Wakulima wadogo wa mpunga watakiwa kutumia wataalamu kuboresha uzalishaji

Na Esther Mnyika, Pwani

Wakulima wadogo wa mpunga nchini wametakiwa kushirikiana na wataalamu wa kilimo walioko kwenye ngazi ya vijiji na kata, ikiwemo maafisa kilimo na maafisa ugani, ili kuimarisha kilimo chao tangu hatua za awali na kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa zao hilo.

Mkuu wa Divisheni ya Kilimo na Uvuvi wilaya ya Bagamoyo, Gerald Mwamuhamila, alitoa wito huo Novemba 6, 2024, wakati akifunga mafunzo ya uzalishaji wa mbegu bora za mpunga yaliyotolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mpunga (IRRI). Mafunzo hayo yaliandaliwa kwa vikundi 13 vya uzalishaji mbegu kutoka mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuboresha kilimo cha mpunga nchini.

“Walichojifunza hapa ni kwa niaba ya wakulima wote nchini; tunawasihi waendelee kubadilishana uzoefu na wataalamu waliopo katika maeneo yao ambao ni madaktari wa mazao,” alisema Mwamuhamila.

Afisa Utafiti wa Mifumo ya Mbegu kutoka IRRI, Martine Ndomondo, alifafanua kuwa mafunzo hayo yaliwalenga hasa wanawake ili kuwawezesha kiuchumi kupitia kilimo cha kisasa. Aidha, Beatrice Swai wa Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) aliwataka wakulima waliopata mafunzo hayo kutumia ujuzi huo kuwanufaisha wenzao kwa kuwashirikisha maarifa waliyojifunza.

Washiriki kutoka mikoa ya Mbeya na Rukwa walieleza kufurahishwa kwao na mafunzo hayo, wakisema kuwa yatawawezesha kuachana na kilimo cha mazoea na kufuata mbinu bora zaidi za kilimo. Mafunzo hayo yaliwashirikisha jumla ya wakulima 35 kutoka vikundi mbalimbali vya uzalishaji mbegu nchini.

Related Posts