Serikali yapigia chapuo kilimo | Mwananchi

Iringa. Serikali imejenga uwezo wa wadadisi na wasimamizi wa utafiti wa kilimo 178 kutoka maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha sera na utekelezaji wa mipango endelevu inayolenga kukuza sekta ya kilimo, ufugaji, na uvuvi kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa chakula.

Hayo yamebanishwa na Mwananchi Digital leo wakati wa kufunga mafunzo ya siku 14 kwa wadadisi na wasimamizi wa utafiti wa kilimo kwa mwaka wa 2023/24 yaliyofanyika mjini Iringa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa, amesema sekta ya kilimo inaendelea kukua na kuchangia zaidi ya asilimia 26 ya pato la taifa, ikilinganishwa na sekta nyingine za uchumi.

“Hii ni dalili nzuri kwamba kilimo kinachangia kuongeza kipato cha Watanzania, hususan wale wanaoishi vijijini,” alisema Dk Chuwa.

Amesisitiza pia umuhimu wa utafiti huo kwa kueleza kuwa sekta ya kilimo inaajiri zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wenye uwezo wa kufanya kazi, hasa katika maeneo ya vijijini.

Dk Chuwa ameongeza kuwa utafiti huu ni muhimu si tu kwa kuimarisha uchumi wa nchi, bali pia kwa kuboresha maisha ya Watanzania, ikiwa ni pamoja na ajira zao na usalama wa chakula.

“Utafiti huu una umuhimu mkubwa kwa kuwa unatoa takwimu rasmi zinazohitajika katika kufanya maamuzi ya kuboresha sekta ya kilimo, mifugo, na uvuvi,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Kasimu Salumu Ally, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya serikali za Tanzania Bara na Zanzibar ili kuhakikisha kuwa takwimu zinazokusanywa zina ubora na usahihi unaohitajika.

“Takwimu ni nyenzo muhimu katika kuboresha uzalishaji na kuhakikisha usalama wa chakula. Tumefurahi kuona wadadisi na wasimamizi wakiwa na uwezo wa kukusanya, kuchambua, na kutumia takwimu kwa ufanisi zaidi,” amesema Ally.

Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo wadadisi na wasimamizi ili waweze kuchangia kwa ufanisi katika kuleta maendeleo endelevu kwenye sekta ya kilimo, mifugo, na uvuvi, na hivyo kukuza uchumi wa taifa.

Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDG) yanataka ifikapo mwaka 2030, dunia iwe imeondokana na baa la njaa.

Takribani watu milioni 690 duniani wanakabiliwa na njaa, na Tanzania kama sehemu ya dunia inatekeleza mikakati mbalimbali kuhakikisha uzalishaji wa chakula unaimarika, ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wadadisi na wasimamizi wa utafiti wa kilimo.

Akihitimisha mafunzo hayo, Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Anne Makinda, amewasisitizia wadadisi na wasimamizi umuhimu wa kuchangia maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha uzalishaji wa chakula cha kutosha kwa taifa na pia kwa kuuza nje ya nchi.

Amesema, wadadisi na wasimamizi wa utafiti wa kilimo wanatakiwa kujituma na kufanya kazi kwa weledi ili kutoa takwimu bora za kilimo, mifugo, na uvuvi zitakazosaidia kukuza na kuimarisha sekta hizi, na hivyo kulifanya taifa kujitosheleza kwa chakula na kuimarisha uchumi wake.

“Serikali imejizatiti kutumia rasilimali tulizonazo ardhi, mvua, na watu ili kuzalisha chakula cha kutosha na kujiendeleza kiuchumi,” amesema Makinda.

Aidha, Makinda aliongeza kuwa asilimia 53.4 ya Watanzania ni vijana wenye nguvu, lakini nguvu kazi hii inahitaji mwongozo wa takwimu ili kuelewa wanacholima na masoko yaliyopo.

Kwa mwaka 2023, mchango wa sekta ya kilimo katika pato la taifa ulikuwa asilimia 26.5, ambapo kilimo cha mazao kilichangia asilimia 16.1, mifugo asilimia 6.2, misitu asilimia 1.7, na uvuvi asilimia 2.5.

Mafunzo haya yamewanufaisha walengwa kama Paul Nondo, amesema kuwa mafunzo hayo yamewawezesha kufahamu maeneo ya kilimo na ufugaji yanayohitaji utafiti wa kina.

“Tunapokwenda kufanya utafiti, tunaangalia maeneo ya kilimo, mazao yanayolimwa, mifugo, na viumbe wa maji kama samaki,” ameeleza Nondo.

Related Posts