Lwasa: sasa nitafunga sana! | Mwanaspoti

KIUNGO mshambuliaji wa Kagera Sugar Mganda, Peter Lwasa amesema baada ya kuondoka kwa aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Paul Nkata, alihisi huenda angepitia changamoto ya kucheza ingawa anashukuru ameendelea kuaminiwa na benchi jipya.

Nyota huyo aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu baada ya kuachana na KCCA FC ya kwao Uganda, alisema Nkata ndiye sababu kubwa ya kujiunga na Kagera hivyo alijisikia vibaya kuondoka kwake, kwani alimuamini kupita kiasi na hakumuangusha pia.

“Unajua ukiwa mchezaji kuna wakati unaona maisha yanaenda kuharibika hasa anapokuja mtu mwingine tofauti na yule ambaye umemzoea, Nkata alikuwa ananikubali sana na nashukuru sikumuangusha japo tumepitia kipindi kigumu kikosini,” alisema.

Nyota huyo mwenye mabao manne ya Ligi Kuu Bara huku akiwa ndiye anayeongoza ndani ya kikosi hicho aliongeza, hata baada ya ujio wa Melis Medo ndani ya timu hiyo bado alionyesha imani kubwa kwake jambo linalompa motisha ya kupambana zaidi.

“Baada ya kukaa naye kwa muda mchache ameonyesha imani kubwa juu yangu, nashukuru pia ameniamini na kuna wakati anataka nisicheze mbali na lango la wapinzani wetu tunaokutana nao, kiukweli imeniongezea motisha japo ni deni linalonikabili.”

Nkata aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwamo SC Villa na Express FC za kwao Uganda, alijiunga na Kagera Agosti 10, mwaka huu na kutimuliwa Oktoba 10, kutokana na matokeo mabovu, kisha kikosi hicho kukabidhiwa Mmarekani Medo Oktoba 17.

Tangu kocha huyo achukukue nafasi ya kukinoa kikosi hicho, alikiongoza katika jumla ya michezo saba ya Ligi Kuu Bara kwa msimu huu wa 2024-2025, ambapo kati yake alishinda mmoja, sare mmoja na kupoteza mitano akiiacha nafasi ya 14 na pointi nne.

Related Posts