Mbeya. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) imezipa siku 90 taasisi 18 kuwasilisha mafao ya Sh4 bilioni ya wafanyakazi wao.
Akizungumza leo Alhamisi Novemba 7, 2024 na waandishi wa habari, Mkuu wa Takukuru mkoani humo, Maghela Ndimbo amesema hadi sasa tayari wameshafanya mazungumzo na waajiri kuhakikisha wanatekeleza maelekezo hayo.
Amesema kushindwa kufanya hivyo ni kinyume na sheria na taratibu, akieleza wanaamini miezi mitatu waliyotoa kwa makubaliano watatekeleza haki hiyo kwa wafanyakazi.
“Takukuru ilifanya kikao kazi Septemba pamoja na waajiri na Meneja wa NSSF, kwa ajili ya kuwekeana mikakati ya kumaliza changamoto ya madeni sugu na tukakubaliana wailipe ndani ya miezi mitatu,” amesema.
“Kutofanya hivyo ni kuiuka utaratibu na hatua zitachukuliwa, waajiri wana madeni sugu ya jumla ya Sh4 bilioni, hii ni baada ya uchambuzi wa mfumo ya uwasilishaji wa makato ya wanachama wa NSSF,” amesema Ndimbo ambaye hakuwa tayari kuzitaja taasisi hizo.
Mkuu huyo ameongeza kwa sasa taasisi hiyo imejipanga kutumia kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa kufuatilia kwa ukaribu waratibu, wasimamizi na wagombea kwa yeyote atakayehusika na viashiria vya rushwa kuchukuliwa hatua.
Amesema kwa kipindi cha uchukuaji na urejeshwaji fomu, Takukuru mkoani humo haikupokea malalamiko yoyote aidha kwa chama cha siasa wala mgombea na kuwaomba wananchi kufichua vitendo vyote vya rushwa.
“Katika uchaguzi huu tutafanya ufuatiliaji kwa wagombea na wapambe, vyama vya siasa kabla, wakati na baada ya uchaguzi, lakini kutoa elimu kuhusu madhara ya rushwa na kuchukua hatua,” amesema.
“Lakini pia kwa kipindi cha Julai hadi Septemba, Takukuru ilipokea jumla ya malalamiko 135, ambapo Halmashauri na Mahakama ziliongoza kwa kulalamikiwa zaidi,” amesema Ndimbo.
Kuhusu miradi ya maendeleo, Mkuu huyo amesema kwa kipindi cha miezi mitatu, walifuatilia miradi 51 yenye thamani ya zaidi ya Sh97 milioni, ambapo miwili kati ya hiyo Sh435 milioni ilikuwa na dosari na kuelekeza irudiwe.
Mmoja wa wananchi, Lucy Sinkala amesema zipo baadhi ya Taasisi ambazo hazifuati utaratibu katika kutekeleza haki za wafanyakazi, akiomba mamlaka kufuatilia na kuchukua hatua.
“Inaumiza sana, mtu anafanya kazi kwa uadilifu hadi anastaafu au pengine kuachishwa kazi lakini hapati stahiki zake alizokuwa anakatwa kwenye malipo yake, hili litazamwe zaidi haki itendeke,” amesema Lucy.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta) mkoani Mbeya, Lugano Bansilile amesema ni mapema kulifafanua suala la madai akieleza atalitolea maelezo baada ya kupitia barua zilizowasilishwa na watumishi wa taasisi husika.
“Ni jambo la msingi mtu kupata haki yake, nimesikia kuna barua zimefika ofisini kutoka kwa baadhi ya watumishi wa taasisi kuhusu mafao yao, hivyo naomba nizipitie kisha nitaeleza na hatima yake,” amesema Bansilile.