Dar es Salaam. Tanzania imepanga kuwafikia diaspora wafanyakazi milioni moja ifikapo mwaka 2028.
Pia inataka diaspora hao ambao ni Watanzania waishio ughaibuni kuchangia Dola 1.5 bilioni (sawa na Sh3.75 trilioni) ikiwa ni mara mbili zaidi ya wanazochangia sasa ambazo ni zaidi ya Dola 600 milioni (sawa na Sh1.5 trilioni).
Hayo yameelezwa Novemba 6, 2024 kwenye kongamano la kitaifa lililojadili uhamiaji wa wafanyakazi likilenga kukuza ajira salama na zenye staha kwa wahamiaji wa Kitanzania.
Mkurugenzi wa Huduma za Ajira katika ofisi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Joseph Nganga amesema kutokana na mchango wao, Serikali inapanga kuongeza idadi ya diaspora wafanyakazi.
Nganga aliyemwakilisha Waziri wa wizara hiyo, Ridhiwani Kikwete amesema ifikapo mwaka 2028 Serikali inataka kuwa na diaspora wafanyakazi milioni moja kutoka 500,000 waliopo sasa.
Amesema mkakati uliopo wa kufikia lengo hilo ni kuweka mazingira rafiki na fursa mbalimbali ili wote wanaokwenda ughaibuni waende kihalali.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 ilisema kwa kushirikiana na wadau wengine itaendelea kuboresha huduma kuwawezesha diaspora kupata huduma za kifedha, kushiriki katika uwekezaji, uanachama katika mifuko ya hifadhi ya jamii na mifuko ya bima ya afya.
Pia kuboresha mifumo ya utambuzi na ya usajili wa diaspora kidijitali ili kuwezesha upatakanaji wa takwimu sahihi za kufanikisha maamuzi ya kisera.
Tayari kumeanzishwa programu ya kifedha kwa Waafrika ijulikanayo Kuda ambayo huenda ikachochea ongezeko la kiwango cha fedha kinachotumwa Tanzania na diaspora kwa ajili ya shughuli mbalimbali, ikiwemo uwekezaji.
Programu hiyo inatangazwa baada ya Kuda kupewa leseni ya Mtoa Huduma za Malipo (PSP) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania, uhitaji wa kutuma fedha kutoka nje ya nchi unaofanywa na Watanzania wanaoishi ughaibuni umekuwa ukiongezeka na kwa mwaka 2021, kiasi cha fedha zilizotumwa Tanzania kilifikia Sh1.53 trilioni.
Taarifa ya Benki ya Dunia kuhusu mwenendo wa uhamiaji duniani (KNOMAD, 2024) inaonyesha Watanzania bado wanatuma kiasi kidogo cha fedha kutoka sehemu walipo.
Ripoti hiyo inazitaja Nigeria na Kenya kuongoza barani Afrika kwa kupokea kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwa raia wao walioko ughaibuni.
Ripoti inaonyesha hadi Desemba 2023, Diaspora wa Nigeria walituma Dola bilioni 19.5 (Sh53.04 trilioni) kwa nchi hiyo, ikiwa ndiyo kiwango kikubwa zaidi barani Afrika. Kiasi hicho ni zaidi ya robo ya jumla ya Dola bilioni 54 zilizopokewa na nchi 49 za ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kenya ilipokea makadirio ya Dola bilioni 4.2 za Marekani (Sh11.42 trilioni), huku Tanzania ikipokea makadirio ya Dola milioni 700 (Sh1.9 trilioni) kutoka kwa diaspora mwaka 2023.
Kwa Nigeria, sababu kubwa inatajwa kuwa ni idadi ya raia wengi wanaoishi au kufanya kazi nje ya nchi wanaweza kuwa raia wa Nigeria au wenye asili ya nchi hiyo.
Miongoni mwao wapo wenye ujuzi wa kitaalamu ambao wamepata nafasi katika soko la ajira ughaibuni.
Kwa Afrika, michango ya diaspora ni muhimu kwani inaweza kuzidi kiasi cha mikopo au misaada ya kimataifa kwa mwaka.
Ufanisi wa Kenya unachangiwa na maendeleo ya teknolojia ya malipo na utumaji fedha kidijiti, ambayo imeongeza kasi na kupunguza urasimu katika kupokea fedha kutoka nje.
Pia sehemu kubwa ya raia wa Kenya walioko ughaibuni ni wenye elimu ya juu na hufanya kazi za staha, hususan katika nchi za Ghuba, Ulaya, na Amerika Kaskazini.
Mbali ya hayo, Watanzania wameshauriwa wanapoondoka kwenda ughaibuni watumie njia halali na kufuata taratibu.
Mkurugenzi wa diaspora na fursa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Salvatory Mbilinyi wanaoondoka pasipo kufuata utaratibu ‘kujilipua’ wanakuwa katika hatari.
“Wengi wanafanya hivyo wakihisi wakifika Ulaya wametoboa kimaisha si kweli, wapo ambao wanarudi wamezeeka na kuishia kupoteza muda tu huko,” amesema katika kongamano hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Eco Scope na kufanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Amesema elimu zaidi inahitajika kwa vijana kuwaondolea dhana kwamba kwenda Ulaya ni kutoboa kimaisha.
“Kuna Wazungu wazaliwa wa huko na hawana kazi, hivyo kukimbilia Ulaya siyo kutoboa, utarudi umetoboka.
“Unajilipua unakwenda kule miaka 10; ukiwa huko huwezi kuoa, kukaa na familia. Sawa utapata pesa, lakini gharama za maisha nazo zipo juu, unaishia kupata pesa ya kula na kurudi umezeeka, unamkuta rafiki yako uliyemuacha hapa nyumbani ana maendeleo makubwa, vijana wetu, waelimishwe katika hili,” amesema.
Amesema wanaokwenda kwa njia ya panya huwa wanajifichaficha na hata wakiwa huko hawawezi kwenda ubalozini kujiandikisha na wengine wakienda hawawezi kurudi kutokana na namna walivyoondoka.
Mwakilishi wa sekretarieti ya kuzuia na kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu, Inspekta Celestine Makoba amesema wapo vijana wanoondoka nchini kinyemela na kwenda nje kwa lengo la kufanya vibarua.
“Wakifika huko na kupata changamoto ndipo wanaikumbuka Serikali, kuna mabinti 17 tumewaokoa Aprili ambao walipelekwa huko Kurdistan kwa kuahidiwa kazi, lakini ikawa tofauti.
“Kibaya zaidi kule hata ubalozi hatuna, hata hivyo tulifanikiwa kuwaokoa. Changamoto inakuja kwa wengi wanaoondoka kwa njia za panya huwa hawatoi ushirikiano kwenye ushahidi,” amesema.