Dodoma. Ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa Marekani umeibua mgawanyiko ndani ya Chama cha Democratic, wakishutumiana kusababisha kushindwa kwenye uchaguzi huo na Republican.
Wengine wanamlaumu Rais Joe Biden kwa kujitoa katika kinyang’anyiro wakati usio muafaka, hatua wanayoamini iliongeza mzigo kwa chama hicho kongwe nchini Marekani kilichoanzishwa mwaka 1828.
Katika uchaguzi wa Novemba 5, Trump alijipatia kura za majimbo ‘electoral college’ 295 dhidi ya Kamala Harris aliyepata 226, hali iliyosababisha hasira na lawama miongoni mwa wanachama wa Democrat.
Chama hicho kilishindwa si kwenye nafasi ya urais pekee, bali pia kwenye seneti, baraza la wawakilishi, na nafasi za ugavana dhidi ya Republican, chama kilichoanzishwa mwaka 1854.
Baadhi ya wanachama wanaamini uamuzi wa kumteua Kamala kuwa mgombea ulikuwa dhaifu na umekigawa chama hicho kisiasa na kimtazamo.
Mwigizaji na mfadhili wa kampeni za Rais Biden, George Clooney (63), ametupiwa lawama kwa kumshinikiza kiongozi huyo kujitoa kwenye kinyang’anyiro cha urais bila kusoma alama za nyakati.
Clooney, aliyewezesha kukusanya Dola milioni 30 kwa kampeni za Biden, alieleza kiongozi huyo hakuwa na nafasi ya kushinda kutokana na changamoto za kiafya, kimwili na kiakili, ambazo zilionekana wazi katika mdahalo kati yake na Trump.
Julai 10, kupitia jarida la New York Times, Clooney alimshauri Biden ajiondoe kwa kusema: “Hawezi kushinda uchaguzi wa Novemba.”
Clooney aliwalaumu viongozi wa Democrat kwa kupuuza viashiria muhimu vinavyohusiana na afya ya Biden, akisisitiza kutomwondoa mapema kulikiweka chama hicho katika nafasi mbaya zaidi.
Julai 21, siku 107 kabla ya uchaguzi, Biden alitangaza kujitoa na Clooney alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kumpongeza kwa uamuzi huo, akiamini Kamala angeweza kumshinda Trump kwenye uchaguzi.
Hata hivyo, uteuzi wa Kamala umegawanya zaidi chama, kwani wengi wanahisi hakuwa na uwezo wa kushawishi wapigakura ipasavyo.
Wakosoaji wanasema Kamala alikosa ujasiri katika kampeni na kushindwa kutumia fursa kujenga imani kwa wapigakura.
Pia wanasema Kamala alijikuta katika hali ngumu kwenye mahojiano ya televisheni, kwa kuonyesha kutojiamini na changamoto za mbinu za kuzungumza.
Wafuasi wa Democrat wameelekeza lawama kwa mgombea wao Kamala, wakieleza mapungufu yake kadhaa katika kampeni hizo.
Kamala ameonekana kama mgombea mwenye udhaifu aliyeshindwa kuhimili shinikizo la kampeni na kuungana kikamilifu na wapigakura.
Wakosaji wanasema kutokana na ukosefu wa uzoefu na mbinu za mawasiliano, aliepuka mahojiano muhimu na waandishi wa habari, jambo lililowaacha wengi na maswali juu ya uwezo wake.
Kwa mujibu wa wakosoaji wiki tatu za kwanza za kampeni zilikuwa ngumu kwake, kwani hakuwa na mahojiano yoyote na alionekana kutojiamini wakati akihojiwa na CNN Agosti 29 akiwa na mgombea mwenza, Tim Walz.
Hali hiyo ilitafsiriwa na wakosoaji kuwa ni ishara ya kutokuwa na uhakika katika masuala anayoyasimamia.
Mahojiano mengine ya Septemba kwenye kituo cha ABC huko Pennsylvania, Kamala alionekana kuwa na timu ya kampeni karibu yake, hali iliyodhihirisha alikuwa na hofu ya kukosea, ikichukuliwa na wakosoaji kama dalili ya kutokuwa na msimamo thabiti.
Siku moja kabla ya kupiga kura, mpigakura kutoka New Hampshire, Jim Olivera, alinukuliwa akisema Kamala alikuwa kama anayeelekezwa nini cha kusema.
Hali hiyo ilichochea mashaka kuhusu uhalali wa msimamo wake na uaminifu kwa wapigakura, ikihusisha mapungufu yake katika kampeni kama moja ya sababu za kushindwa kwake katika uchaguzi.
Wakosoa matumizi ya lafudhi
Kamala, mwenye asili ya Jamaica na India, amekosolewa kwa kubadilisha lafudhi hadharani kulingana na eneo na hadhira, jambo lililoibua maswali kuhusu uhalisia wake kama mgombea.
Wapigakura nchini Marekani walimwona Kamala kama anayebadilisha sauti na mtindo wa kuzungumza ili kujipendekeza kwa hadhira tofauti na mpinzani wake, Trump ambaye alihusishwa na uhalisia.
Kwa mfano, wakati wa hotuba kanisani Philadelphia, Pennsylvania, Kamala alidhihakiwa kwa kutumia lafudhi iliyoonekana kama ya kasisi, kitendo kilichotafsiriwa kuwa ni mbinu ya kujitafutia umaarufu katika jamii.
Septemba, Kamala alikumbana na ukosoaji zaidi alipobadili lafudhi alipozungumza na wapigakura huko Detroit, Michigan ili kuonekana anaelewana na wafanyakazi wa eneo hilo.
Wakosoaji waliona mabadiliko hayo ya lafudhi kama kitu feki na kiashiria cha kukosa msimamo thabiti, hali iliyowakatisha tamaa baadhi waliotarajia uthabiti zaidi kutoka kwa mgombea.
Mmoja wa wakosoaji alieleza mabadiliko ya lafudhi yalionekana kuwa ya maonyesho, Kamala akijitahidi kwa kiasi kikubwa kujipendekeza.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa kampeni, mbinu hiyo ilimpa taswira ya kutokuwa na uhalisia na baadhi ya wapigakura walihisi hakuwa na msimamo wenye nguvu.