Dar es Salaam. Mshtakiwa Hamisi Said Luwongo anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya mkewe, Naomi Orest Marijan na kuuteketeza mwili kwa moto ameulalamikia upande wa mashtaka kwa kile alichokiita kuchelewesha kesi hiyo huku akidai inafuatiliwa hata na Rais.
Mshtakiwa huyo anayekabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam ametoa malalamiko hayo mahakamani leo Alhamisi, Novemba 7, 2024, baada ya shahidi wa upande wa mashtaka na shahidi pekee kwa leo, kumaliza kutoa ushahidi wake.
Hamisi, mkazi wa Gezaulole, wilayani Kigamboni, jijini Dar es Salaam anakabiliwa na kesi ya mauaji ya mkewe huyo kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kana ilivyorejewa mwaka 2019, akidaiwa kutenda kosa hilo Mei 15, 2019.
Anadaiwa baada ya kumuua mkewe aliuchoma mwili wake kwa kutumia magunia mawili ya mkaa na kisha akaenda kuzika majivu yake shambani kwake.
Kesi hiyo iko katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka.
Leo baada ya shahidi wa 10 kumaliza ushahidi wake, mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwasiti Ally ameieleza mahakama haikuwa na shahidi mwingine na kwamba shahidi wao mwingine waliyemtegemea ambaye ni mkemia amesafiri nje ya nchi na anatarajia kurudi Novemba 10, 2024.
Hivyo Wakili Mwasiti ameiomba Mahakama itoe ahirisho mpaka tarehe nyingine ili kummalizia mashahidi waliobakia.
Alipoulizwa na Jaji Hamidu Maanga idadi ya mashahidi waliobakia, Mwasiti amejibu wamebakia watatu, kuwa mbali na huyo mkemia bado kuna mpelelezi na mtunza vielelezo.
Kutokana na maelezo Jaji Mwanga amesema kesi hiyo ilipangwa kuisha leo lakini akasema kuendelea nayo Jumanne, Novemba 12, 2024 ili iishe, huku akitoa tahadhari pande zote kuwa zijiandae kwa hilo.
“Mjue siku hiyo naahirisha kesi nyingine, kwa hiyo mtu ambaye hatakuwa na shahidi ananitafuta ubaya,” amesema Jaji Mwanga na kusisitiza kama shahidi huyo atakuwa hajarudi atasikilizwa huko huko nje kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano ya video (video conference).
Hata hivyo, baada ya maelezo hayo ya Jaji mshtakiwa huyo Hamisi ameomba nafasi na alipopewa na Jaji ndipo akatoa malalamiko yake, huku akihoji kama shahidi huyo mmoja yuko na wapo wengine akiwemo mpelelezi kwa nini upande wa mshtaka wasingemleta leo ili kuokoa muda.
“Mheshimiwa upande wa mashtaka umesema bado kuna mashahidi watatu. Kama mkemia yuko nje ya nchi lakini huyo mpelelezi yupo, kwa nini wasimlete kuokoa muda,” amesema Hamis na kuongeza:
“Kesi hii inafuatiliwa na pande zote na jamii inataka kujua hatima yake na hata Rais anafuatilia lakini upande wa mashtaka wanachelewesha hii kesi.”
Jaji Mwanga amemweleza kesi zote zinafuatiliwa si yake tu bali hata nyingine za mauaji kwa hiyo haijalishi nani anafuatilia lakini akamtuliza kuwa ndio maana ametafuta nafasi nyingine ya kumalizia kesi hiyo ambayo ilipaswa iishie leo.
Pia Jaji Mwanga amemfafanulia mshtakiwa huyo anaelewa kwa nini mpelelezi hajaja maana vielelezo vya mkemi kuwa kama vimefungwa mpelelezi hawezi kuvifungua mpaka mkemia kwanza aje avifungue.
Awali, shahidi wa 10 Mkaguzi wa Polisi, Filibert Rwegasira Katabazi (54) katika ushahidi wake akiongozwa na kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Yasinta Peter ameieleza Mahakama jinsi alivyohusika katika upelelezi wa kesi hiyo.
Amesma wakati wa tukio hilo alifanya kazi katika Kituo cha Polisi Chang’ombe ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya (OC-CID) na kwamba Juni 13, 2019 alikabidhiwa jalada la taarifa ya kutokuonekana kwa Naomi iliyokuwa imetolewa na kaka wa Naomi, Ismail Orest Marijani.
