WAANDISHI WA HABARI WAPIGWA MSASA KUELEKEA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MTAA

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Kuelekea uchaguzi wa serikali ya za mitaa,Waandishi wa Habari nchini wametakiwa kutumia weledi, maadili, sheria na miongozo ya taratibu za uchaguzi katika kuandika Habari za uchaguzi wa serikali za mitaa huku wakitoa haki kwa vyama vyote vya siasa nchini.

Hayo yamesemwa leo Novemba 7,2024 Jijini Dodoma na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Maelezo kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Serikali Zamaradi Kawawa wakati akifungua semina ya siku mbili ya kuwajengea uwezo waandishi wa Habari kuandika Habari za uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka 2024 iliyoandaliwa na mtandao wa mashirika yanayotoa msaada wa sheria Tanzania (TANLAP).

“Tunatarajia kuwa vyombo vya habari vitaripoti mchakato mzima wa kuelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa ikiwemo Kampeini na matokeo ya uchaguzi kwa kuzingatia weledi, maadili, sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya uandishi wa Habari, na uchaguzi katika nchi yetu,”amesema.

Pia amewahimiza kujitahidi katika utekelezaji wa majukumu yao kuwa na malengo ambayo yataangazia maslahi ya nchi na watakachokiripoti kiwe kinachochea amani na utulivu na sio kuleta vurugu na uvunjifu wa amani.

Akitoa elimu kuhusu uandishi wa Habari za Uchaguzi Meneja wa huduma za utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA), Mha. Endrew Kisaka amewasisitiza waandishi kutopendelea chama chochote ikiwa ni pamoja na kuzingatia usawa wakati wa kuwasilisha taarifa.

“Mkiwa kwenye vipindi msipendelee chama chochote na mnapoandaa midahalo hakikisheni wagombea wanasema sera zao na siyo kumsema mtu au kusema chama kingine,”amesema Mha. Kisaka.

Awali akitoa salamu Mkurugenzi wa mtandao wa mashirika yanayotoa msaada wa sheria Tanzania (TANRAP) Christina Luhinda amesema kuwa mtandao huo umeweka wanasheria maalumu wa kuangalia mambo ya ukatili wa kijinsia katika uchaguzi wa serikali za mitaa wanaofanyiwa baadhi ya makundi yakiwemo Wanawake,Vijana na watu wenye ulemavu.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (Tamisemi), Ntenghenjwa Hoseah akiwasilisha kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 amesema uchaguzi huo unaongozwa na kanuni Nne zilizopo kwenye tangazo la serikali na. 571,573, 574  na 572 la mwaka 2024.

“Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI ambaye ndiye mwenye dhamana ya uchaguzi atatakiwa kutoa tangazo la uchaguzi litakaloainisha ratiba ya uchaguzi, shughuli zinazohusiana na uchaguzi na masharti muhimu ya uchaguzi, “amesema.

Related Posts