Malijendi wampa ujanja mpya Manula

KIPA wa Simba, Aishi Manula imeelezwa anapaswa kurudisha morali na kujiamini, ili kurejesha kiwango chake kitakachomshawishi kocha wa Simba, Davis Fadlu kumtumia kikosi cha kwanza.

Msimu uliopita Manula alikaa nje kwa muda mrefu akiuguza majeraha, baada ya kurejea akadaka mechi dhidi ya Yanga, Simba ikifungwa mabao 5-1 Novemba 6, 2023 na tangu hapo hajawa na namba kikosini.

Kipa wa zamani wa Simba, Idd Pazi alisema alimtazama Manula mechi dhidi ya Sudan ya kufuzu michuano ya CHAN na alichogundua amepoteza kujiamini na morali yake ipo chini.

“Manula ni kipa mzuri, apambane kuhakikisha anaposimama golini anajiamini, naona yupo fiti, hivyo ni suala la muda kuanza kucheza na kutegemewa na Simba.

Aliongeza; “Jambo la msingi katika akili yake asahau yaliopita, ajue soka ni kazi yake, apambane bila kujali nani anaongea nini, kazi yake uwanjani ndiyo iwe na nguvu ya kuwashawishi watu kuanza kuzungumzia anachokifanya, hilo litamsaidia kumrejesha katika mstari.”

Aliyekuwa kocha wa makipa Mtibwa Sugar, Patrick Mwangata alisema kiufundi Manula yupo vizuri, anachokiona kinamsumbua ni kupoteza kujiamini na morali yake kushuka.

“Makocha waanze kumwamini, kwani mwili wake kwa sasa una utimamu na kiufundi yupo sawa, akicheza mechi kama sita ama saba, atarudisha makali yake, kwani bado ni kijana pia Taifa linamtegemea,” alisema.

Wakati wadau wakiiona changamoto hiyo kwa Manula, kuna tetesi huenda msimu ujao kipa huyo asiwe sehemu ya kikosi hicho.

Related Posts