Amesema alikwenda huko Kigamboni Gezaulole akiongozana na askari watatu na Ismail hadi nyumbani kwa mshtakiwa ambaye hawakumkuta lakini walimpigia simu na alipofika walijitambulisha kwake na kumweleza wanamtafuta Naomi Orest Marijan na Hamisi akasema anamfahamu ni make wake.
“Tulimuuliza yuko wapi akasema hafahamu na yeye pia anamtafuta,” amesema Katabazi na kuongeza Hamisi alifungua mlango wakaingia ndani na wakaangalia vyumba vyote lakini hawakumpata.
Amesema Hamis akawaandikia namba za simu za Naomi namba ya akaunti ya Naomi ya Benki ya Posta na kisha wakaandika maelezo yake kuwa anajua nini kuhusu mkewe.
“Katika maelezo alisema na yeye hafahamu chochote isipokuwa alipokea ujumbe mfupi (sms) kutoka kwa Naomi ikieleza mimi naondoka naenda zangu nje ya nchi….,” amesema Katabazi akimnukuu Hamisi akielezea ujumbe huo.
Amesema walirudi kituoni wakaandika barua kwenda kwenye kampuni za simu za Tigo na Airtel kwa namba za Naomi ambazo Hamis aliwapa ili kujua mawasiliano ambayo yalifanyika kwenye namba hizo za simu na barua nyingine kwenda Benki ya Posta.
Katabazi amesema katika taratibu za upelelezi mtu ambaye alikuwa karibu kusaidia kutupa taarifa alikuwa ni mumewe Naomi, Hamisi hivyo alikuwa anafika kituoni hapo ofisini kwake mara kwa mara.
Amesema Julai 3, 2019 walitaka namba za simu za Hamisi ambazo alikuwa ametumiwa zile meseji na Naomi, wakagundua Naomi alikuwa na simu nyingine na walipomuuliza Hamis mahali zilikokuwa akasema ziko kwenye mkoba wake uko nje kwenye gari aina ya Subaru.
Shahidi huyo amesema walikwemda kuzichukua mkoba huo lakini wakamchukua simu za Hamis kuzifanyia uchunguzi.
Amesema Julai 6, 2019 Hamisi alifika kituoni baada ya kumpigia simu wakamchukua pamoja na jalada la uchunguzi huo wakampeleka ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Kanda (ZCO).
“Tangu nilipomfahamu Hamisi hiyo Juni 13 na alikuwa kwangu ofisini mara kwa mara alikuwa ni mzima wa afya alikuwa mzima wa akili,” amesema Katabazi.
Hata hivyo, akihojiwa maswali ya dodoso na mawakili wa utetezi, Mohamed Majaliwa (kiongozi wa jopo) na Zidadi Mikidadi, Katabazi amesema hakuwahi kupata majibu ya barua walizoziandikia kampuni za Tigo na Airtel na wala barua hizo hakuzitoa mahakamani hapo.
Pia amekiri hakutoa ushahidi kuthibitisha ujumbe ambayo mshtakiwa Hamisi aliwaleza aliandikiwa na Naomi.
Kwa mujibu wa maelezo na ushahidi wa upande wa mashtaka Julai 16, katika Kituo Kikuu cha Polisi, wakati akihojiwa na ofisa wa Polisi mshtakiwa alikiri kumshambulia na kumuua mkewe Mei 15, 2019 ndani ya nyumba yao.
Kisha aliuchukua mwili wake na kwenda kuuchoma moto katika banda lililokuwa limeandaliwa, kwa kutumia mkaa na vitu vingine alivyokuwa ameviandaa.
Anadaiwa aliondoa majivu na masalia mengine kwa kutumia gari lake aina ya Subaru Forester lenye namba za usajili T 206 CEJ mpaka shambani kwake katika kijiji cha Marogoro, wilayani Mkulanga, mkoani Pwani, ambako aliyazima katika mashimo yaliyokuwa yameandaliwa kisha kapanda migomba.
Siku hiyohiyo, Julai 16, 2019 mshtakiwa aliongozana na maofisa wa polisi na maofisi wengine mpaka eneo la tukio (nyumbani) na kisha shambani ambako ofisa kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali alichukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba (DNA).
Matokeo ya uchunguzi wa sampuli hizo yalionesha majivu yale yalikuwa ni ya binadamu ambayo yalioana na baadhi ya ndugu wa marehemu Naomi.
Kisha maelezo ya ziada ya mshtakiwa yalichukuliwa na Mlinzi wa Amani (Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo), ambako pia alikiri kutenda kosa hilo.