ACHANA na ushindi wa kwanza wa Pamba Jiji walioupata jana ugenini, Kipa wa Fountain Gate, Fikirini Bakari anakuwa miongoni mwa makipa watano Ligi Kuu kufanya makosa ya kuzigharimu timu zao.
Pamba Jiji iliyopanda Ligi Kuu msimu huu, ilikuwa timu pekee iliyokuwa haijaonja ushindi wowote kwenye michezo 10 iliyocheza na kuwa katika nafasi mbili za mkiani.
Juzi ikicheza katika kiwango bora kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, mkoani Manyara, iliichakaza Fountain Gate mabao 3-1 na kufufua upya matumaini ya kujiweka pazuri kwenye msimamo.
Hata hivyo, licha ya ushindi huo ulioamsha mzuka kwa mashabiki wa TP Lindanda ndani na nje ya Jiji la Mwanza, Bakari atajilaumu kwa mpira wa faulo alioupiga bila hesabu na kujikuta timu yake ikifungwa bao la tatu.
Wakati Fountain Gate ikiugulia maumivu ya kipigo hicho, kipa huyo anaungana na makipa wengine wanne waliofanya makosa na kujikuta timu zao zikipoteza mechi muhimu.
Wengine waliofanya makosa kama hayo ni Mussa Mbisa wa Tanzania Prisons dhidi ya Simba na wakati akiokoa mpira wa faulo wa Kibu Denis mpira wake ulimponyoka na Che Malone kuusukuma wavuni.
Fabien Mutombora wa KMC naye alijikuta akifanya makosa wakati wa mechi yao dhidi ya Fountain Gate baada ya mpira wa faulo uliopigwa na Dickson Ambundo na kumpita katikati ya miguu yake.
Moussa Camara wa Simba naye aliigharimu timu yake alipopangua mpira wa faulo na Clatous Chama (Yanga) ambao ulionekana unatoka nje na kuurejesha uwanjani na kujikuta Kelvin Kijili kujifunga kwenye piga nikupige golini mwao.
Denis Richard wa JKT Tanzania aliigharimu timu hiyo wakati wakinyukana dhidi ya Yanga na alishika mpira nje ya eneo lake akiokoa shuti la Pacome Zouzoua na kuonyeshwa nyekundu.
Kipa wa zamani wa Simba, Idd Pazzi alisema bado yapo mapungufu kwa makocha wa eneo hilo namna ya kuwafundisha makipa jinsi ya kusimama golini na kushika mipira.
“Eneo la golini ni pagumu sana, naona kuna upungufu kwa makocha namna ya kuwaelekeza na kuwafundisha makipa wenyewe namna ya kukaa langoni na kushika mipira,” alisema Pazzi.