Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), umeendelea na utaratibu wake wa kujengea uwezo wanawake viongozi katika Mamlaka za serikali za Mitaa ili waweze kuendeelea kubeba agenda ya usawa wa Kijinsia katika uongozi na kuwezesha wanawake wanaotarajiwa kuwa viongozi kujenga hoja zenye mtazamo wa kijinsia zitakazokubalika na wananchi
Mafunzo hayo ya siku mbili, yanawahusisha wanawake kutoka vyama mbalimbali vya siasa, kutoka manispaa za Dar es salaam, wilaya ya Kibaha na Chalinze mkoani Pwani na Morogoro, ambao wanajengewa uwezo juu ya umuhimu wa ushiriki wa wanawake kwenye nafasi za uongozi, masuala muhimu ya kijinsia ya kufanyia kazi wakati wa kuandaa mipango ya bajeti, miongozo na ushiriki wa wanawake kwenye kamati za ardhi, shule, bodi za shule, kamati za zahanati na kamati za vituo vya afya.
Aidha, wamejengewa uwezo juu ya ujenzi wa nguvu ya pamoja kama wanawake ili waweze kushikamana na kuwezesha wanawake wengi zaidi kushiriki kwenye nafasi mbalkimbali za uongozi ili kusimamia ajenda ya maendeleo shirikishi kwa wote.