Wiki hii kumekuwa na maendeleo chanya kwenye masoko ya fedha na mitaji ambapo tumeshuhudia uwepo wa fursa za uwekezaji kupitia vipande, hatifungani na pia hisa.
Pia tumeona kuwa mabenki, hasa yaliyoorodheshwa kwenye soko la hisa na mitaji yakiripoti kufanya vizuri kwenye mawasilisho ya robo ya tatu ya mwaka.
Inapotokea nafasi kama hizi ni wakati wa kufikiria kuwekeza kwa sababu kuna utafiti ambao utakuwa umefanyika na kuwa kuna matarajio mazuri mbeleni.
Linapokuja suala la kuwekeza, wengi wanaweza kudhani kwamba uwekezaji ni kwa wale wenye kipato kikubwa au waliobobea kwenye masuala ya fedha, lakini ukweli ni kwamba, uwekezaji unapatikana kwa kila mtu – na ni njia thabiti ya kujenga urithi wa kifedha kwa muda mrefu. Pia si kwamba unatakiwa kuwa na fedha nyingi ili uweze kuanza, bali ni kuanza kujijengea tabia ya kuwekeza.
Uwekezaji ni kuchukua sehemu ya mapato yako na kuiweka kwenye mali au miradi ambayo itakua kwa thamani kwa muda na kukuletea faida zaidi.
Unaweza kuwekeza kwenye hisa, vipande, hatifungani, au hata kwenye mali kama nyumba au ardhi. Njia hizi za uwekezaji zinalenga kukusaidia kutengeneza faida zaidi ya kile unachoweza kupata kupitia akaunti za akiba tu au kuweka pesa nyumbani.
Kuna fursa zinazopatikana kwa mwezi huu wa Novemba na Desemba. Kuna aina tatu kuu za uwekezaji zinazopatikana kwa watu wa kipato chochote. Aina hizi ni pamoja na hisa, vipande (au mutual funds), na hatifungani.
Kwa hisa, Benki ya DCB inauza hisa kwa ambao tayari wanamiliki hisa za DCB. Kama unamiliki hisa DCB unaweza kuwasiliana na Wakala wa Soko la Hisa.
Pia ununuaji na uuzaji wa hisa unafanyika kupitia mawakala wa Soko la Hisa na unaweza kuamua kununua hisa. Azania Bank imetangaza kuuza hatifungani ya miaka minne kwa kiwango cha chini cha uwekezaji cha shilingi laki 5.
Bondi itakuwa inalipa asilimia 12.5 kwa kila robo ya mwaka. Vilevile kampuni ya uwekezaji ya iTrust imetangaza kuuza vipande vya aina tano tofauti ambavyo ni kwa ajili ya kuwekeza na mauzo yanafanyika ndani ya hii miezi miwili.
Unapowekeza kwenye hisa, unakuwa unamiliki sehemu ndogo ya kampuni inayouza hisa zake kwenye soko la hisa. Hii inamaanisha kuwa, kampuni inapopata faida, nawe unafaidika kwa namna fulani.
Faida hii inaweza kuja kwa njia ya gawio – yaani, sehemu ya faida ya kampuni inayotolewa kwa wamiliki wa hisa, au kwa ongezeko la thamani ya hisa unazomiliki. Kukiwa na hasara hakuna gawio.
Unapowekeza kwenye vipande unapata nafasi ya kumiliki sehemu ya miradi au mali zinazozalisha kipato. Hapa, fedha za wawekezaji mbalimbali hukusanywa pamoja na kuwekeza kwenye maeneo mengi tofauti, kama vile hisa za makampuni, hatifungani, na mali nyinginezo.
Uwekezaji wa hatifungani ni aina ya mkopo ambapo wewe, kama mwekezaji, unakopesha taasisi kama kampuni ambayo inazitumia kutekeleza mpango wake wa kibiashara.
Hati fungani inakupa uhakika wa kupata faida kwa njia ya riba. Hii ni njia nzuri ya kupata kipato cha ziada kwa riba, wakati ukiweka mtaji wako katika hatari ndogo ukilinganisha na uwekezaji wa hisa.
Fursa za uwekezaji zipo – chaguo ni lako.