Teknolojia kuongeza ubora, kupunguza upotevu wa mwani

Unguja. Changamoto ya wakulima wa mwani kutegemea jua kukausha zao hilo baada ya kuvuna, huenda likapata ufumbuzi baada ya kupatikana teknolojia ya kukausha ambayo itasaidia pia kuongeza ubora na kupunguza upotevu baada ya kuvunwa.

Uharibifu wa mwani na kukosekana kwa soko la uhakika ni kikwazo kwa wakulima hao, licha ya Zanzibar kuwa mzalishaji mkuu wa mwani ikizalisha takribani tani 170,000 kwa mwaka.

Wakizungumza wakati wa kukabidhi mashine hizo kwa vikundi viwili vya Pongwe Pwani na Bweleo, leo Novemba 7, 2024 baadhi ya wakulima wamepongeza hatua hiyo, wakieleza itawaokoa kutokana na athari wanazopata kwa sababu ya changamoto zinazowakabili.

“Mashine hizi zitatusaidia wakati wa mvua na kuzalisha mwani mwingi, wenye ubora unaokubalika kwenye soko. Tunashukuru kutuwezesha kuanza kulima kilimo hiki cha mwani,” amesema mkulima wa zao hilo kutoka Pongwe, Salama Abdalla.

Mkulima mwingine Safia Ali Khamis amesema wameanza kutambuliwa tofauti na ilivyokuwa zamani, hivyo wanatarajia kuendelea kujishughulisha na zao hilo ikiwa ni sehemu ya kujipatia vipato vya familia na kuchangia uchumi wa Taifa.

Mkurugenzi wa Mavunolab ambao wametengeneza mashine hizo kwa kushirikiana na Chuo cha Sayansi ya Teknolojia Karume (Kist), Waziri Rutha amesema lengo ni kupunguza upotevu wa mwani baada ya kuvuna.

Amesema wana imani kuwa kadri wakulima watakavyoendelea kutumia mashine hizo ndivyo wataendelea kupata mwani bora na kukuza vipato vyao.

Mwani ni zao la biashara linalotoa ajira kwa wanawake na wasichana. Sekta hiyo imeajiri zaidi ya watu 25,000 huku asilimia 85 ni wanawake.

Hata hivyo, wanazalisha zao hilo kwa njia ambazo si bora, wengi wakitegemea jua kukausha mwani, hivyo ikitokea mvua kiasi kikubwa huharibika.

“Sisi watu wa Mavunolab kwa kushirikiana na Chuo cha Karume tulipata ufadhili kutoka UNDP (Shirika la Kimataifa la Maendeleo), kuanza kufanya tafiti za kutengeneza mashine za kukaushia mwani kutumia umeme jua,” amesema.

Kutokana na hilo, Juni mwaka huu amesema lilianzishwa wazo kwa vijana 10 kutoka KIST waliotengeneza mashine nne zilizokabidhiwa kwa wakulima wa mwani zenye uwezo wa kukausha hadi kilo 200.

Mbali ya kukausha mwani mashine hizo zinakausha dagaa, karafuu na mbogamboga nyingine.

“Kwa sababu ya njia wanazotumia ubora wa mwani si mzuri hivyo kuwafanya wauze kwa bei ndogo, imani yetu ni kwamba mashine zitasaidia kuongeza ubora na kupunguza mavuno kupotea,” amesema.

Kwa sasa Serikali imetoa bei elekezi kuwa kilo moja ya mwani iwe Sh1,000.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mazao ya Baharini Zanzibar, Dk Salum Soud Hemed amesema

moja ya maeneo ya vipaumbele vya uchumi wa buluu ni sekta ya mwani.

“Kwa hiyo unapokuwa na chanzo cha ajira kinachogusa wanawake basi ni sehemu ya vyanzo vya ajira ambavyo vinahitaji kipaumbele cha hali ya juu,” amesema.

Amesema uzalishaji wa mwani kila siku unaongezeka na sasa Zanzibar ni ya kwanza kwa Afrika na ni miongoni mwa nchi tano zinazozalisha zao hilo kwa wingi duniani.

“Hata hivyo, tunajua zao hilo lina changamoto nyingi na moja ya utatuzi wake ndio huu, tunakabidhi na kuwa na njia mbadala ya kukaushia mwani, wakulima wamezoea kukaushia chini kwa kutumia jua, hii itasaidia kuongeza ubora na kupunguza upotevu,” amesema.

Kuacha kuanika mwani chini kutasaidia usiwe na uchafu na kubaki na ubora wake, hivyo kuongeza thamani yake.

Amesema matumizi ya mashine hizo zinazotumia nguvu za umeme jua yatapunguza utegemezi wa umeme kwa hiyo teknolojia hiyo ni rafiki kwa mazingira.

Kwa sababu mwani unatumika katika chakula, amesema kutumia teknolojia hiyo kunalinda afya ya mlaji.

“Hata ukimueleza mteja jinsi unavyoutunza na kukausha ni rahisi kumshawishi anunue, hususani masoko yanayolengwa ama kwa watalii au kuuza nje,” amesema.

Amesema wanatamani jitihada hizo zifike Pemba ili makaushio hayo yakawe chachu ya ongezeko la mwani.

Related Posts