Wakuu wa mataifa na viongozi wengine wa ngazi ya juu kote duniani wakiwemo kutoka barani Afrika wamempongeza Donald Trump kwa ushindi wake.
Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi amemtakia Trump kila la heri na mafanikio katika jitihada za kufikia malengo ya watu wa Marekani. Amesema anatumai kushirikiana naye katika kurejesha amani, kuendeleza utulivu wa kikanda na kuimarisha ushirikiano kati ya Misri na Marekani.
Soma zaidi: Viongozi wa dunia wamimina pongezi kwa Trump
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed wa Ethiopia kupitia ukurasa wake wa jukwaa la mtandao wa kijamii wa X ameandika kuwa anatazamia kufanya kazi pamoja na Trump katika kuimarisha uhusiano wa nchi yake na Marekani katika muhula utakaoanza wa uongozi wa Trump.
Naye Rais wa Afrika ya Kusini Cyril Ramaphosa amempongeza Donald Trump akitarajia kuwa kiongozi huyo wa Marekani ataendeleza ushirika wenye manufaa kati ya nchi hizo mbili katika nyanja zote.
Aidha, Ofisi ya Rais wa Nigeria Bola Tinubu imetoa kauli kuhusu ushindi wa Trump ikisema kuwa unaakisi imani waliyoiweka Wamarekani katika uongozi wake na kwamba pamoja Nigeria na Marekani zinaweza kukuza ushirikiano wa kiuchumi, amani na kushughulikia changamoto zinazowaathiri raia katika mataifa hayo.
Iran: Uchaguzi wa Marekani hautuhusu
Mbali na pongezi kutoka Afrika msemaji wa serikali ya Iran Fatemeh Mohajerani imesema matokeo ya urais ya Marekani hayana athari kubwa kwa Iran.
Amesema kuwa, uchaguzi wa Rais wa Marekani hauihusu Iran na kuwa sera muhimu za Marekani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hazibadiliki na hazitabadilika kwa kiasi kikubwa kwa kubadilisha watu.
Kando ya Iran, Waziri Mkuu wa Japan Shigeru Ishiba amesema angependa kufanya kazi kwa karibu Trump katika kuukuza uhusiano wa nchi zao.
Soma zaidi: Trump arejea Ikulu ya White House kwa ushindi wa kushangaza
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amempongeza Trump na kusema ana matumaini kuwa kupitia uongozi wake mizozo ya kikanda na ya dunia itakoma hasa mzozo wa Palestina.
Wizara ya mambo ya kigeni ya China imesema taifa hilo litaendelea kuushughulikia uhusiano wa China na Marekani kwa misingi ya kuheshimiana.
Pongezi nyingine kwa Trump zimetolewa na Mfalme Salman na Mwanamfalme Mohammed bin Salman wa Saudi Arabia, Mfalme Abdullah II wa Jordan, Rais wa Taiwan Lai Ching-te, Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil, Yoon Suk Yeol wa Korea Kusini na Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk.