawati 400 kupitia makaa ya mawe, hivyo kupitia mkutano huu nafikiri ni nafasi pekee ambayo tunaweza kuitumia kunadi makaa yetu. Kuzalisha megawati 400 ni fedha nyingi ni karibu Dola 500 milioni za Marekani,” amesema.

Related Posts