Sababu Geita kukubwa na mafuriko zatajwa

Geita. Uchunguzi uliofanywa na kamati ya maafa ya Wilaya ya Geita umebaini chanzo cha mafuriko yaliyotokana na mvua iliyonyesha kwa saa moja ni ujenzi kwenye njia za asili za kupita maji na uchafu kutupwa kwenye mitaro.

Uchunguzi huo umewekwa hadharani Novemba 6, 2024 mjini Geita, ikiwa ni siku moja baada ya mafuriko hayo kutokea, huku ikiripotiwa watu 15 walijeruhiwa kutokana na mafuriko hayo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Wilaya ya Geita, Hashim Komba amesema hayo alipozungumza na wananchi na wafanyabiashara walioathiriwa na mafuriko hayo.

Amewataka wananchi kuzingatia usafi wa mazingira na kutotumia mvua kama kichaka cha kutupa uchafu kwenye mitaro.

“Kilichojitokeza ni baadhi yetu kutozingatia usafi wa mazingira, mitaro ilijaaa viroba vya taka. Nawasihi msitumie mitaro ya maji kutupa takataka, mtu anakusanya taka nyumbani anazitunza mvua ikinyesha anatupa kwenye mtaro, hii inasababisha njia za maji kuziba. Kuweni mabalozi wa kutunza mazingira,” amesema.

Komba amewataka wananchi kutoa taarifa wanapoona mtu akijenga kwenye njia za asili za maji kupita ili kuepuka kuziziba na kusababisha madhara yasiyo ya lazima mvua inaponyesha.

“Tusaidiane kwenye maeneo tunayoishi tunapoona kuna njia ya asili ya maji na mwananchi akajenga toeni taarifa mapema ili achukuliwe hatua. Njia za kupeleka maji kutoka hapa stendi zimezibwa na makazi ya watu maji yakijikusanya yanarudi nyuma, lazima tuchukue hatua kali kwa hawa wanaoziba njia za maji ili kuepuka madhara mengine,” amesema.

Kamati hiyo pia imeunda timu ya wataalamu ikiongozwa na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Geita itakayofanya kazi kwa siku 14 kukagua maeneo yaliyoathiriwa na kufanya tathmini ya nini kifanyike ili changamoto iliyojitokeza isijirudie.

“Tunataka ndani ya siku 14 kamati hii ije na majibu ni namna gani shughuli zitafanyika kwenye eneo la stendi sambamba na kuangalia njia za maji ambazo watu wamejenga, mapokeo ya maji yanapoelekea, na mdomo wa kupokea maji kuyapeleka mtoni nini kifanyike na njia za kupita zitengenezwe vipi,” amesema Komba ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Geita.

Katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa eneo la kituo cha mabasi mjini Geita, ameutaka uongozi wa halmashauri kuharakisha mchakato wa ujenzi wa kituo kipya cha mabasi eneo la Usindwake unakamilika.

Komba amesema wananchi wamechoka kusikia ahadi zisizotekelezwa za ujenzi wa kituo kipya.

Amesema kiu ya wananchi ni kuona kituo kipya cha mabasi kinajengwa kwa kuwa tayari fedha za ujenzi zimetolewa.

“Dhamira ya Serikali ni kuboresha mji wa Geita, tunajenga barabara kwa kiwango cha lami kilomita 17 kwa mradi wa Tactic na mradi wa pili ni ujenzi wa stendi, lazima tuwakumbushe watu wa halmashauri lazima muongeze kasi ujenzi ukamilike ili waondokane na adha hii ya muda mrefu,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mji wa Geita, Yefred Myenzi amesema tayari mchakato wa kumpata mkandarasi umekamilika na wakati wowote ujenzi wa kituo kipya cha mabasi kinachojengwa kwa gharama ya Sh14 bilioni eneo la Usindwake utaanza.

Related Posts