Dar es Salaam. Donald Trump amekuwa kikwazo kwa wagombea wanawake kuingia Ikulu ya White House, ndivyo unavyoweza kusema kutokana na ushindi wake dhidi yao anapogombea nao.
Bilionea huyo kutoka Jiji la New York amegombea urais mara tatu, mwaka 2016, 2020 na 2024. Katika awamu alizogombea, ameshinda mara mbili na amepoteza mara moja.
Trump amekuwa Rais wa pili wa Marekani kushinda urais katika awamu mbili tofauti. Yeye ni Rais wa 45 wa Marekani na pia ndiye Rais Mteule wa 47 wa Taifa hilo lenye nguvu duniani.
Wa kwanza kuweka rekodi hiyo alikuwa Grover Cleveland aliyekuwa Rais wa 22 wa Marekani kati ya mwaka 1885 -1889 na pia Rais wa 24 kati ya 1893 -1897.
Hivyo, Marekani imeongozwa na marais 45 tu kuanzia kwa George Washington aliyeanza mwaka 1789 – 1797 hadi wakati huu wa Trump ambaye atahitimisha miaka yake minne 2028 na baada ya hapo hataruhusiwa kugombea tena.
Katika historia ya Marekani, wanawake wawili wamejitokeza kugombea urais katika Taifa hilo lenye jumla ya watu milioni 334.9 na katika nyakati wanazojitokeza, wanakutana na Trump ambaye amekuwa mwiba mkali kwao.
Tukirejea uchaguzi wa Novemba 8, 2016, Trump aliyewakilisha chama cha Republican, alishindana na Seneta Hillary Clinton, ambaye alikuwa mke wa Rais wa 42 wa Marekani, Bill Clinton na Waziri wa Mambo ya Nje wakati wa utawala wa Rais Barack Obama.
Katika uchaguzi huo uliokuwa na msisimko mkubwa, huku Hillary akipewa nafasi kubwa ya ushindi, Trump alishinda kwa kura za majimbo 306 dhidi ya Hillary aliyepata kura 232, na hivyo akawa Rais wa 45 wa Marekani.
Licha ya kupoteza katika kura za majimbo ambazo ndizo huamua mshindi, Hillary alipata kura nyingi za wananchi (popular votes) akiongoza kwa kura 65,853,514 sawa na asilimia 48.2, wakati Trump alipata kura 62,984,828 sawa na asilimia 46.1.
Kutokana na matokeo hayo, Hillary aliyepata uungwaji mkono na makundi mbalimbali ya watu mashuhuri, alipoteza fursa ya kuweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kuliongoza Taifa hilo lenye nguvu za kiuchumi, kijeshi na kiteknolojia duniani.
Uchaguzi wa mwaka 2020, Trump aligombea muhula wa pili dhidi ya Joe Biden. Hata hivyo, Trump alipoteza kwenye uchaguzi huo na Biden ambaye alikuwa Makamu wa Rais wakati wa utawala wa Obama, akawa Rais wa 46 wa Marekani.
Trump hakukata tamaa, alikaa benchi miaka minne na kurejea tena kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi akitaka kuhitimisha muhula mmoja uliobakia kwa mujibu wa Katiba ya Marekani.
Katika uchaguzi wa mwaka 2024, alikuwa amkabili Biden lakini kwa sababu zilizokuwa dhahiri, Biden alitangaza kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho na kumpisha Makamu wake, Kamala Harris.
Hiyo ilikuwa fursa nyingine kwa wanawake kuitafuta Ikulu ya Marekani, hata hivyo ilikwamishwa na Trump yuleyule aliyemkwamisha Hillary mwaka 2016.
Katika uchaguzi wa Novemba 5, 2024, Trump amepata ushindi mkubwa dhidi ya Harris, hivyo kuhitimisha jaribio jingine la mwanamke kuitafuta Ikulu na kufanya uamuzi kwa niaba ya wananchi katika ofisini ya kihistoria inayojulikana ‘Oval Office’.
Matokeo yaliyotolewa jana Novemba 6, 2024 yanaonyesha Trump amepata kura za majimbo 295 wakati Harris amepata kura 226, hivyo Trump kuibuka kidedea akirejea White House kwa kishindo baada ya miaka minne tangu alipotoka Ikulu.
Tofauti na ilivyokuwa mwaka 2016, safari hii Trump ameongoza pia kwa kura za wananchi, amepata kura 73,523,637 sawa na asilimia 50.92 wakati Harris akipata kura 68,683,845 sawa na asilimia 47.5.
Kwa matokeo hayo, mwanamke mwingine aliyepata fursa hiyo anakwamishwa na Trump na kuendelea historia ya siasa za Marekani kama ilivyo katika mataifa mengine mengi duniani kuongozwa na wanaume.
Kumekuwa na maoni tofauti kuhusu ushindi wa Trump na Harris kupoteza uchaguzi huo licha ya kwamba alionekana kuwa na mvuto na kura nyingi za maoni zilionyesha akiwa mbele ya Trump kwa kiwango kikubwa.
Baadhi ya wachambuzi wanaeleza jamii ya Wamarekani bado haijawa tayari kuongozwa na mwanamke, hivyo kura zao zimemwangukia Trump moja kwa moja kama mgombea mwanaume kwenye nguvu kwenye uchaguzi huo.
Licha ya mitanzamo hiyo, bado dunia inaendelea kupigania usawa wa kijinsia katika nyanja zote ili kuhakikisha wanawake pia wanashiriki kwenye uongozi wa juu ikiwemo nafasi ya urais kama ilivyo kwa wanaume.
Harris amebaki na rekodi yake ya kuwa mwanamke wa kwanza wa Marekani kuwa Makamu wa Rais. Kwa umri wake wa miaka 60 sasa, bado ana nafasi ya kugombea tena katika chaguzi zijazo endapo atapewa nafasi hiyo na chama chake.