Tanzania kusaka wawekezaji wa Saudi Arabia

Dar es Salaam. Tanzania inatarajiwa kutumia siku tatu kutafuta wawekezaji kutoka nchi ya Saudi Arabia ambao watakuwa tayari kuweka fedha zao katika sekta saba ikiwemo mafuta na gesi ambayo bado haijanufaisha nchi ipasavyo.

Katika siku hizo tatu za kuzitangaza fursa za uwekezaji, ujumbe wa wafanyabiasha zaidi ya 100 ikiwemo watumishi mbalimbali wa Serikali utakuwa ni miongoni mwa wale watakaoshiriki katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Saudi Arabia, linaloandaliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), ambalo litafanyika Riyadh nchini Saudi Arabia mwezi ujao.

Akizungumza leo Alhamisi Novemba 7, 2024 na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri amesema lengo la jukwaa hilo ni kukuza biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi mbili hasa katika sekta za kilimo, ufugaji, ujenzi, mafuta na gesi, usafiri na usafirishaji, utalii na madini.

Jukwaa hilo litafanyika kuanzia Desemba 17 hadi 21, 2024, ambapo Teri anabainisha tukio hilo litakuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania na Saudi Arabia.

“Hadi Oktoba mwaka huu, Saudi Arabia imewekeza zaidi ya Sh169.37 bilioni nchini Tanzania, na imezalisha ajira 1,126 kupitia miradi zaidi ya 17 katika sekta za kilimo, huduma, usafirishaji, utalii, na miundombinu,” amesema Teri.

Mbali na hilo pia amesema Saudi Arabia imekuwa ikifanya juhudi za kubadilisha uchumi wake, hasa kwa kupanua uwekezaji katika kilimo na sekta nyingine huku akiweka bayana kuwa jambo hilo linaonyesha umuhimu kwa Tanzania kuchangamkia fursa hiyo kwa kushirikiana na Saudi Arabia wakati inapanua msingi wa uchumi wake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Maganga amesema lengo la safari hiyo ni kufungua fursa za masoko kwa bidhaa na huduma, kupanua mauzo ya nje ya Tanzania kwa Saudi Arabia hususan nyama ya ng’ombe na bidhaa za kilimo, na kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDI).

Maganga amesema uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni unaweza kuwa na faida kubwa hasa katika kuongeza ajira na mapato ya kodi.

“Lengo lingine muhimu ni kuanzisha ushirikiano kati ya biashara za Tanzania na Saudi Arabia katika sekta mbalimbali. Tanzania inafungua sekta mpya ambazo Saudi Arabia imepiga hatua kubwa kama mafuta na gesi na teknolojia nyingine,” amesema Maganga.

Tanzania inakadiriwa kuwa na futi za ujazo za gesi asilia trilioni 230, ingawa zilizothibitishwa mpaka sasa ni futi trilioni 57.5 kulingana na taarifa za Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi tayari imeanza kuchimba gesi katika visiwa vya Songosongo wilayani Kilwa, mkoani Pwani na eneo la Msimbati mkoani Mtwara.

Maganga amesema safari hiyo itatoa fursa kwa biashara za Tanzania kukua kwa kujifunza kutokana na uzoefu wa Saudi Arabia ikiwemo kutembelea maeneo mbalimbali ya viwanda ili kuboresha utendaji wao.

Related Posts